Header Ads

NNAUYE TAZAMA ULIPOTOKA,ULIPO NA UNAPOKWENDWA


Na Happiness Katabazi

“TEMBEA pole pole kama Kobe eeh… akinywa maji lazima ainuie kichwa juuu.” Hayo ni baadhi ya maneno yanayopatikana kwenye wimbo wa Kizimungala uliopo kwenye albamu ya ‘Dunia Kigeugeu’ ya bendi maarufu ya muziki wa dansi nchini ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma.’


Nimelazimika kutumia nukuu ya maneno hayo machache yanayopatikana kwenye kibao hicho cha Kizimungala kwa sababu naamini kabisa maneno hayo machache na mengine yatakayoendelea kwenye makala hii yanafikisha ujumbe uliomo katika makala hii.

Watanzania wote hususan wale wanaofuatilia mustakabali wa masuala ya kisiasa hapa nchini, watakumbuka hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete aliendesha vikao vya chama chake mjini Dodoma.

Wakati akiendesha vikao hivyo Rais Kikwete alitangaza kuivunja sekretarieti ya chama hicho kwa madai kuwa imeshindwa kumsaidia kazi tangu alipoiunda miaka michache iliyopita.

Waliokuwemo kwenye sekretarieti iliyovunjwa ni Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Katibu wa Uchumi na Fedha, Amos Makalla, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu, George Mkuchika na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje , Bernad Membe.

Na alipoivunja aliwaacha wote na kumchukua John Chiligati kumpatia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu katika sekretalieti ya sasa, Katibu Mkuu ni Willson Mkama, Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje, Januari Makamba na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi ni Nape Nnauye na Mweka Hazina ni Mchemba.

Hakuna ubishi tangu mwenyekiti wa chama hicho alipoiunda rasmi sekretarieti mpya, mara kwa mara tumekuwa tukimsikia Nnauye kwenye vyombo vya habari akinukuliwa akisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC ) kimetoa siku 90 kwa watuhumiwa wa ufisadi wajivue madaraka, chama kimezaliwa upya na kadhalika.

Kwa hakika kasi ya Nnauye ya kutoa matamko kwenye vyombo vya habari imekuwa kubwa ukilinganisha hata ile ya wajumbe wenzake wa Sekretarieti.

Binafsi naya fahamu majukumu ya Katibu Mwenezi kwenye vyama vyote vya siasa. Na nina fahamu uhuru wa mtu yeyote, akiwemo Nape mwenyewe kutoa maoni yake kama wanavyoruhusiwa na Ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Na moja ya kazi ya katibu mwenezi katika chama ni kuwa mshereheshaji katika mikutano ya hadhara ya chama husika.

Ninavyojua mimi chama chochote makini cha siasa uwa kinatoa ahadi kwa wananchi kuhusu jambo fulani kwamba kitatekeleza na kabla hakijatoa ahadi kwa umma au kwa wananchama wake ni lazima vikao husika vimeketi vimelipisha hilo na ahadi hiyo imeandikwa kwenye miniti za vikao husika.

Na si leo hii tunavyoona vioja vinavyofanywa na baadhi ya vyama vya siasa kusimama majukwaani kusema vitatekeleza hili na lile wakati hata kwenye ilani za uchaguzi wa vyama vyao hakuna na hata kwenye kumbukumbu za vikao vyao vya juu hakuna. Ni uhuni na uzandiki wa kupindukia.

Sasa kuhusu kasi ya Nnauye kuzungumza kwenye vyombo vya habari kwa kasi tena kwa kipindi hiki kifupi, sisi wachambuzi wa mambo tumeanza kujiuliza kichini chini hivi anafahamu kuwa yote anayoyazungumza kupitia vyombo vya habari wananchi wanayarekodi kwenye vitabu vyao vya kumbukumbu?

Na siku ikifika hayo anayoyasema yasipotekelezwa na chama chake, waananchi watawabana kwamba ni kwanini chama chake kimeshindwa kutekeleza yale yote anayoyasema kwenye vyombo vya habari hivi sasa?

Kama yote anayonukuliwa kwenye vyombo vya habari hivi sasa yapo kwenye rekodi za vikao vya chama hicho, basi mwisho wa siku hata kama hayatatekelezwa basi mwanasiasa huyo anaweza akasalimika kisiasa, ila kama hizo ahadi hazipo kwenye rekodi za vikao vya CCM, ila yeye kupitia wadhifa wake ameamua kuyazungumza kwa kuwa chama kimezaliwa upya, basi wakati ukifika wanachama wa CCM watamfuata kutokana na matamko yake ambayo hayakuwa yametekelezeka.

Mabadiliko ya uongozi wa juu wa chama hicho yaliyofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho na matamko ya Nape kwenye vyombo vya habari yamebadilisha upepo mbaya uliokuwa ukivuma ndani ya chama hicho.

