Header Ads

MABADILIKO YA KATIBA YASIVURUGE AMANI YETU


Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema: “Uhuru bila nidhamu ni sawa uendawazimu na nidhamu bila uhuru ni sawa na utumwa.”


Nimelazimika kuyatumia matamshi hayo kwasababu kwa wale ambao ni wafuatiliaji wa masuala yahusiyo mustakabali wa taifa hususan hili la taifa liandike Katiba, mtakubaliana nami kwamba baadhi ya wananchi wanatumia uhuru bila nidhamu.

Matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Aprili 7, mwaka huu yalitokea katika Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam wakati wa mjadala wa mabadiliko ya Katiba na kusababisha mjadala huo kuvunjika.

Tukio jingine lilitokea siku hiyo hiyo katika viwanja vya Bunge Dodoma na kusababisha wanausalama kutumia mabomu ya machozi, risasi, virungu na mabango ya kuikebehi serikali baada ya wananchuo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kudaiwa kutishia hali ya usalama katika eneo hilo.

Pia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika Ukumbi wa Shule ya Haile Selassie mjini Zanzibar.

Inaelezwa kuwa polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) na wanausalama walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wanachuo hao waliotaka kutumia nguvu kuingia katika Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa kushiriki mjadala huo.

Amri ya kupiga mabomu ilitolewa na Mkuu wa Mkoa, Dk. James Msekela baada ya wanachuo hao kuanza kurusha mawe na kumjeruhi mpiga picha wa gazeti la Mwananchi, Edwin Mjwahuzi na askari mmoja.

Wanachuo hao waliokuwa wakiimba nyimbo na mabango ya kuikebehi serikali kwa zaidi ya saa tatu, waliamua kuvurumisha mvua ya mawe ndani ya eneo la Bunge, wakipinga wadau wengine kuendelea na mjadala wakati wao wako nje.

Kwa upande wake Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, alilaani vurugu hizo na kusema wanachuo hao walikuja kwa shari maana hata kukaguliwa walikataa.

Kama maelezo ya viongozi hao ni sahihi basi yale matamshi ya Mwalimu Nyerere kwamba: “Uhuru bila nidhamu ni sawa na wendawazimu,” ni sahihi kabisa.

Nchi yetu imeridhia taifa linaloongozwa na Katiba, kanuni mbalimbali za serikali, taratibu na mazoea ya serikali; hivyo kila mwananchi anatakiwa kufuata sheria hizo anapodai dai lake.

Aidha kitendo cha mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM-Tambwe Hizza na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba wakati wakitoa maoni yao kuzomewa na kupigiwa makelele wasiendelee kutoa maoni yao, ni wazi miongoni mwetu tunaohitaji hitaji hilo la katiba, tuna ajenda zetu za siri ambazo tumezivika kilemba cha dai la Katiba mpya.

Aiingii akilini kwa mtu mwenye akili timamu anayeelewa nini maana ya demokrasia na Ibara ya 18(a) ya Katiba ya mwaka 1977 inayosema: “Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake,” kufanya uhuni kama uliofanywa na baadhi ya wanachuo hao na wale washiriki wa mdahalo wa Karimjee uliosababisha uhairishwe kwa ajili ya wananchi kumkatiza kwa makusudi Hizza asiendelee kutoa maoni aliyotumwa na chama chake.

Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake bila kuvunja sheria na ana haki ya kusikilizwa hata kama maoni yake yanatofautiana na mawazo ya watu wengine na hiyo ndiyo demokrasia.

Kitendo cha baadhi ya washiriki kushindwa kumvumilia Hizza amalize kutoa mawazo yake, wamekosa nidhamu, hawajakomaa kidemokrasia na wana ajenda yao binafsi.

Katika mdahalo wa Karimjee imeelezwa kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wastaafu wa serikali na waliopo serikalini kwa sasa na wasomi walikuwepo na kudiriki kuleta fujo za kutupiana maneno ndani ya ukumbi huo.

