Header Ads

KESI YA UCHOCHEZI KIBANDA,MAKUNGA, YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kuruhusu kuandikwa kwa makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake jana ulimsomea shtaka la kuchapisha waraka huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga.


Sambamba na hilo Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alieleza kuwa mbali na kumsomea mshtakiwa huyo watatu(Makunga) shtaka lake kwasababu Machi 7 mwaka huu, alipounganishwa na hati hiyo kufanyiwa marekebisho na kisha kuwasomea mashtaka mapya washtakiwa hayo,Makunga hakuwepo mahakamani pia unaifanyia hati hiyo marekebisho ya majina ya mshtakiwa wa pili na watatu(Kibanda na Makunga) kwani yalikuwa yamekosewa hapo awali ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo.

Machi 7 mwaka huu, hati hiyo ya mashtaka majina ya Kibanda na Makunga yalikuwa yamekosewa kuandikwa.Jina la Kibanda lilikuwa likisomeka kuwa ni Kibamba na Makunga lilikuwa likisomeka Maingu.

Wakili Kaganda akimsomea shtaka hilo ambalo kwa mujibu wa hati ya mashtaka ni shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake, ambalo ni la kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti Na.229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwamba Novemba 30 mwaka 2011, Makunga akiwa na wadhifa huo alichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011.

Hata hivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo na Hakimu Lema alisema masharti ya dhamana ni kama yale yaliyoyatoa Desemba 8 mwaka 2011 ambayo yalishatekelezwa na washtakiwa wenzake, ambapo ili apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya shilingi milioni tano kila mmoja, na kuwasilisha hati ya mali isiyoamishika yenye thamani hiyo ya fedha, kuripoti mara moja kwa mwezi katika Kituo Kikuu cha Polisi na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, masharti ambayo yalitimizwa na Makunga na yupo nje kwa dhamana.

Wakili Kaganda pia aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuwa imekuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini hawapo tayari kuwasomea kwa jana na kwamba wanaiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kuja kuwasomea maelezo hayo ya awali.

Ombi ambalo lilikubaliwa Hakimu Lema ambaye aliairisha kesi hiyo hadi Aprili 24 mwaka huu, kwaajili ya washtakiwa kuja kusomewa maelezo ya awali.

Machi 7 mwaka huu, Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando ,Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na John Mhozya na Frank Mwilongo.

Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 27 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.