Header Ads

UGONJWA WA DK.MWAKYEMBE USITUGAWE



Na Happiness Katabazi

ITAKUMBUKWA kuwa tangu Oktoba 2 mwaka jana, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Dk.Harrison Mwakyembe aliondoka hapa nchini na kupelekwa India kwaajili ya matibu, maneno maneno na hisia mbalimbali zimekuwa zikibuliwa kupitia vyombo vya habari na huko mitaani.


Kuna watu wamediriki kujitokeza adharani na kwanjia ya mitandao ya kijamii akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Samwel Sitta zaidi ya mara moja amenukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza Dk.Mwakyembe amelishwa sumu na mafisadi bila kuyataja majina hayo ya mafisadi.

Na wengine wamekuwa wakienda mbali zaidi kupitia hiyo mitandao ya kijaami wakijinasibu kuwa wamefanya uchunguzi wao binafsi kuhusu chanzo cha ugonjwa anaosumbuliwa nao naibu waziri huyo na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya na wakaitimisha kwa kusema serikali kupitia Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ambayo kwasasa inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu Rashid Othman.

Kwa wale wanaotembelea mitandao hiyo ya kijaami karibu kila siku watakubaliana na mimi kuna taarifa moja zinawekwa humo ambazo waandishi walioandika taarifa hizo wanadai kuwa wamefanya utafiti na kubaini kuwa ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo wameshiriki kikamilifu kumdhuru Dk.Mwakyembe na Profesa Mwandosya.

Na siyo waraka huo tu pia kuna waraka mwingine ambao unadaiwa kuandikwa na Mwakyembe mwenyewe ambapo gazeti hili iliandika habari hiyo na kudai kuwa inayo nakala yake ambayo ndani ya wakala huo eti Dk.Mwakyembe amewataja kwa majina wabaya wake waliomtenda.

Na waraka huo ambao unadaiwa kuwa umeandikwa na Dk.Mwakyembe mwenyewe kwa ndugu na jamaa zake ambao hadi sasa hatujamsikia Dk.Mwakyembe akiukanusha, unaeleza kuwa kuna sabuni na kitaulo ambacho aliwekewa ofisini kwake na mhudumu na alipotumia ndiyo alianza kuwashwa na baada ya muda mfupi akasikia mhudumu alifariki na akaenda kuzikwa kijijini kwao Ipinda –Kyela mkoani Mbeya hali ambayo naibu waziri huyo anasema katika waraka huo kuwa kifo hicho cha ghafla cha mhudumu huyo kilimshtua.

Awali ya yote naomba nieleweke kuwa mtazamo huu hauna lengo la kupora matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi ambayo yanampa haki mwanachi kueleza fikra zake kuhusu afya kiongozi huyo la hasha mtazamo huu una lengo la kuvitaka vyombo vya dora hususani kuamka usingizini na kuanza kuwashughulikia wale wote ambao wanaojitokeza adharani kwa majina yao halisi au bandia kueneza taarifa dhidi ya mgonjwa huyo kuwa amelishwa sumu bila kuambia ni watu gani wamemlisha sumu, na ni kwanini Dk.Mwakyembe alishwe sumu?Na alilishiwa wapi na lini?

Inawezekana madai hayo yana ukweli ndani yake kuwa lakini ikumbukwe kuwa kifungu cha 7(1) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinasema mtu yoyote ambaye anafahamu kutendeka kwa kosa, mtu huyo ana wajibu wa kupeleka taarifa hizo katika vyombo husika ana akishindwa kufanya hivyo atashtakiwa kwa kosa la kusaidia kutenda kosa kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Sasa hawa wanasambamba za taarifa kuwa Mwakyembe kapewa sumu kwenye mitandao na kwenye vyombo vya habari wanapaswa wapeleke taarifa hizo kwenye mamlaka husika na wakishindwa kufanya hivyo wanatakiwa waadhibiwe.

Ikumbukwe kuwa minong’ono na hisia kama hizo uliwahi kuibuka pia katika kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Horace Kolimba alizidiwa ghafla wakati yupo kwenye kikako cha Kamati Kuu kilichokuwa kikifanyika mjini Dodoma.

Baada ya kifo hicho kutokea Mwenyekiti wa Chama cha Democraty(DP), Mchungaji Chsristopher Mtikila alijitokeza adharani na kusema kuwa Kamati Kuu ya CCM, ndiyo iliyomua Kolimba kwani masaa manne kabla ya Kolimba kuingia kwenye mkutano ule alikuwa ni mzima wa afya.

Kufuatia matamshi hayo ambayo yalianza kujenga hisia mbaya kwa wana jamii, Jeshi la Polisi lilimkamata Mtikila na kumfungulia kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kisha Hakimu Gabriel Mirumbe ambaye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na mwaka 1999 alimhukumu Mtikila kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo ambalo Mtikila alishindwa kuleta ushahidi ambao ungethibitisha maelezo yake kuwa ni kweli Kamati Kuu CCm ndiyo iliyomuua Kolimba.

Na Mtikila alitumikia adhabu hiyo katika gereza la Keko na alikata rufaa katika Mahakama ya Kuu na Mahakama ya Rufaa lakini rufaa zake zote mbili zilitupwa na mahakama hizo za juu nchini kwasababu waliona rufaa ya mwanasiasa huyo haina msingi wowote.