Siku nyingine wanaoandaa mdahalo huo, kama hawatawaita vyombo vya usalama, ipo siku washiriki wataingia na silaha za jadi kama fimbo, wembe na nyinginezo.

Suala la mjadala wa mabadiliko ya Katiba ni suala nyeti sana kwani ni la ustawi wa taifa letu sasa kama serikali na vyombo vyetu vya dola kama havitakaa imara katika mijadalo hiyo ni wazi kabisa uvunjifu wa amani utakuwa ukitokea mara kwa mara.

Katiba haijaundwa mmeishaanza kuleta vurugu je, huko mbele ya safari ikaundwa halafu hao washiriki wakorofi wakabaini maoni yao hayakuingizwa kwenye Katiba hiyo, si watatuletea vurugu hapa nchini?

Ieleweke kwamba kila sehemu kuna viongozi na sheria na taratibu zake. Sasa kitendo kilichofanywa na wanachuo wa UDOM eti kwa sababu wamezuiliwa kuingia ndani ya ukumbi huo, kimeshusha heshima ya wasomi hao na kimetushangaza na kuona huenda wasomi hao walikuwa na ajenda nyingine zaidi ya kuruhusiwa kuingia kwenye mdahalo huo.

Siku zote jamii inaamini wasomi ni watu waliostaarabika na wawe mfano kwa jamii.
Haiingii akilini kabisa wanafunzi hao kuelezwa kwamba ukumbi huo ni mdogo hauwezi kubeba tena idadi hiyo ya wanafunzi ambao wanakisiwa kuwa ni zaidi ya 9,000 na badala yake wakaruhusu wanafunzi wachache waingie lakini wanafunzi hao wakaamua kuzua tafrani hilo eti kwa kigezo cha kuzuiiliwa kuingia ukumbini.

Watanzania tukumbuke ni hawa hawa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wamekuwa wakilalamika kuwa madarasa na mabweni wanayosemea na kulala yameelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi na kuishinikiza serikali itanue vyuo hivyo kwa kujenga majengo zaidi, lakini ghafla wiki iliyopita wanafunzi hao wakakengeuka na kutaka waruhusiwe kujazana kwenye ukumbi huo licha ya kuambiwa umejaa.

Tuwahoji wanafunzi hawa endapo Dk. Msekela na uongozi wa ukumbi wa Msekwa wangekuwa legelege na wangewaruhusu wanachuo hao wote wakajazane kwenye ukumbi huo na kwa bahati mbaya hewa ingekosekana na watu kupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa hewa, wangemlaumu nani?

Na ambao wangenusurika kifo hicho ndiyo wangekuwa wa kwanza kuishutumu serikali kuwa ilishindwa kudhibiti mapema idadi ya watu kuingia ukumbini humo?

Tuwaulize wasomi hawa hadi walifikia hatua ya kushupalia kuingia kwa nguvu kwenye ukumbi huo, hivi wanafikiri huyo aliyekuwa anaendesha mdahalo huo angeweza kutoa nafasi kwa kila mwanachuo wa UDOM kutoa maoni yake?

Sasa swali ni je hivi kama wanafunzi hao walikuwa na lengo moja la kushiriki mdahalo huo, yale mabango waliyobeba waliyapata wapi katika kipindi kifupi namna ile?
Huko ni kukosa ni dhamu mbele ya viongozi waliowazidi umri waliokuwa ndani ya ukumbi na jamii kwa ujumla.

Ni kweli wanafunzi hao walikuwa na haki ya kushiriki na kutoa maoni yao kwenye mdahalo huo na midahalo mingine itakayokuja, lakini haki hiyo iligeuka kuwa ghasia kwa wapita njia na wakazi wa maeneo hayo kutokana na vurugu walizozifanya.

Tunaamini wao ni wasomi na wengine wanasomeshwa na kodi za wananchi kama waliona haki yao imeporwa si vyombo vya dola vipo wangeenda kulalamika.

