Header Ads

MADAKTARI,WAUNGWANA HAWASIFIWI USHENZI



Na Happiness Katabazi

HII ni mara ya pili narudia kuandika makala hii ambayo ninaendelea kusisitiza mgomo wa madaktari uliofanyika Februali mwaka huu na mgomo mwingine ulioanza Machi 7 mwaka huu ,huenda una ajenda mbaya nyuma yake na tusipokuwa macho ipo siku tutajikuta unatufikisha baya kama taifa.


Na kwamba mgomo huu haramu wa Februalia mwaka huu , ulilelewa na serikali yetu na ndiyo maana leo hii madaktari hao wameanza kuwa na kiburi cha kutoa amri kwa rais Jakaya Kikwete kutaka aridhie mawaziri hao wajiuzuru ama sivyo watagoma tena.
Madaktari hao wanaposhinikiza Waziri wa Afya Dk.Haji Mponda na Naibu wake Dk.Lucy Nkya wajiuzuru hadi kufikia jana,ni wazi wanamshikiniza rais wa nchi awawajibishe hao wateule wake na aridhie kujiuzuru kwao hata kama yeye haoni haja kwa wateule wake wajiuzuru.

Ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasomeka hivi “Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote , isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote”.
Kwa hiyo ibara hiyo inampa uhuru rais katika utendaji kazi na shughuli zake hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote isipokuwa pale anapotakiwa na Katiba na Sheria. Kwahiyo kumbe mashinikizo hayo ya madaktari na wanaharakati kumshinikiza rais awawajibishe mawaziri, rais halazimiki kisheria kufuata ushauri huo wa madaktari.

Nalazimika kuamini hivyo kwani mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania(MAT), Dk.Namala Mkopi alizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari uliofanyika Dar es Salaam, ambapo alisema yeye na chama chake wameazimia kugoma kuanzia jana ikiwa Waziri wa Afya, Dk.Haji Mponda na Naibu wake Dk.Lucy Nkya hawatajiuzuru nyadhifa zao kwani mgomo wa awali ulisababisha vifo vya wananchi wengi na kwamba mawaziri hao ni kikwazo katika majadiliano yao na serikali.

Dk.Mkopi alikwenda mbali zaidi na kujinasibu kuwa mgomo huo utakuwa ni mgomo mkubwa na wa aina yake.Tamko hilo linasikitisha na kukera.

Wakati Dk.Mpoki na hao madakatri wenzake wakifikia uamuzi huo serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda Jumatatu wiki hii, amenukuliwa na gazeti moja akisema anasikitishwa na uamuzi huo wa wanataaluma kwasababu serikali ingali ikiyafanyia kazi madai yao.

Na Juzi jioni Pinda amezungumza na waandishi wa habari kuhusu tishio hilo la mgomo na akawataka madaktari hao wasigome na kwamba sheria za nchi zinakataza baadhi ya wanataaluma wa aina fulani kugoma na kwamba serikali imejipanga kukabiliana na hali mgomo huo endapo utatokea.

Mapema kabisa naomba nieleweke kuwa madai yao ya kuboreshewa maslahi yao na kuboreshewa vitendea kazi kwa wanataaluma hao siyapingi.

Ninachopingana na chama hicho ni hali yake ya hivi sasa kutaka kuiweka serikali mifukoni mwao na wao ndiyo wawe wenye sauti ya mwisho na amri ya kuiamrisha serikali ifanye wanachokitaka wao na kwa muda wanaoutaka wao wakati kada nyingine kama walimu ambao ndiyo wamewatoa hao madaktari umbumbumbu ambao wana maisha mabaya sana kuliko wao lakini wanatumiaga busara sana katika kudai maslahi yao.

