Header Ads

HAKIMU AKATALIWA

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa Serikali katika kesi ya jinai Na.149/2010 ya utakatishaji fedha haramu ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.8 inayomkabili Afisa wa Mamlaka ya Mapato(TRA), Justice Katiti na wenzake,katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana waliwasilisha ombi la kumuomba Hakimu Mkazi anayesikiliza kesi hiyo Waliarwande Lema ajitoe kwenye kesi hiyo kwasababu hawana imani naye.


Mbali na Katiti, washtakiwa wengine ni Samweli Renju , Haggay Mwatonoka na Hope Lulandala afisa wa Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) na mfanyabiashara Erick Lugereka ambao wanaendelea kusota rumande tangu mwaka 2010 walipofikishwa mahakamani hapo kwa kosa hilo la utakatishaji fedha haramu ambalo kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kosa hilo halina dhamana.

Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Oswald Tibabyekomya kwaniaba ya mawakili wenzake Wakili Kiongozi wa Serikali Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro mbele ya hakimu Lema wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Akiwasilisha ombi hilo huku akionekana kujiamini, Wakili Tibabyekomya aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa lakini upande wa jamhuri haupo tayari kwaajili kuanza kusikilizwa kwasababu wamekuja na ombi la kuomba hakimu Lema ajitoe na asiendelee kusikiliza kesi hiyo kwasababu hawana imani nae kwani tangu waanze kuindesha kesi hiyo wakili Manyanda na Kimaro wamekuwa wakipokea vitisho vinavyohatarisha usalama wao kwa njia ya ujumbe mfupi kutoka kwa namba moja ya simu ya kiganjani.

Wakili Tibabyekomya aliendelea kueleza kuwa kufuatia mawakili wenzake anaoendasha nao kesi hiyo kupokea vitisho mara kwa mara walifikia uamuzi wa kwenda kutoa taarifa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, na ile namba iliyokuwa ikitumika kuwatumia vitisho waliwapatia makachero wa jeshi la polisi ambapo makachero hao walianza kuchunguza namba hiyo na bado wanaendelea na upelelezi wao na kwamba katika upelelezi wao wa awali ukabaini ujumbe huo mfupi wa vitisho ulikuwa ukitumwa kwao na mtu asiyefahamikwa na alikuwa akitumia simu ya mkononi inayosadikiwa kuwa ni Hakimu Lema.

“Na kwamba Machi 13 mwaka huu, Hakimu Lema jeshi la Polisi lilimtaka afike katika makao makuu ya Jeshi hilo, na hakimu Lema aliitii amri hiyo na alipofika na kuhojiwa na makachero hao kuhusu hilo hakimu huyo alikanusha tuhuma hizo…na kwa kuwa hali ni hiyo sisi mawakili wa serikali ili tuone haki inatendeka katika kesi hii tunakuomba wewe hakimu Lema ujitoe kwenye kesi hii ili apangwe hakimu mwingine ambaye hatutakuwa na mashaka naye ili aweze kuendelea kusikiliza kesi hii”alidai wakili Tibabyekomya.

Kwa upande wake Hakimu Lema alisema amelisikia ombi hilo na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 12 mwaka huu, ambapo siku hiyo atatoa uamuzi wake kuhusu ombi hilo la mawakili wa serikali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Machi 28 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.