Mkae mkijua mlichokifanya kimeishajengeka vichwani mwa watu kwamba wanafunzi wa UDOM ni wakorofi wanatumiwa na wanasiasa kirahisi na mwisho wa siku sifa hiyo mbaya hata kama mtakuwa mmefaulu vizuri itawawia vigumu kupata ajira kwenye soko la ajira.

Tunafahamu si wanafunzi wote ni wakorofi ila kuna baadhi yao wamesahau dhiki za majumbani kwao na matokeo yao wamejisahau kilichowapelekea chuoni hapo ni kupata elimu na si huo mdahalo wa mabadiliko ya Katiba ambao haupo hata katika mtahala wa masomo yanayotolewa na Chuo hicho.

Lakini wasomi hao busara hiyo hawakuichukua wakaamua kutumia njia ovu ya kurusha mawe na kutoa maneno ya kashfa dhidi ya serikali na CCM.

Tuwaulize wanafunzi hao hivi ndani ya ukumbi ule ulihudhuriwa na wana CCM peke yao?
Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema, alisema yeye ndiye aliyekwenda katika Chuo Kikuu cha Dodoma kuwahamasisha wanafunzi hao waje kwa wingi katika mdahalo huo.

Kwanza kabisa wanafunzi hao kabla ya kufika katika viwanja hivyo walipaswa kumuuliza Lema kwamba yeye ndiye mratibu wa mdahalo huo?

Na je, ameweka utaratibu upi ambao ungewawezesha mamia ya wanafunzi hao kuweza kushiriki katika mdahalo huo?

Kama maswali hayo yote wangemuuliza mapema mbunge huyo ni wazi wasingekubali kuswagwa namna ile ambapo mwisho wa siku wakajikuta yule aliyewaalika (Lema) amepata nafasi ya kuingia ukumbini na wao kuishia nje na kupata mkong’oto toka kwa Jeshi la Polisi.

