Header Ads

JK ALINIPA IDHINI YA KUNUNUA JENGO LA UBALOZI-MAHALU




Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyempatia mamlaka ya kisheria (Special Power of Attoney) ya kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchi Italia kwa kutimia njia ya mikataba miwili kwa thamani ya Euro 3,098,034
.


Sambamba na hilo Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta ametupilia mbali pingamizi la wakili wa serikali Ponsian Lukosi,Ben Lincol lilotaka mahakama hiyo isipokee barua ya Machi 21 mwaka 2001 iliyoandikwa na Mahalu kwenda kwa Kikwete ambaye wakati huyo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akimwarifu kuhusu jengo hilo litauzwa na mwenye jengo kwa mikataba miwili.

Wakili Lukosi alidai kuwa barua hiyo ilikuwa ni ya siri na binafsi na siyo ya kiserikali, hoja mbayo hakimu huyo aliitupilia mbali kwa maelezo kuwa barua hiyo ni ya kiserikali kwani ina nembo ya serikali na inatunzwa na ofisi za serikali na kwamba nakala ya barua hiyo ya Mahali aliituma pia kwa viongozi wengine wa serikali na akasema anaipokea barua hiyo kama kielelezo cha upande wa utetezi.

Profesa Mahalu alitoa maelezo hayo kwa maandishi jana wakati akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake Mabere Marando mbele ya Hakimu Mkazi Elvin Mugeta.Ambapo jana mshtakiwa huyo alimaliza kujitetea.

Profesa Mahalu ambaye tangu aanze kujitetea amekuwa akitumia nyaraka mbalimbali za serikali ambayo ni mawasiliano baina yake na viongozi wengine wa serikali kuhusu ununuzi wa jengo hilo lilivyonunuliwa kwa kutumia mikataba miwili ambapo alidai kuwa akiwa Balozi mjini Rome,Kikwete ambaye wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alimpatia nguvu maalum ya kisheria ya (Special Power of Attoney) ya kununua jengo hilo kwa thamani ya Euro Milioni tatu ambapo nguvu hiyo ya kisheria inaonyesha kutolewa na rais huyo Septemba 2002 na kwamba aliipokea na kuifanyia kazi kwa vitendo na ilikuwa na saini ya rais Kikwete.

Aliendelea kueleza kuwa Machi 24 mwaka 2004 , alimwandia barua waziri wake Kikwete na kwamba ndani ya barua hiyo alikuwa ameambatanisha nyaraka zote za ununuzi wa jengo hilo la ubalozi ikiwemo mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo na kipindi hicho tayari jengo hilo lilikuwa limeishanunuliwa na serikali na kwamba nakala ya barua hiyo nilimtumia Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Mhasibu Mkuu wa Serikali wa wakati huo Brandina Nyoni na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo na akaomba atoe barua hiyo kama kielelezo ambapo pia mahakama ilikipokea barua hiyo kama kielezo.

“Mheshimiwa hakimu Aprili 23 mwaka 2008 shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri ambaye alikuwa ni mhasibu wa ubalozi huo Steward Migwano alipotoa ushahidi wake alileta nyaraka mikataba hiyo miwili na nyaraka za kibenki za kibalozi zilizokuwa zikionyesha jinsi ofisi ya ubalozi ilivyopokea fedha toka serikali ya Tanzania na jinsi ubalozi wetu ulivyokuwa ukizitoa fedha hizo kwa awamu na kwenda kumlipa mmiliki wa jengo hilo kwa awamu na itoshe kusema kuwa ushahidi wa shahidi huyo wa tatu wa jamhuri unaunga mkono utetezi wangu;

“Na Oktoba 24 mwaka 2008 shahidi wa tano ambaye ni Mchunguzi toka TAKUKURU, Isidori Kyando alitoa ushahidi unaotofautiana na ushahidi wangu na hotuba ya Kikwete aliyoitoa Bungeni Agosti 3 mwaka 2004 , ambapo shahidi huyo alidai yeye anautambua mkataba mmoja tu wa (Official price) ambao unaonyesha jengo hilo lilinuliwa kwa Euro Milioni 1,032,913.80 “ alidai Profesa Mahalu.

