KIBANDA ABADILISHWA HATI YA MASHTAKA
Na Happiness Katabazi
UPANDE wa Jamhuri katika kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba jana ulishindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao na badala yake umeibadilisha hati ya mashtaka na pia kumuongeza mshtakiwa mmoja.
Katika hatua nyingine kwa mujibu wa hati hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake inayoonyesha imeletwa mahakamani hapo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), Dk.Eliezer Feleshi ambaye aliisaini Machi 6 mwaka huu, majina ya washtakiwa yanasomeka kimakosa kama ifuatavyo Samson Maingu Mwigamba, Absalom Norman Kibamba na Theophil Christian au Maingu.
Wakati majina sahihi ya washtakiwa hao yalipaswa yasomeke kwa usahihi kama ifuatavyo Mangu Samson Mwigamba ,Absalom Norman Kibanda na Theophil Christian Makunga. Lakini mwisho wa siku ni mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutamka vinginevyo kuhusu hati hiyo.
Wakili wa Serikali Elizabeth Kanda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini imeshindwa kufanya hivyo kwasababu inabadilisha hati ya mashtaka na kumwongeza mshtakiwa mwingine ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga na hivyo kufanya kesi hiyo jinai Na.289 ya mwaka 2011.
Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na John Mhozya.
Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake ni la kuchapisha makala hiyo ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Na.229 ya mwaka 2002 , ambapo alidai kuwa Novemba 30 mwaka jana Makunga akiwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Ltd, ilichapisha makala hiyo ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa Askari wote’ ambayo ilichapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima.
Hata hivyo washtakiwa hao wawili yaani Mwigamba na Kibanda ndiyo waliokuwepo mahakamani walikanusha kosa hilo, lakini Makunga hakuwepo mahakamani na wakili Kaganda akaiomba mahakama itoe hati ya wito ya kumuita Makunga mahakamani ili aje asomewe shtaka linalomkabili katika kesi hiyo na kwamba wanaiomba mahakama hiyo iwapangie tarehe ya kujakuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wote hao wa tatu.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Lema alikubaliana na maombi hayo ambayo alitoa amri ya kutoa wito wa kuitwa mshtakiwa wa tatu(Makunga) kuitwa mahakamani na kwamba Machi 26 mwaka huu, kesi hiyo itakuja kwa upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya washtakiwa hao.
Kubadilishwa kwa hati hiyo ya mashtaka jana kumefanya sasa washtakiwa hao kushitakiwa kwa kosa hilo la uchochezi na kuchapisha makala hiyo ya uchochezi kwa kinyume na Sheria ya ya Magazeti ya mwaka 2002 na siyo kama ilivyokuwa hapo awali ambao washtakiwa hao yaani Mwigamba na Kibanda walikuwa wakishtakiwa kwa makosa ya kuchapisha makala iliyokuwa inachochea uasi kwa askari na maofisa wa Jeshi la Ulinzi(JWTZ), Jeshi la Polisi na Magereza kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , kwamba askari hao wasitii amri zinatolewa na makamanda wao.
Desemba 21 mwaka jana, upande wa Jamhuri ulibadilisha hati yake mashtaka kwa kumuongeza mshtakiwa wa pili(Kibanda) na hivyo kufanya jumla ya washtakiwa kuwa wawili yaani Mwigamba na Kibanda.
Ambapo wakili Kaganda alidai washtakiwa alidai wanakabiliwa na kosa moja la kuwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, magereza na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutoendelea kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete kinyume na kifungu cha 46(b),55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Desemba 8 mwaka jana, Mshtakiwa wa kwanza Mwigamba ambaye ndiye aliyeandika makala hiyo inayodaiwa na upande wa Jamhuri kuwa ni uchochezi alifikishwa mahakamani hapo peke yake kwa kosa hilo ambapo mwisho ilipofika Desemba 21 mwaka jana ndipo Jamhuri ilibadilisha hati ya mashtaka kwa kumuongeza Kibanda.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 8 mwaka 2012
No comments:
Post a Comment