Ebu watanzania wenye akili timamu na tunaofikiri sawa sawa ,tuamke usingizini na tuanze kujiuliza huu ni mgomo kweli wa madaktari au kuna manyang’au ya kisiasa yenye uchu wa madaraka yanayotaka nchi hii isitawalike yameamua kuwatumia baadhi ya madaktari kuanzisha migomo kila kukicha ili serikali iliyopo madarakani ionekane ni dhahifu na imeshindwa kufanya kazi na wananchi wenzetu wapoteze maisha kwa kukosa huduma za kitabibu?

Aiingii akilini kabisa kwa madaktari ambao ni wasomi kwa ridhaa yao walianza kukaa meza moja ya majadiliano na serikali ili waweze kuyapatia ufumbuzi matatizo yao tena ndani ya kipindi kifupi tu serikali inasema ndiyo inaanza kuyafanyia kazi matatizo yao wanaibuka tena na kutaka mawaziri hao wajiuzuru mara moja na kwamba hivyo ndivyo walivyokubaliana na serikali kupitia Pinda na madaktari walitiliana saini Februali 9 mwaka huu.

Hivi nyie madaktari wa kisasa mmeona mgomo ndio dili sana? Hivi aliyeajiriwa katika hospitali kutoa huduma za kitabibu ni madaktari au waziri Mponda na Dk.Nkya?
Aliyegoma kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa Februali mwaka huu, kwa zaidi ya wiki tatu na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma na wengine kufa kwa kukosa huduma ya kitabibu ni madaktari au mawaziri hao?

Sasa kwani huyu Dk.Mkopi anataka kujiepusha na hilo kuwa hata wao madaktari kama ni hivyo nao wanapaswa kuwajibika kwanza kwani ni wao waliutangazia umma kuwa wamegoma na wataalamu wa sheria wanatueleza mgomo wao wa awali ni batili kisheria?
Sawa mawaziri wanaweza kuwajibika baada ya kubainika kuwa walishindwa kusimamia vyema ofisi wanazoziongoza na mwisho wa siku uzembe huo ukasababisha madhara kwa wananchi.

Lakini vipi kuhusu nyie madaktari ambao mnaviapo vyenu ambacho vinawazuia msigome lakini miongoni mwenu mlisaliti viapo vyenu na mkagoma mbona na nyie hatuwasikii mkijisema kuwa katika hilo mlikiuka maadili ya kazi yenu?

Lakini hao wanaharakati na hao madaktari waache unafki wa kushinikiza waziri na naibu wake wajiudhulu peke yao bila kushinikiza na madaktari nao wachukuliwe hatua ya kukiuka viapo vyao kwa kugoma na kusababisha baadhi ya wananchi wenzetu kukosa huduma za kitabibu.

Serikali na wananchi kwa ujumla tuwe macho na madaktari wa aina hii kwani hawana msimamo na siku zote mtu au kiongozi yoyote asiye na msimamo mwisho wake anawaweza kutufikisha pabaya.

Ningali nikikumbuka katika mgomo wa awali, ni hawa hawa madaktari walijinasibu mfululizo kwenye vyombo vya habari kuwa kama hawataongezewa mishahara na kuboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hawatasitisha mgomo, lakini Februali 9 mwaka huu, Pinda alipokwenda kuzungumza nao pale Hospitali ya Muhimbili akatangaza kuwa serikali imewaongezea posho na akaridhia kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Brandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali Deogratius Mtasiwa kupisha uchunguzi , madaktari hawa walichekelea na wakarejea kazini.

Zilienea taarifa ambazo hadi sasa hazijathibishwa kuwa katika ule mgomo wa awali ni Brandina Nyoni ndiye haswa alikuwa anatakiwa aondolewe madarakani.Na uamuzi wa Pinda wa kumsimamisha kazi mama huyo ambaye baadhi ya madaktari wanamtambulisha kuwa ni mwanamke mbabe ni hatua ya mafanikio ya ajenda ya baadhi ya madaktari hao iliyokuwa imejificha.