Kama wangeondokana na mawazo mgando baada ya kupata mwaliko wa mdomo toka kwa mbunge huyo ambaye naye alikuwa ni mwaliko kama walivyokuwa waalikwa wengine, serikali ya wanafunzi wa chuo hicho ingeteua wawakilishi wachache waende kushiriki kwa niaba ya wanafunzi wote.
Mwanachuo yoyote aliyekuwa ana mawazo yake angeandika wazo lake na kuwapatia wawakilishi hao ambao wangelifikisha kwenye mdahalo huo ama kwa mdomo au kwa maandishi.
Hivyo idadi kubwa ya wanafunzi wangebaki chuoni na kuendelea kujisomea kwani sisi tunachojua kilichowapeleka wanafunzi hao pale UDOM ni masomo na si ujuha kama ule.
Wanafunzi na wananchi wengine wanaoleta vurugu kwenye midahalo hiyo wajue kwamba wao si waamuzi wa kuruhusu muswada wa mabadiliko ya Katiba upite au usipite.
Waamuzi ni wabunge wetu wanaotuwakilisha bungeni ambapo Alhamisi na Ijumaa wiki hii wataujadili muswaada huo na kuupigia kura za muswada huo upite au usipite.
Hivyo kazi yetu sisi ni kutoa maoni kwa njia ya amani na kazi ya kuamua kuamua mswaada huo upite au usipite ni ya Bunge.
Hivyo msituvurugie amani kwaajili ya ajenda zenu za siri.
Fukuto la Jamii linawaasa wafuasi wa vyama vya siasa hapa nchini vinavyodaiwa vimekuwa vikiwatumia wanachama wao kuleta vurugu kwenye midahalo hiyo, viache tabia hiyo, kwani muswada huo hauna vyama bali unawahusu Watanzania.
Desemba 31 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete wakati akizungumza na wananchi kupitia hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, alisema anakubali hoja ya kuundwa kwa Katiba mpya.
Kila mmoja wetu amelichukulia hilo kivyake, na hii ndiyo tabia ya Watanzania ambo hawajajenga mila, desturi na utamaduni wa kushiriki katika mjadala wa kitaifa.
Mjadala wa kitaifa ni mchakato wa kujenga hoja kwa masilahi ya taifa. Kamwe hauendeshwi kwa kila mtu kujenga hoja kutetea tumbo lake.
Kwa hiyo wengi wanaojenga hoja ya kutaka kuundwa kwa Katiba mpya, wanafikiri matumbo yao, masilahi binafsi na umaarufu binafsi.
Vipo vyama na wapo watu na vikundi ambavyo bila kujali umaarufu binafsi wameendeleza hoja hii hadi leo.
Wapo baadhi ya wanasiasa watakaojaribu kuibinafsisha hoja hiyo ili waonekane ni waasisi wa hiyo hoja.
Wanaamini kwamba kumbukumbu za Watanzania ni duni hawawezie kukumbuka hoja hii ilianza lini na waasisi ni kina nani.
Tena katika hali ya kushangaza kama sio kustaajabisha wanachama wa vyama vya siasa na baadhi ya viongozi wao hawajui katiba za vyama vyao ambazo zimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na wala hawafahamu zimeandikwa nini ndani yake.
Sasa iweje leo hii wawe na ukereketwa wa kudai Katiba mpya ikiwa tu ibara za katiba ya vyama vyao hawazijui zinasema nini?
Wengine hata gamba la Katiba ya Jamhuri hawajawahi kuliona na duka la vitabu vya serikali ambapo ndipo sheria zote za Katiba ya nchi zipo yapo wapi?
Rais Kikwete katika hotuba yake ile pia alitamka kwamba mwaka huu ni wa Watanzania kujadili hoja ya Katiba mpya na yeye ataunda tume ya kuongoza mchakato wa kupata Katiba mpya.
Na kweli ahadi hiyo ya rais imetimia katika kipindi kifupi, kwani tayari muswada umeshaandaliwa na kupelekwa bungeni tayari kwa kuanza kujadiliwa.
Ni vema tukampongeza Rais Kikwete kwa kutekeleza ahadi hiyo katika hatua hii ya awali kwa kuzingatia kwamba hatua hiyo ni ya kijasiri sana kwani ukweli ni kwamba kundi kubwa la wanaopinga hoja hiyo wapo katika chama anachokiongoza cha CCM na serikali anayoingoza.
Sasa Watanzania tuko wapi? Je, tunaelewa kilichomsibu rais hadi akubali hoja ya Katiba mpya?
Kabla ya kupinga na kuona nia ya rais wetu ni mbaya eti kama ana jaribu kuteka hoja au kupora hoja ya wapinzani, tujiulize ni wangapi wanaelewa maana kamili ya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2010?
Ni wangapi miongoni mwetu wameishaisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977?
Nimalizie kwa kuwakumbusha wale wote wanaoleta vurugu kwenye mijadala hiyo kwamba utawala wa serikali yetu ni utawala unaoongozwa na sheria na Katiba na kamwe utawala huo haufanani na ule utawala wa samaki aina ya kambale ambao baba, mama na mtoto wote wana ndevu.
Hivyo sote tunapaswa tufuate sauti moja ya misingi tuliyojiwekea.
Hakuna ubishi, yale matamshi ya Mwalimu Nyerere kuwa “Uhuru bila nidhamu ni sawa uendawazimu,” yametimia kutokana na matukio hayo niliyoyataja na mengine sijayataja ambayo yametokea na yanaoendelea kutokea chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne.
Sasa unapokuwa na taifa lenye wananchi wanaotumia vibaya uhuru wa kutoa maoni ni wazi kabisa muda si mrefu taifa hilo litajikuta linafuga na kuwalinda wananchi wengi ambao ni wendawazimu.
Navyo vyombo vya habari visifanye ushabiki katika suala hili la mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Kwa sababu hoja hiyo si mali binafsi ya Rais Kikwete, CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi wala vyama vingine vya upinzani bali ni hoja ya Watanzania wote kwa masilahi yao.

Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 12 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.