Header Ads

NG'UMBI AAMRILIWA KULIPA MIL 9/-

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwamuru imemwamuru aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo (CCM), Hawa Ng’umbi kulipa jumla ya Shilingi milioni tisa ndani ya 14 kuanzia jana fedha ambazo ni dhamana ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza John Mnyika (Chadema) kuwa mbunge wa jimbo hilo .


Mbali na Mnyika , Ng’umbi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe katika kesi hiyo anamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ambapo Mnyika anatetewa na wakili wa kujitegemea, Edson Mbogoro. Ng’umbi ambaye anatetewa wakili Issa Maige alifungua kesi hiyo Na. 107/2010 Machi 22 mwaka huu, akitaka mahakama hiyo itengue ushindi wa Mnyika kwa sababu sheria ya uchaguzi ilikiukwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Upendo Msuya ambapo alisema alisikiliza kwa makini ombi la mlalamikaji(Ng’umbi) la kutaka apunguziwe kiwango cha kulipa dhamana ya kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002 inamtaka mlalamikaji alipe sh milioni tano kwa kila anamshtaki na kwamba alisikiliza hoja za mawakili wa wadaiwa zilizowasilishwa na Mbogoro ambazo zilitaka ombi la mlalamikaji litupwe kwasababu mlalamikaji ni mkuu wa wilaya na ana uwezo wa kifedha wa kuweza kulipa sh milioni 15 na kwamba mlalamikaji hakutoa vielelezo vinavyoonyesha yeye hana uwezo wa kulipa shilingi milioni 15.

Jaji Msuya alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili amebaini kuwa Ng’umbi ameshindwa kuleta vielelezo vinavyoonyesha kuwa hana uwezo wa kiuchumi ambao haumruhusu kulipa dhamana ya shilingi milioni 15 hivyo mahakamana hiyo inamwamuru kulipa shilingi milioni tatu kwa kila mdaiwa ambayo jumla yake ni shilingi milioni tisa badala ya milioni 15 na kwamba fedha hizo anapaswa awe ameziliwakilisha mahakamani hapo ndani ya siku 14 kuanzia jana.

“Ng’umbi ameshindwa kuleta vielelezo vinavyounga mkono ombi lake la kutaka apunguziwe dhamana ya shilingi milioni 15 na kwa maana hiyo mahakama hii inamwamuru mlalamikaji huyo alipe shilingi milioni tatu kwa kila mdaiwa na fedha hizo anatakiwa azilipe ndani ya siku 14 kuanzia leo(jana) kama Sheria ya Uchaguzi ya Taifa ya mwaka 2002 inavyotaka.”alisema Jaji Msuya.

Aprili nane mwaka huu,Wakili wa Ng’umbi, Issa Maige, aliiomba mahakama hiyo impunguzie kulipa jumla ya shilingi milioni 15 ambapo kwa upande wake wakili wa wadaiwa Mbogoro na wakili wa serikali Sehel, waliomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa sababu mlalamikaji anajiweza kiuchumi, hivyo ana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kama sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002 inavyomtaka.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.