Header Ads

MTIKILA ANASWA KESI YA KUMWITA JK GAIDI


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Part(DP), Mchungaji Christopher Mtikila ana kesi ya kujibu katika kesi ya kuchapisha na kuusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.


Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake baada ya kuwaleta mashahidi watano kutoa ushahidi wao.

Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri,amefikia uamuzi wa kumuona Mtikila ana kesi ya kujibu na kwamba maana hiyo Mtikila atatakiwa na mahakaa hiyo kupanda kizimbani Aprili 11 mwaka huu kwaajili ya kuanza kujitetea.


Baada ya Hakimu Fimbo kutoa uamuzi huo, Mtikila alidai kuwa anatarajia kuleta mashahidi 10.

Februali mwaka huu, Mtikila alikiri maelezo aliyochukuliwa na afisa wa polisi ni yake na kwamba hana pingamizi nayo na hivyo mahakama iliyapokea kama kielezo cha upande wa jamhuri.Mtikila katika maelezo hayo ya onyo alikiri kuwa ni kweli aliuandaa waraka huo na kuusambaza ila akakanusha waraka huo si wa uchochezi ila unahusu maneno ya mungu.

Mtikila alikiri maelezo hayo yaliyosomwa na kutolewa mahakamani kama kielelezo baada ya shahidi wa Jamhuri, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ibeleze Mrema (54) kudai kwamba Aprili 15, mwaka 2010 akiwa kituo cha polisi kikuu jijini Dar es Salaam, aliitwa na mkuu wake wa kazi na kumpa kazi ya kumhoji Mtikila kuhusu tuhuma za kukutwa na waraka wa uchochezi.

Alidai kuwa wakati akimhoji mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na nyaraka hizo na kwamba alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuokoa wakristo na alisaini yeye waraka huo.

“Mtikila alikiri kuhusika kuandaa waraka huo kama mwenyekiti alisaini kwa niaba ya wengine … nilipomhji walichapisha wapi mtikila hakupenda kusema bali alidai kuwa zilikuwa nyaraka 100,000 ambazo zilisema kwamba Rais Kikwete anaangamiza ukristo na amekuwa jasiri kuingiza uislamu katika katiba ya Jamhuri” alidai Mrema kupitia maelezo hayo yaliyotolewa na Mtikila.


Mrema aliendelea kudai kupitia maelezo hayo kwamba, Mtikila alikuwa anahamasisha wakristo wajitoe mhanga kukomesha ugaidi na wamuweke rais mkristo Ikulu.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshitakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu' alinukuliwa Mtikila.

Katika shitaka la pili, Aprili 16, mwaka 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii.Na katika kesi hii Mtikila hana wakili wa kumtetea na anajitetea mwenyewe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Machi 14 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.