Kuna baadhi ya watumishi wa Wizara ya Afya wanaeleza kuwa Nyoni alikuwa ni mwiba mkali na aliziba mirija ya fedha zisitumike ovyo na alipenda mambo yote yafanyike kwa kufuata utaratibu na siyo kienyeji na wengine walimtuhumu mama huyo si msafi.Vyovyote iwavyo minaamini ipo siku ukweli wa mambo utakuja kufahamika.

Kwa mtazamo wangu nasisitiza kuwa huenda kuna ajenda ya siri iliyojificha katika sakata hili la madaktari kwani aingii akilini kuwa madaktari hawa wamekubaliana na serikali matatizo yao yafanyiwe kazi na majadiliano baina yao yanaendelea ,wakati matatizo yao yanaanza kufanyiwa kazi wanatangaza kuibua balaa jingine la mgomo.

Huu ni uhuni na ufedhuli wa aina yake na serikali yoyote imara kokote duniani isingeweza kuuvumilia kwani mwisho wa siku tunaokuja kupata madhara makali ya mgomo huu ni sisi wananchi ambao hatuna uwezo wa kifedha wa kwenda kutibiwa hospitali binafsi za zile za nje ya nchi.

Niwaulize maswali wewe Dk.Steven Ulimboka na Dk.Namala Mkopi kama mnadini na kama dini zenu zinaruhusu kupata mshahara mnono kupitia vifo vya wagonjwa vilivyotokana na mgomo wa awali na mliohuamasisha?

Wewe Dk.Ulimboka,DK.Mkopi itokee kipindi cha mgomo mliouamasisha baba zenu,mama zenu waliowazaa,watoto wenu,wake zenu wanaitaji huduma ya upasuaji ya haraka ,mtakuwa tayari kutowapatia huduma kwasababu mpo kwenye mgomo? Bila shaka hamtakuwa tayari kwasababu wahenga walisema ‘damu nzito kuliko maji.

Sasa kama hivi ndivyo muwe na roho za utu,msipende maisha manono au kujipatia umaarufu kupitia migomo ambao mwisho wa siku sisi wananchi ambao kodi zetu ndiyo zimewasomesha na leo ndiyo zinawalipa mishahara ndiyo tunaoathirika.

Endapo rais Jakaya Kikwete ataridhia hao mawaziri wake Dk.Mponda na Dk.Nkya wajiuzuru kwaajili ya shinikizo la madaktari hao ambao hivi sasa wanajiona taaluma yao ni bora kuliko taaluma zingine hapa nchini , basi siku si nyingine yeye Kikwete na waziri mkuu Pinda nao watajikuta wakijiuzuru nyadhifa zao kwa mashinikizo ya aina hiyo.

Na mwisho wa serikali ya awamu ya nne itaweka rekodi ya viongozi wake kujiuzuru mara kwa mara, na kodi za wananchi zitakuwa zikitumika kuwalipa mafao na kuwatunza wastaafu hao.

Ikumbukwe kuwa hata kipindi kile cha mwaka 2008, wakati Waziri mkuu alikuwa Edward Lowassa, kuna watu waliokuwa hawataki Lowassa aendelee kuwa waziri mkuu kwa sababu anaandamwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, na watu hao walifanikiwa kupenyeza ajenda yao kwenye vyombo vya habari, mitaani na kwingineko na hatimaye waasisi wa ajenda hiyo walifanikiwa kumjaza jazba Lowassa na hatimaye mwisho wa siku bungeni badala ya kujibu hoja zilizowasilishwa na Kamati ya Bunge kuchunguza mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC, akaishia kusema kusema ‘nimesikitishwa sana, nimeuzunishwa sana na nimekasilishwa sana….’ Akatangaza kujiuzuru wadhifa wake na kisha Pinda akatangazwa kumrithi.

Kwa maana hiyo basi mgomo huu wa madaktari vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa vifanye kazi yake kikamilifu na kubaini mgomo huo ni wa madaktari kweli au kuna watu wanaotaka madaraka ya urais na kuonyesha serikali hii imeshindwa kuongoza.