Chama hicho kilikuwa kikiandamwa na wakosoaji wa masuala ya kisiasa kwamba ni chama kilichozeekana na kimekosa dira na kwamba baadhi ya viongozi wake wamefilisika kisiasa.

Na wakati wote tuhuma hizo zimekuwa zikirushiwa chama hicho chenye makada wake ambao wana mafunzo na mbinu za kila aina za kuweza kukabiliana na mikikimiki ya wapinzani wake, lakini kwa kipindi chote hicho chama hicho kilishindwa kujipanga vema na kuweza kujisahihisha hadi heshima yake kuporomoka mbele ya jamii.

Ila siwezi kusema moja kwa moja chanzo cha kuporomoka kwa heshima ya chama hicho chanzo ni sekretarieti iliyopita.

Hata baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM ngazi ya matawi, kata, wilaya na mikoa nao walikuwa chanzo kikubwa cha tatizo hilo kwani baadhi ya matendo yao, uzalendo wao kwa wananchi wenzao na wale wafuasi wa vyama vingine ulikuwa ukilalamikiwa kila kukicha.

Sasa kuhusu Nape, akumbuke kipindi kile alichokuwa akiungurumisha kile alichokiita ni ufisadi katika upangishwaji wa jengo la UVCCM kwa mwekezaji, ambapo alidai kuna ufisadi katika upangishwaji wa jengo hilo na matokeo ya madai yale aliyapata kutoka katika vikao vya UVCCM.

Kwa hiyo basi hana budi kutazama alikotoka, alipo na anakokwenda. Ningefarijika kukuona Nnauye unatumia muda mwingi kubuni mbinu thabiti ya kukinadi chama na hiyo idara yako kujipanga upya kwa kuandika maombi ya fedha kwa mweka hazina wenu za kuandaa mafunzo au semina hata ya wiki moja ya makatibu wenezi wa mikoa yote na wilaya maana wewe ni ndiye kiongozi wao ukawaeleza umejipanga vipi na wewe unataka wafanye nini na waache kipi ili mwendelee kukijenga chama chenu, badala yake karibu kila kukicha tunakusikia kwenye vyombo vya habari ukitueleza yale yale mliyoyajadili kwenye chama ya kujivua gamba.
Nilitegemea Nnauye sasa hivi uwe unaumiza kichwa kwa kubuni mkakati ule wa chama chenu mliouasisi miaka ya nyuma ya kuwa na chipukizi wengi kutoka mikoani na kwenda kuimarisha matawi ya chama chenu kwenye vyuo vikuu sambamba na kujenga nguvu za hoja zitakazowashawishi wana vyuo vikuu ambao wamekitema chama chenu na kujiunga kwa wingi na Chadema.

Nilitegemea Nnauye na UVCCM sasa hivi na nyie mngeanzisha mitandao mbalimbali na kuanza kukinadi chama na kuonyesha kwa miaka sita hii ya utawala wa Rais Kikwete amefanya nini, ameshindwa wapi na ana kusudia kufanya nini kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010?

Wakati mwingine huwa najiuliza, hivi hiyo mishahara na posho wanayopewa na chama pamoja na kutanua na magari ya kifahari kila kukicha na matokeo yake wanashindwa kukitetea chama kwa yale mazuri waliyofanya na kuweka bayana udhahifu ili kesho na kesho kutwa wasirudie udhahifu huo, wanalipwa za nini?

Matokeo yake hivi sasa tumekuwa tukiona nguvu ya vijana wa chama hicho ikitumika kwa nguvu zote nyakati za uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Hii ni kasumba ambayo ndiyo sasa inaanza kuwatafuna vijana wengi wa nchi ambao hata wengine hawana hadhi ya kuwa viongozi lakini wanajitumbukiza kwenye ulingo wa siasa kwa lengo moja tu la kupata madaraka harakaharaka na si kuvitumikia vyama vyao na taifa kwa ujumla.

Ikiwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) si chama tawala na hakina ruzuku kubwa kama CCM, kwa kipindi kifupi tu kimeweza kuwa na viongozi vijana hata ndani ya vyuo vikuu wenye uthubutu wa kulisimamia lile wanaloliamini, inakuwaje CCM vijana wake wawe goigoi na wawe mabingwa wa kutoa matamko wakati wa chaguzi za ndani zinapofika?

Binafsi nilishawahi kuandika makala zaidi ya nane huko nyuma kuitahadhalisha CCM ijitazame upya na isome alama za nyakati kwamba Watanzania wa sasa si wa jana na kweli hivi karibuni chama hicho kikaamua kukikiri kwamba tuhuma za ufisadi zimekiathiri, lakini kukiri tu hakutoshi tunataka kama kweli kuna wanachama wake wana tuhuma za aina hiyo basi wafikishwe kwenye vyombo vya dola kama wengine licha ya kuwa hayo ni maamuzi ya chama chenyewe na sisi watu wa nje hatupaswi kuyaingilia.

