Header Ads

LOWASSA UMEANZA MAPAMBANO NA SERIKALI?



Na Happiness Katabazi

MTUME Muhamad (SAW) katika Sura Tul munafikuna alifundisha kwamba mnafiki ana alama tatu. Alama hizo ni: ‘Mnafiki akizungumza huwa ni uongo, akiahidi jambo halitimizi na akiaminiwa hufanya hiana.’


Nimelazimika kutumia nukuu hiyo ya kiongozi wa dini ya Kiislamu kwa kuwa wengi wetu tumekuwa tukisoma, kusikiliza na kufuata maagizo ya viongozi wa kiimani ili tuweze kuwa na maisha bora hapa duniani na huko ahera.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwa nyakati tofauti katika nyumba tofauti za ibada (makanisa) amekuwa akidai kuwapo kwa tishio la bomu la ukosefu wa ajira kwa vijana ambalo likilipuka nchi itakuwa kwenye hatari.

Kiongozi huyo amekuwa akiwaomba maaskofu wa Kanisa Katoliki na mengineyo anayopata nafasi ya kushirki shughuli za kidini kusaidia kutatua tatizo hilo ambalo linaonekana kutovaliwa njuga kikamilifu na serikali.

Lowassa na wananchi wengine wana haki ya kufurahia matakwa ya Ibara ya 18(1) ya Katiba ya nchi ambayo yanatoa haki kwa kila mwananchi kutoa fikra zake pasi kuvunja sheria.

Sitaki kupora haki yake ya kutoa tamko hilo bali ninajiuliza imekuwaje analiona tatizo hilo hivi sasa ilhali yeye alikuwa Waziri Mkuu ambaye alipaswa kuonyesha mfano wa kulitegua bomu hilo?

Chama chake cha CCM ndicho kinaunda serikali ambayo kila kukicha imekuwa ikijinasibu kuzalisha ajira nyingi pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania ambayo sasa yanazidi kudorora badala ya kuboreka.

Ni Lowassa huyu huyu wiki iliyopita alirejea nchini akitokea Ujerumani alizungumza na waandishi wa habari akisema yeye ni mzima wa afya na kwamba yupo tayari kwa ajili ya mapambano yaliyopo mbele yake.

Najiuliza, mapambano aliyoyasema ndiyo haya ya kupambana na serikali ya Rais Kikwete ambayo sasa inalazimika kutumia nguvu kubwa kujibu mashambulizi ya kada wake?

Lowassa alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kundi la wanamtandao waliopigana kufa na kupona mwaka 2005 kuhakikisha Rais Kikwete anaingia madarakani, alimsaidiaje rafiki yake kutegua bomu la ajira kwa vijana?

Ilani ya CCM ya mwaka 2005 na ile ya mwaka 2010 iliweka wazi kuwa iwapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi kitatengeneza ajira kwa vijana, ahadi hiyo sasa imegeuka takwimu zisizo na mashiko.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka, Jumatano wiki hii aliamua kuyakanusha madai ya Lowassa kwa kutumia takwimu alizonazo kuwa nguvu kazi ya Tanzania ni watu milioni 20.6 kati ya watu milioni 37.5, watu milioni 18.3 sawa na asilimia 88.3 wana ajira na kwamba watu laki nane mpaka milioni moja wanaingia katika ajira mpya.

Sasa nimuulize Lowassa ni kwanini anatoa tamko la aina hiyo kila mara wakati serikali ya chama chake imefanya ‘vizuri’ kwenye kutengeneza ajira mpya, kama vigogo wa chama tawala wanakanganyana kiasi hiki mwananchi ashike la nani?

Hivi Lowassa anataka kuuambia umma kuwa zama za ajira nyingi kutolewa na serikali bado zipo? Kama ni hivyo mbona hatukumuona akisimamia utengenezaji wa ajira mpya wakati akiwa waziri mkuu?

Kila kukicha serikali ya CCM imekuwa ikiongeza nguvu na kuijengea uwezo sekta binafsi ambayo imeongeza wigo wa ajira, haya yote Lowassa hayaoni au ana lake jambo?

Kwa mujibu wa tamko hilo la Lowassa, kiongozi huyo anataka umma utafsiri kuwa yeye na serikali ya chama chake cha CCM wameshindwa kutekeleza ile ahadi ya kutoa ajira kwa vijana waliyotuahidi mwaka 2005?

Kama hivyo ndivyo ninamshanga sana Lowassa anavyoendelea kuwa mwanachama wa chama hicho ambacho serikali yake imeshindwa kutekeleza ahadi hadi leo. Katika hili nikisema Lowassa ‘anauhadaa umma’ nitakuwa nimekosea?

Lowassa nilimshuhudia Oktoba mwaka 2010 wakati akinadiwa jukwaani jimboni kwake na aliyekuwa mgombea mwenza wa CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambapo mara baada ya Dk. Bilal kumaliza ngwe yake alipanda Lowassa kunadi sera za CCM na alisema serikali yake imeweza kufanya mengi ikiwemo kuwapatia ajira vijana.