Profesa Mahalu alidai ushahidi wa Kyando unatofautiana na ushahidi wake na hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete katika mkutano wa 16 Kikao cha 39 cha Bunge, Agosti 3 mwaka 2004, ambapo wao wawili yaani (Mahalu) na Kikwete kwa maandishi walieleza kutambua kuwa jengo hilo lilinuliwa kwa mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni ule wa (book value ) ambao unaonyesha jengo lilinuliwa kwa Euro milioni 1.032,913.80 na kisha jengo hilo katika tarehe tofauti likaja kununuliwa katika mkataba wa pili uotambulika kwa bei ya kibiashara(Commercial price) ambapo katika mkataba huo wa pili unaonyesha jumla jengo hilo lilinuliwa kwa thamani ya Euro 3,098,034.

Aidha aliendelea kueleza kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake bungeni kuhusu sakata la ununuzi wa jengo hilo kwa mikataba miwili, alilieleza bunge kupitia Hansard ya bunge ukurasa wa 166, Rais Kikwete alisema “Naibu Spika mwaka 2001-2002 Wizara ya Mambo ya Nje ilinunua jengo hilo la ubalozi kwa thamani ya Euro 3,098,034 ili serikali iweze kuondokana na mzigo wa kupanga ofisi na kwamba ununuzi wa jengo hilo ulifuata taratibu sote za serikali na na kwamba tayaribu hizo zilipata baraka za wizara ya yake ,wizara ya ujenzi Fedha na kwamba Machi 6 mwaka 2002 serikali ilituma fedha za awali kwaajili ya manunuzi hayo katika ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Italia, na akaomba kumbukumbu hiyo ya bunge ipokelewa kama kielelezo ambapo Hakimu Mugeta alikipokea.

“Kwa hiyo mheshimiwa hakimu utaona bei ya manunuzi ya jengo hilo iliyotajwa na Rais Kikwete Bungeni na bei ya jengo hilo niliyoitaja mimi na yule shahidi wa upande wa Jamhuri Migwano zinafanana “alidai Mahalu.

Hata hivyo alidai kuwa anashangazwa na upande wa jamhuri kumfungulia kesi hiyo ya uhujumu uchumi kuhusu ununuzi wa jengo hilo kwasababu hadi upande mashtaka unaifunga kesi yake mwaka juzi, haujaleta ushahidi unaonyesha aliyekuwa akiuza jengo hilo alikuwa hajapa fedha hizo ambazo zilitumwa na serikali katika ubalozi wa Tanzania nchini Italia ili wamlipe muuzaji wa jengo lile na pia upande wa mashtaka haujaleta ushahidi wowote wa maneno au nyaraka unaonyesha serikali iliwahi kukataza au kulalamikia utaratibu wa ununuzi wa jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili:

“Na ili kuithibitishia mahakama hii kuwa nchini Italia, kununua ardhi, jengo au kupangisha jengo mikataba miwili haizuwi kisheria naomba nitoe kitabu kilichoandikwa na mwandishi aitwaye Tobias Jones ambacho kina kichwa cha habari kisemacho “ The Dark Hearty Italy’ kama kielelezo.

“Ukurasa wa 139-140 wa kitabu hicho,Mheshimiwa hakimu, mwandishi huyo raia wa Italia, anaeleza wazi kuwa suala la mikataba miwili nchini ni la kawaida na wananchi wa Italia wamekuwa wakiifuata utaratibu huo ambao hauzuiwi kisheria na akafafanua kuwa mkataba wa kwanza ambao unaitwa (book value) ndiyo mwisho wa siku unakuwa hati ya mali liwe jengo au ardhi na kwamba katika ununuzi wa kupitia mikataba miwili risiti ya ununuzi inakuwa ni moja tu”alidai Profesa Mahalu.

Hata hivyo wakili Marando alipomuuliza Mahalu kuwa amewahi kupata rekodi yoyote ya ubadhirifu wa mali ya umma, Mahalu alikanusha hilo na kuonyesha yeye ana rekodi nzuri tena ya kimataifa zinazoonyesha yeye ni mhadilifu na akatoa zaidi ya medani tano mahakamani hapo alizotunukiwa na Raia wa Italia, na marais wengine dunia na mashirika mengine ya Kimataifa kwa ajili ya uhadilifu, uchapakazi wake na jitihada zake za kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali ya Italia na Tanzania.

Wakili Marando alidai kuwa huo ndiyo mwisho wa utetezi wa Mahalu na Wakili wa Jamhuri Lukosi akadai kuwa hayupo tayari jana kuanza kumhoji mshtakiwa huyo na kwamba anaomba kesi hiyo iarishwe ili aweze kwenda kujiandaa ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Mugeta ambaye aliarisha kesi hiyo hadi Machi 21 mwaka huu, ambapo siku hiyo upande wa Jamhuri utaanza kumhoji mshtakiwa huyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi Mosi mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.