Tungali tukikumbuka Nyerere Foundation miaka miwili iliyopita ilifanya mdahalo wake pale ukumbi wa Karimjee na washiriki ambao wengi walishawahi kushika nyadhifa za juu serikalini waliikosoa wazi wazi serikali na kusema kwamba inakabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Lakini kwa kuwa siku hazigandi, Aprili mwaka huu, kwenye kikao cha NEC Rais Kikwete na wajumbe wa mkutano huo walikiri wazi wazi kwamba upepo wa kisiasa dhidi ya chama chao ni mbaya sana, kwani tuhuma za ufisadi zinazowakabili viongozi wake nazo zimechangia chama hicho kupatwa na msukosuko wa kisiasa na hivyo kuwataka wanachama wanaokabiliwa na tuhuma hizo wajivue madaraka.

Sasa tuwahoji wale makada wote waliojitokeza kuwakebehi kina Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku kuwa ni wazi, leo hii wanaziweka wapi sura zao? Maana mwenyekiti wao amekiri kashfa za ufisadi zimekipaka matope chama chao.

Kwa hiyo nimalizie kwa kumuasa Nnauye kwamba cheo ni dhamana, asikubali kutumika kuwaumiza wenzie na kwamba kuna msemo usemao: “Yaliyomkuta mamba na kiboko yatamkuta” kwa sababu wote wanaishi majini.

Hivyo yaliyoikuta Sekretarieti na Kamati Kuu iliyopita mwisho wa siku yanaweza kuikuta hata sekretatieti ya sasa, kwani tungali tukikumbuka mwaka 2006 aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa alistaafu wadhifa huo kabla ya muda wake kule Dodoma na akamkabidhi kiti Rais Kikwete, ambaye dakika chache baada ya kukabidhiwa kiti aliichagua sekretarieti mpya ambayo iliundwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Naibu Katibu Mkuu, Jaka Mwambi, Mweka Hazina, Rostam Aziz, Mambo ya Nje, Dk. Asha-Rose Migiro, hivyo kuiacha sekretarieti ya Mkapa ambayo Katibu Mkuu alikuwa Philip Mangula, Naibu Katibu Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Katibu wa Itikadi na Uenezi , Omar Ramadhani Mapuli na Mweka hazina marehemu Salome Mbatia.

Sote tunamkumbuka aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, enzi za Mkapa. Mangula alikuwa si aina ya kiongozi wa kupayuka payuka na kuzungumza ovyo ovyo na vyombo vya habari kama alivyokuwa Yusuf Makamba.

Tuliokuwa kwenye fani ya uandishi wa habari enzi zake ni mashahidi kwamba siku CCM ikitoa mwaliko kwa vyombo vya habari kwamba Katibu wake Mangula siku fulani atazungumza na waandishi wa habari, basi wahariri ndani ya vyumba vya habari nao hujipanga kwa kumwandaa mhariri au mwandishi mwandamizi makini ambaye pia wanamwandaa na kumpatia maswali ya kumuuliza katibu mkuu huyo. Na katika hili tutabaki tukimkumbuka Mangula.

Na kama Nnauye asipokuwa makini na kuikwepa sifa hiyo mbele ya safari itakuja kumghalimu.

Kwa mifano hai hiyo, Nape unapaswa uzifahamu vyema siasa za chama chako zikoje kwamba ni za kupanda na kushuka, tena wakati mwingine unashuka kwa ajili ya mizengwe na uzushi na matamanio ya kisiasa ya wakati huo, kuliko hali halisi au kutibu tatizo.

Hivyo Nnauye , January na Mchemba mtambue bado mna maisha marefu kwenye ulingo wa siasa hapa nchini, kama mtapenda hivyo ni vyema mjiepushe kujiingiza au kuingizwa kwenye magomvi binafsi na wakubwa wenu ambayo yamepewa misamiati ya kila aina.

Watanzania na wanachama wa chama chako wanataka kuona una fanyakazi kwa vitendo na si maneno majukwaani na kwenye vyombo vya habari.

Kama kweli NEC iliazimia viongozi hao wajivue nyadhifa zao na azimio hilo likaandikwa kwenye kumbukumbu za kikao hicho, basi ni wakati mwafaka sasa wananchi kusubiri hizo siku 90 zifike tuone kama kweli watu hao watakuwa wameishajivua madaraka na hilo likishindikana, basi Nape na viongozi wenzake wa chama chake tutawaweka kwenye kapu lilelile la viongozi wanaopenda kusema majukwaani, lakini utendaji ni sifuri.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 26 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.