Header Ads

DOWANS YAWAJIBU LHRC

Na Happiness Katabazi

KAMPUNI ya Dowans Holding SA na Dowans Tanzania Ltd, zimeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itupilie mbali mapingamizi waliyowekewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wengine, kwa madai kuwa hawana haki ya kisheria kupinga tuzo waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) isajiliwe na mahakama hiyo.


Mbali na LHRC, wengine walioweka mapingamizi ya kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania isisajili tuzo hiyo ni mwandishi wa habari mwandamizi, Timothy Kahoho, Lawyers Environment Action Team na Sikika Company.

Ombi hilo la kutaka mapingamizi hayo yatupiliwe mbali liliwasilishwa hivi karibuni mahakamani hapo na wakili wa Kampuni ya Dowans, Kennedy Fungamtama, kwa madai kuwa LHRC na wengine wanaopinga tuzo hiyo hawana haki kwa sababu hawakuingia nao mkataba wa kufua na kuzalisha umeme.

Nakala ya mapingamizi hayo ya Dowans ambayo Tanzania Daima inayo, inaeleza kuwa wenye haki ya kupinga tuzo hiyo ni TANESCO ambao waliingia nao mkataba na si watu, ama taasisi nyingine.

Nakala hiyo ya Dowans imechambua kuwa; Kahoho hana haki wala masilahi yoyote ya kisheria yanayompa nguvu ya kisheria ya kupinga tuzo, kwa sababu mkataba uliingiwa na pande mbili ambazo ni Dowans na TANESCO na kuongeza kuwa hata TANESCO ilipovunja mkataba huo ni Dowans ndiyo ilikwenda ICC kuifungulia kesi TANESCO na hatimaye Oktoba 15 mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa hukumu ambapo Dowans ndiyo ilishinda kesi hiyo.

Wakili huyo wa Dowans, Fungamtama anadai kuwa hata katika mkataba walioingia Dowans na TANESCO , Kahoho hawakuwa sehemu ya mkataba huo (Power Off –Take Agreement (POA) ambapo kwa mujibu wa mkataba huo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa endapo itatokea tofauti miongoni mwao, mgogoro wao utatatuliwa na Mahakama ya ICC.

Alisema pande zote zilikubaliana kwamba mkataba huo ni mzuri na kwa mazingira hayo, Mahakama ya Tanzania haitakuwa na mamlaka ya kuona mkataba huo ni batili, hivyo wapingaji hao hawana mamlaka ya kuupinga.

Kuhusu hoja ya Kahoho kwamba Dowans isilipwe, Fungamtama alidai kuwa si ya msingi na haina mantiki kisheria, kwani tayari Mahakama ya ICC ilishatoa hukumu yake na ikaiamuru TANESCO kuilipa fidia Dowans, ikiwa ni hasara waliyoipata baada ya TANESCO kuvunja mkataba kinyume cha makubaliano.

Aidha, kuhusu mapingamizi ya LHRC, Lawyers Environment Team na Sikika Company Ltd, dhidi ya Dowans, kwanza Fungamtama alihoji uwezo wao kisheria, uwakilishi wao kwa watu wasiofahamika kama walivyodai kuwa wanawawakilisha wananchi na kuongeza kuwa hawana sababu ya kisheria ya kusema kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi wanaopinga tuzo hiyo isisajiliwe na kulipwa.

Wakili Fungamtama alidai kuwa walalamikaji hao walikosea kutaja kiwango cha tuzo aliyoshinda mteja wake. Tuzo aliyoshinda mteja wake ni dola za Marekani 65,812,630.33 na si dola 123,223,270.98 kama walivyoainisha kwenye hati yao ya madai na kuongeza kuwa si kwamba mkataba ulioingiwa na TANESCO na Dowans hauwabani .

Baada ya mahakama kupokea mapingamizi hayo ya Dowans, iliitaka TANESCO ijibu pingamizi lililowekwa dhidi yake na Dowans Mei 27, mwaka huu.

Kadhalika LHRC na Kahoho nao wajibu mapingamizi waliyowekewa na Dowans Mei 20 mwaka huu, na kwamba majibu yote hayo yajibiwe kwa njia ya maandishi na akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 28 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye TANESCO, LHRC na Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.

Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO, Novemba 15 mwaka jana, ambapo mahakama iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaiamuru iilipe fidia ya shilingi bilioni 94, hukumu ambayo imezua mjadala mkali hapa nchini kuanzia kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa na makundi mengine, ambapo wengine wanataka Dowans ilipwe huku wengine wakitaka kampuni hiyo isilipwe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 7 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.