Header Ads

KESI YA MPENDAZOE YAFIKA PATAMU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mei 25,26 na 27 mwaka huu, itaanza rasmi kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya Jimbo la Segerea uliofanyika mwaka jana yaliyomtangaza Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk.Makongoro Mahanga kuwa ndiye mbunge iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya (Chadema), Fred Mpendazoe.


Mbali na Dk.Mahanga wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo na katika madai yake mlalamikaji ambaye ni Mpendazoe anataka mahakama kuu itengue ushindi wa Dk.Mahanga kwakuwa taratibu za sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010 hazikufuatwa

Kwa mujibu wa hati wito wa kuitwa mahakamani iliyotolewa na mahakama ambayo Gazeti hili limefanikiwa kuona nakala yake, wahusika wa pande zote katika kesi hiyo wameishapewa nakala hiyo ya wito wa kufika mahakamani siku hiyo mbele ya Jaji Profesa Ibrahim Juma.

Kwa upande wake wakili Mpendazoe, Peter Kibatala alilithibitishia gazeti hili jana kwamba tayari ameishapokea kwaniaba yake nakala hiyo ya wito na kwamba watafika bila kukosa siku hiyo ambapo kesi yao itaanza kuunguruma rasmi.

Kesi hiyo ya Mpendazoe ni kesi ya kwanza kati ya kesi tisa za kupinga matokeo ya Uchaguzi wa ubunge wa mwaka 2010 kufikia hatua hiyo ya juu ya kuanza kusikilizwa.Kwani kesi nyingine za aina hiyo bado zipo katika hatua za awali mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 15 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.