Header Ads

MATTAKA AONGEZEWA MASHITAKA




Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara Kampuni ya serikali ya Air Tanzania Limited(ATCL) ya dola za Kimarekani 143,442.75 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo David Mattaka na wenzake umebadilisha mashtaka na kuwaongezea mashtaka washtakiwa hao.

Mbali na Mattaka anayetetewa na wakili Peter Swai,washtakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Mathew Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji anayetetewa na wakili Alex Mgongolwa.

Mbele ya Hakimu Ritta Tarimo wakili wa serikali Shadrack Kimaro, Oswald Tibabyekomya na wakili wa Mwandamizi toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Ben Lincoln waliikumbusha mahakama hiyo kuwa jana kesi hiyo ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ili hawataanza kuwasomea maelezo ya awali kwanza kwasababu wamebadilisha hati ya mashataka kwa mujibu wa kifungu cha 234 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, na hivyo wataanza kuisoma hati hiyo ya mpya ya mashtaka yenye jumla ya makosa sita ukilinganisha na hati ya awali iliyokuwa na jumla ya makosa matatu tu.

Wakili Kimaro alidai kuwa shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote watatu ni la kula njama kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007 ambapo Mattaka na wenzake katika tarehe tofauti Machi –Julai 2007 jijini Dar es Salaam, walikula njama na watu wengine wasiojulikana kutenda kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma .

Wakili Kimaro alidai shtaka la pili ambalo pia linawahusu washtakiwa wote ni la matumizi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu ch 31 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa hao wakiwa ni watumishi wa umma wa kampuni hiyo ya ATCL kwa nyadhifa zao wakati wakitekeleza majukumu yao kwania ovu walitumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha ununuzi magari yaliyokwishatumika 26 kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Na.21 ya mwaka 2008 pamoja na kanuni zake zilizotengenezwa na sheria hiyo.

Alidai shtaka la tatu pia ni kwa washtakiwa wote ambalo ni matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru ambapo mshtakiwa wa kwanza na wapili (Mattaka na Komba) wakiwa waajili wa ATCL wakati wakitekeleza majukumu yao na kwania ovu,walitumia madaraka yao vibaya na kisha waliagiza magari hayo ya mitumba bila kutangaza tenda ya ushindani na wakayanunua magari hayo kwa thamani ya dola za kimarekani 809,000 kutoka kampuni ya 3 IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai katika Jamhuri ya Emireti, kinyume na kifungu cha 59 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake.

Wakili Kimaro alidai shataka la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya Takukuru, na kwamba Agosti 2007 washtakiwa hao wakiwa ni waajiliwa wa Kampuni ya Ndege ya Taifa( ATCL) wakati wakitekeleza majukumu yao na kwania ovu walinunua magari hayo 26 ya mitumba kwaniaba ya ATCL inayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 58(3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008.

Wakili Kimaro alidai shtaka la tano ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru na kwamba kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 katika wilaya ya Ilala, washtakiwa wote kwa pamoja wakati wakitekeleza majukumu yao kwa nia ovu waliruhusu kununuliwa kwa magari hayo toka kwa kampuni ya 3 IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai bila kuwepo kwa mkataba baina ya kampuni hiyo na ATCL ambapo kwa upande wa ATCL Mkataba huo ulipaswa usainiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinyume na kifungu cha 55 Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni ya 15 ya sheria hiyo.

Katika shitaka la sita alidai ni la kusababisha hasara kampuni hiyo ya ndege ya taifa kinyume na kifungu cha 284(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 ,katika tofauti Julai 2007-Desemba 2001 jijini Dar es Salaam.Washtakiwa wote wakiwa waajiliwa wa ATCL ,walishindwa kuchukua taadhali na wakanunua magari hayo ya mitumba 26 toka kwa kampuni hiyo bila kuwepo kwa bajeti iliyotengwa na serikali kwaajili ya kununulia magari hayo.

Baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka hayo mapya ,wakili Kimaro akaiomba mahakama iwasomea maelezo ya awali washtakiwa, ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi Alex Mgongolwa na Peter Swai ambao waliomba maelezo hayo ya awali yasisomwe jana ili wapate waende wakayasome ili siku ya kuja kusomwa kwa maelezo hayo ya awali wawe wameelewa nini wanakikataa na nini wanakikubali hata hivyo wakili mwandamizi wa serikali Tibabyekomya alipinga hoja hiyo kwasabababu haina sababu za msingi na kuiomba mahakama ikubali wawasomee washtakiwa hao maelezo ya awali.

Malumbano hayo yalisababisha Hakimu Tarimo saa nne asubuhi aiarishe kesi hiyo hadi saa 6:40 ili aje kutolea uamuzi wa ama maelezo ya awali yasome au yasisomwe jana ambapo alilikataa ombi la upande wa Jamhuri lilotaka kuwasomea maelezo hayo ya awali washtakiwa jana kwamaelezo kuwa ili haki ionekane imetendeka ni lazima upande wa wadaiwa nao upewe nafasi ya kujiandaa kwaajili ya washtakiwa kusomea maelezo .

Akitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao, Hakimu Tarimo alisema ili mshtakiwa apate dhamana kwa mujibu wa hati hiyo mpya ya mashtaka ni lazima kila mshtakiwa atoe fedha taslimu au kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya Sh milioni 38 na washtakiwa hao walitimiza masharti hayo ya dhamana kwa kuwasilisha hati za mali isiyoamishika na kesi imearishwa hadi Machi 20 mwaka huu, ambapo kesi hiyo nitakuja kwaajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Novemba 22 mwaka 2011,washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa matatu,kosa la kwanza lilikuwa ni la kushindwa kutunza kumbukumbu za mawasiliano ya manununuzi ya magari hayo waliyokuwa wamefanya na kampuni hiyo na kosa la tatu ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambalo lilikuwa likimkabili Mattaka peke yake.

Itakumbukwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania Desemba 21 mwaka 2005 muda mchache baadaye alimteua Mattaka kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la ATCL na kisha baadaye kumteua Mattaka kuwa Mjumbe wa Tume ya Rais ya Kikosi Kazi cha Kurekebisha Shirika la Bima la Taifa.

Wakati Rais Kikwete akimteua Mattaka kushika nyadhifa hizo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, wananchi mbalimbali walilaani uteuzi huo bila mafanikio.

Na kabla ya Rais Kikwete kumteua Mattaka kushika nyadhifa hizo,Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikuwa amemstaafisha Mattaka kwa manufaa ya umma.Na wakati Mkapa anamstaafisha mshtakiwa huyo kwa manufa ya umma alikuwa akishikilia cheo cha Ukurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pesheni wa Mashirika ya Umma(PPF).

CHANZO;GAZETI LA TANZANIA DAIMA LA JUMAMOSI, MACHI 17 MWAKA 2012.

No comments:

Powered by Blogger.