Sasa anapoibukia makanisani na kutoa tamko hilo ambalo limeishapingwa na serikali, kwa kweli nilimshangaa sana, sijui ni kiongozi wa aina gani asiyekumbuka kile alichokiahidi miaka miwili iliyopita au ndiyo mikakati yake ya kuelekea 2015?

Nimalizie kwa kumshauri mzee wangu Lowassa, fikiri kwa kina kila unaloambiwa au unalotaka kusema ili usije ukajijengea mazingira ya ‘kuumbuka’ kama ilivyo hivi sasa.

Inawezekana ziara zako hizo za kila kukicha makanisani ndiyo miongoni mwa mbinu ulizopewa na kikosi kazi chako ambacho kinadhani unaweza ukapenya kwenye chekeche la kuwania urais mwaka 2015, lakini ni vema akili za kuambiwa ukachanganya na zako.

Huku mitaani baadhi ya marafiki zako wamekuwa wakihusisha kauli zako na kuwania urais. Hata hivyo sijakusikia ukitamka kuwania nafasi hiyo.

Nakuomba uwaangalie watu wanaokusaidia kwenye mikakati ya kuwania uongozi wa nchi wasije wakakuangusha kabla hujaangushwa na wananchi au makada wenzako ambao wanajua kinaga ubaga unachokifanya.

Binafsi siamini kama kuna jipya ulilotuonyesha ili utushawishi wewe ni mtu mpya na unaweza kulikabili tatizo la ukosefu wa ajira, tofauti na njia zinazotumiwa na serikali ya chama chako.

Mimi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache tulioalikwa katika mkutano wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete, mwaka 2005 uliofanyika nje ya ofisi ya Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Pwani.

Katika mkutano huo Rais Kikwete alitangaza rasmi nia yake ya kuomba apitishwe na chama chake ili awanie kugombea urais, kiongozi huyo alisema ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka.

Kwa hiyo kimsingi tukubaliane tamko hilo si jipya katika masikio ya watu ambao tunafuatilia kwa karibu matamshi na mienendo ya viongozi wetu siku hadi siku.

Kikwete alipitishwa na CCM kuwa mgombea urais, wakati wa kampeni za mwaka 2005 alituhakikishia Watanzania kuwa akiingia Ikulu atahakikisha nyumba za serikali ambazo ziliuzwa kwa watumishi wa umma atazirejesha serikalini, ahadi ambayo hadi sasa ameshindwa kuitekeleza kwa vitendo.

Wakati akitoa ahadi hii alikuwa ni mjumbe wa baraza la mawaziri enzi za utawala wa Rais Benjamin Mkapa na uuzwaji nyumba hizo ulibarikiwa na baraza hilo, ikimaanisha na yeye alibariki ila kwa sababu alikuwa akizihitaji kura za wananchi na wananchi wengi ni watu tunaopenda kudanganywa na kutotaka kuchanganua mambo tulifurahia mno ahadi hiyo.

Kwa mifano hiyo hai, ambayo binafsi nimeishuhudia kwa macho, nataka nitoe rai kwa wananchi wenzangu wasilipe uzito tamko la Lowassa, kwani alikuwa mtumishi wa muda mrefu serikalini, CCM na muda wote umma umekuwa ukipigia kelele matatizo mbalimbali, lakini yeye na viongozi wenzake walikuwa wakitubeza.

Ila kwa kuwa hivi sasa hana yale madaraka ya juu yaliyokuwa yanampa upofu wa kutoona wananchi tunakabiliwa na hali mbaya ya ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira, ndiyo leo hii anaanza kuuaminisha umma yupo pamoja nao!

Tusidanganyike, kwani nimejifunza kitu kimoja, watu wengi waliowinda madaraka wanajifanya ni wakosoaji wa uendeshaji wa serikali kila kukicha na wachapakazi, lakini siku wakipewa madaraka watu wa aina hiyo hugeuka mabubu na kuacha kupigania haki za wanyonge ambapo awali wakati wakisaka madaraka walituahidi wangetupigania.

Mifano ni mingi, wala si ya kutafuta. Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Margaret Sitta, enzi zile za waziri wa Elimu akiwa, Joseph Mungai, aliwapigania sana walimu, lakini Rais Kikwete alipoingia madarakani na kumteua kuwa waziri, hatukumsikia tena mwanamama huyo akiendeleza harakati zake za kumkomboa mwalimu hapa nchini.

Kwa hiyo ni wazi kabisa hata Lowassa akiukwaa tena uongozi hatutamsikia tena akilalamikia bomu la ukosefu wa ajira kwa vijana, bali atakuwa akikerwa na kauli za aina hiyo zitakazokuwa zikitolewa na wengine.

Mbinu anayoitumia kiongozi huyo ya kwenda kwenye nyumba za ibada ‘kujisafishia njia’ imepitwa na wakati, haitakusaidia kukufikisha unakotaka kufika.

Mbinu za aina hiyo zilishatumiwa na Rais Kikwete katika hatua zake za mwisho, katika kampeni zake na kweli akafanikiwa na utambue kuwa mbinu iliyotumiwa na Kikwete kuingia madarakani ni nadra mbinu hiyo hiyo kuitumia wewe ili ufanikiwe pia.

Unaweza kubuni mbinu nyingine, haujachelewa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 25 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.