Header Ads

MASHAHIDI 10 KUMVAA LIYUMBA



Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa unatarajia kuleta jumla ya mashahidi 10 na vielelezo 10 katika kesi hiyo siku itakapoanza kusikilizwa.


Wakili wa Serikali Hamphrey Marick mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga alitoa maelezo hayo jana mahakamani hapo ambapo kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kumsomea maelezo ya awali ambapo alimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Wakili Marick akimsomea maelezo ya awali, alidai kuwa Julai 27 mwaka 2011 , Liyumba alikuwa ni mfungwa mwenye Namba 303/2010 ambaye alikuwa amefungwa katika gereza la Ukonga baada ya mahakama hiyo mwaka 2010 kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Wakili Marick alidai mshtakiwa huyo akiwa gerezani alikutwa na kifaa kilichozuiwa na Sheria ya Magereza ambacho ni simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 yenye rangi nyeusi ambayo ilikuwa na line yenye namba 0653 0004662 na IMEI namba 356273/04/276170/3.

Aliendelea kudai siku hiyo ya tukio mshtakiwa huyo alikuwa katika chumba binafsi namba tisa gerezani humo ambapo ndiyo alikuwa akiishi. Na kwamba mfungwa mwenye namba MF 891/169 Hamidu Henji “Tiba” ambaye ni Nyapara, alikuwa akitembea akitembea katika gereza hilo na alimuona Liyumba akiwa ameshika mfuko wa kuifadhia miwani akiwa ameugesha masikioni mwake.

“Mara baada ya Liyumba kumuona Nyapara huyo aliuweka chini ule mfuko wa miwani na kubakia akiongea na simu na hata hivyo Nyapara huyo tayari alikuwa ameishaiona ile simu na ule mfuko na haraka sana Nyapara huyo akaenda kutoa taarifa kwa maofisa wa Magereza waliokuwa kwenye doria siku hiyo gerezani humo”alidai wakili Marick.

Alidai kuwa maofisa hao waliopewa taarifa za tukio hilo na Nyapara huoni ni askari Magereza mwenye namba mwenye namba B 4948 WDR, Patrick na B 4885 WDR Iman Kyejo na askari hao walipokwenda kukagua chumba alichokuwa akiishi Liyumba,walifanikiwa kumkuta Liyumba akiitumia simu hiyo huku akiwa anatuma ujumbe mfupi(SMS) na kwamba kabla ya kutenda kosa hilo, hapo awali akiwa gerezani aliwahi kuonywa aache kutumia simu akiwa gerezani.

“Liyumba alipokutwa na maofisa hao akiitumia simu hiyo chumbani kwake aliamaki na akaomba kwanza wampatie dawa za ugonjwa shinikizo la Damu ili ameze na maji ya kunywa na maofisa hao walimpatia vitu hivyo alivyowaomba na baadaye wakampeleka Liyumba kwa Ofisa Msimamizi Mkuu wa Gereza:

“Akiwa katika ofisi ya Msimamizi Mkuu wa gereza hilo kwaajili ya kuanza kuchukuliwa maelezo,Liyumba akawaeleza maofisa hao kuwa hawezi kutoa maelezo yake kwanjia ya mdomo bali atatoa maelezo yake kwa njia ya maandishi na katika maelezo yake aliyoyatoa kwa njia ya maandishi ,mshtakiwa huyo alikiri kukutwa na simu gerezani’alidai wakili huyo wa serikali.

Wakili Marick alidai kuwa katika maelezo hayo Liyumba alieleza pia kuwa aliichukua simu hiyo kwenye Simintenki la kuifadhia maji ambalo lilikuwa karibu na Pampu ya maji ndani ya gereza hilo na kwamba hakuwai kukabidhi simu kwa hiyo kwa ofisa yoyote wa magereza kwasababu alikuwa anaiitaji kuitumia kwa kufuatilia hoja za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).

Hata hivyo Liyumba alikanusha maelezo hayo na Hakimu Sanga akaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 13 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 16 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.