Natoa rai kwa madaktari wote wawe makini na vinara wa migomo hiyo ya madaktari kwani tayari kuna taarifa za chini chini kuwa vinara wa migomo hiyo ya madaktari wanatarajia kuingia kwenye ulingo wa siasa kwenye baadhi ya majimbo na kwamba wanatumia migomo hiyo kujijengea umaarufu miongoni mwa wa Tanzania kuwa wao ni viongozi shupavu na wanastahili kupewa nyadhifa za uongozi kupitia damu za watanzania maskini na migongo ya madaktari wasiyojua siri iliyojificha katika migomo hiyo.

Naomba serikali iwachukulie hatua viongozi wa mgomo huo kwasababu wanachokifanya hakina tofauti na maofisa wenye nyadhifa za juu serikali ambao walifikishwa pale Mahakama ya Kisutu kwa makosa mbalimbali ya jinai kama matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, uhujumu uchumi na wizi.lakini hawa vinara wa migomo ya madaktari kwa mtazamo wangu naona wanafanya makosa ya wazi ya mauaji ya kukusudia kwani daktari au nesi anapokataa kumtibia mgonjwa ni wazi anataka mgonjwa huyo afe.

Kwanza vinara hawa wa mgomo mnapotembea mkae mkijua mnanuka damu za watanzania maskini waliokufa katika mgomo wa awali.Na kana kwamba hiyo mmeona haiwatoshi mnataka damu nyingine kwa kuitisha mgomo wa pili ambao mmepanga uanze jana.
Ushauri wangu kwenu nyie madaktari kama mnaoa fani ya udaktari hailipi,ingieni kwenye ulingo wa siasa rasmi kama walivyofanya madaktari wenzenu na baadhi ya wasomi wa ngazi juu wenye shahada mbili na tatu.

Ikumbukwe kuwa baadhi ya marais waliowahi kushika nyadhiza za urais katika baadhi ya nchi walikuwa wakitumia vyama vya wafanyakazi kuhamasisha migomo na tafrani kila kukicha kwa serikali iliyopo madarakani na kwa kuwa vyama hivyo vilikuwa na nguvu mwisho wa siku vilifanikiwa kuwang’oa marais waliokuwa madarakani na kisha marais waliokuwa wakivitumia vyama hivyo vya wafanyakazi wakafanikiwa kushika nyadhifa za urais.

Na mfano wa marais waliojijenga kupitia migomo na kufanikiwa kupata madaraka ya nchi ni rais wa Zambia, marehemu Fredrick Chiluba, Waziri Mkuu wa sasa wa Zimbambwe Morgan Shivangilai na wengine wengi.

Sisi kama Tanzania tusijidanganye kwamba hilo halitaweza kutokea hapa nchini kwakuwa hatujampa mungu rushwa, kwani akili, tabia, na roho za Watanzania wengi hivi sasa zimebadilika wengi wetu tumekuwa na tamaa ya kupata madaraka, mali kwa njia isiyompendeza mungu na tumekuwa na roho za kikatili kama hawa visokorokwinyo wanaoongoza mgomo wa madaktari na hatupendani,tumekuwa mabingwa wafitina na wanafki kama ilivyokuwa miaka nyuma,tumeanza kukumbwa na tabia ya ubinafsi na umimi.

Nimalizie kwa kuwakumbusha vinara wa mgomo wa madaktari usemi wa wahenga usemao ‘muungwana asifiwi ushenzi, bali usifiwa kwa matendo yake yaliyomema’.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com
. Machi 9 mwaka 2012

1 comment:

mohammedzahor said...

Umesema vizuri , naomba nikupongeze kwa ujasiri na umakin wa kujenga hoja , HONGERA kwa kututetea sisi wanyonge wa Taifa hili. mashujaa wa aina yako ni wachache.
Mungu yu pamoja nawe na tunamuomba akuzidishie umri umakini na umahiri wa kuweza kujali ktetea na kusimamia haki za wanyonge. Mana vijana wetu wamejisqhau

Powered by Blogger.