Kwa hiyo basi tunaweza kuona vyombo vyetu vya dola vikiamka usingizini na kuona hayo maneno na waraka mbalimbali unaondelea kusambazwa kupitia mitandao, vinaweza kuwachukulia hatua wale wote wanaosema Mwakyembe kalishwa sumu na serikali ,mafisadi kama alivyochukuliwa hatua Mtikila.Nimejiuliza hivi huyu Sitta na Mwakyembe wote si ni viongozi na hivyo ni sehemu ya serikali? Kwa hiyo nao basi wanawafahamu hao watu waliomtenda hivyo sasa kama wanawafahamu kwanini wasiwaje kwa majina kuliko kuishia kusema amelishwa sumu na mafisadi hivi hao mafisadi hawana majina mbona majina hamyataji?

Waraka mwingine unaodaiwa kuandikwa na Mwakyembe ambao eti amewaandikia ndugu na jamaa zake unasema anahisi matatizo yaliyompata uenda chanzo chake kinatokana na sabuni na taulo aliyokuwa amewekea ofisini kwake na mhudumu kwani baada ya kutumia vitu hivyo alianza kuwashwa.

Na kauli hizo za Sitta na Mwakyembe zimeanza kutufanya tuamini kuwa uwenda hawa wamejitenga na serikali yao na walichoamua sasa nikuanza kuipaka matope serikali yao kuwa inawakumbatia wauaji kwamba serikali tena haiwalindi viongozi wake.

Na kushindwa kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu wa aina hiyo ni wazi kabisa vyombo hivyo hivyo vya dola vitakuwa vimeshiriki kikamilifu kujenga taifa la baadhi ya wananchi waropokaji, wenye chuki na hasira dhidi ya serikali yao kupitia TISS kuwa idara hiyo ndiyo ilimsababishia maradhi hayo Mwakyembe wakati idara hiyo ilikuwa na jukumu la kumlinda kiongozi na viongozi wengine.

Na tukiruhusu tufike huko ipo siku nchi hii itajikuta inaingia kwenye vita ya makabila au wenyewe kwa wenyewe .

Kila mmoja kwa nafasi yake alijuilize mfano ndiyo unamuuguza mzazi wako au ndugu yako halafu wanajitokeza watu kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii wanasema wazi kuwa maradhi yanayomsumbua mzazi wako au ndugu yako yamesababishwa na kikundi cha watu fulani au serikali kumlisha sumu?.

Ni wazi kabisa utaanza kujenga chuki na serikali na kikundi hicho na mwisho wa siku mtu yoyote ambaye alishapandikizwa chuki moyoni na akilini anaweza kulipiza kisasi kwa njia yoyote dhidi ya watu alielezwa kuwa ndiyo waliomdhuru mzazi wake hata kama hana ushahidi.

Ieleweke wazi Mwakyembe ni mtu aliwahi kuwa mwalimu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,mbunge, pia ana watu wengi ambao anafahamiana nao nawao anawafahamu na aliowasaidia na waliomsaidia katika maisha.

Sasa inapotokea taarifa za yeye kulishwa sumu bila ya hao wanaozisambaza kutoa ushahidi kukutolea ushahidi amelishwa sumu na nani,lini na ni kwasababu gani hao watu wamlishe yeye ?

Ni wazi watu hao wanaofahamiana na Mwakyembe kama hawana roho nguvu na siyo waelewa wa mambo ni wazi kabisa wataanza kujenga hisia mbaya na chuki dhidi ya wale wanaodaiwa ni maadui wa naibu waziri huyo na serikali.

Nampa pole Mwakyembe kwa maradhi yanayomsumbua ila msimamo wangu ni kwamba siwezi kukubaliana moja kwa moja na wale wote wanaosema kiongozi huyo kalishwa sumu au kugusishwa kwani wameshindwa kuanika ushahidi ni nani aliyemlisha sumu, kwanini yeye alishwe sumu na alilishiwa wapi na hata yeye Mwakyembe hakuna sehemu yoyote ambayo ametamka amelishwa sumu?

Kwani hadi sasa ripoti ya madaktari waliomtibia tumeelezwa kuwa wamebaini kuna kitu kipo kwenye Bon Marro ndiyo kinamsumbua na kwamba wanaendelea na uchunguzi zaidi ya kitabibu .Sasa huko kulishwa kunakodaiwa na baadhi ya watu kunatoka wapi?

Nimalizie kwa kumshauri Dk.Mwakyembe kuwa hivi sasa anatakiwa azingatie ushauri anaopewa na madakatri wake wanaomtibia,amrejee mungu wake ,atulize akili yake na awakataze hao baadhi ya ndugu zake na yeye kueneza taarifa za hisia hasi kuhusu maradhi yayomkabili kwani minaona akiruhusu jamii iendelee kujadili anachoumwa ni wazi hali hiyo pia itakuwa inamsumbua kisaikolojia ata yeye pia pamoja na familia yake na kumshushia hata yeye heshima hasa ukizingatia yeye ni msomi wa sheria kwani wanasheria wanamsemo usemo usemao hoja kwa vielelezo.

Hivyo ni rai yangu kwa watanzania wote kuwa maradhi yanayomkabili kiongozi wetu huyo yasiwe chanzo cha kuusambaratisha ummoja wetu,ugonjwa wa kiongozi huo usigeuzwe ajenda ya kuanza kuwapandikiza chuki wananchi dhidi ya wananchi wenzao na serikali yao kuwa ndiyo waliomlisha sumu wakati tumeishaelezwa kuwa madaktari bado wanatafuta chanzo cha maradhi hayo yanayomsumbua .

Kwa kuwa ni dhahiri baadhi ya wananchi huko mitaani wameishaanza kuamini taarifa hizo kuwa ni kweli kalishwa sumu wakati hiyo ripoti ya daktari haijasema hivyo.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Machi 4 mwaka 2012
www.katabazihappy.blogspot.com

No comments:

Powered by Blogger.