ANTHONY MTAKA
Rais mdogo zaidi riadha duniani
.Apania kuirejesha Tanzania katika ramani
Na Happiness Katabazi
MEI 20 mwaka huu, Chama cha Riadha Tanzania (RT), kiliandika historia mpya baada ya kumchagua kijana mwenye umri mdogo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya (DC), ya Mvomero, Anthony Mtaka (30), kuwa Rais mpya wa chama hicho.
Mtaka anaweza kuingia katika rekodi ya kuwa rais mdogo zaidi miongoni mwa nchi wanachama wa Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Yafuatayo ni mahojiano ya ana kwa ana, aliyofanya mwandishi wa makala hii na Mtaka, kuhusu alivyojipanga kuleta mageuzi ya maendeleo katika chama hicho, ambapo licha ya mchezo wa riadha kuwa na historia iliyotukuka katika kuitangaza Tanzania kimataifa, miaka ya hivi karibuni umedorora.
Swali: Umeupokeaje ushindi wa kuwa Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT)?
Jibu: Binafsi nimeupokea kwa furaha, nikiwa pia na utayari wa kuzikabili changamoto za mageuzi ya riadha nchini.
Swali: Wapenzi wa riadha nchini, watarajie kupata na mageuzi yapi ya kimaendeleo katika kipindi hiki cha uongozi wako?
Jibu: Kikubwa wapenzi wa riadha watarajie mafanikio, japo itachukua muda kuyafikia, kwani riadha ya Tanzania inahitaji mabadiliko na mageuzi ya kimfumo katika chombo chenyewe na baadaye kuwapata wanariadha mahiri wa kutufaa kama tuliowahi kuwapata miaka ya nyuma.
Ahadi yangu kwa wapenzi wa riadha nchini ni kutupa muda mimi na wenzangu tuliochaguliwa, kuhakikisha tunaleta mapinduzi yenye tija katika mchezo huu wa riadha nchini; natambua watu wanahamu ya kuona medali, lakini hazitakuja kwa usiku mmoja, tuko kwenye mipango ya muda mfupi na mrefu, kuhakikisha mashindano yajayo nchi yetu inaondokana na kuwa msindikizaji.
Swali: RT imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, je umejipangaje kuzitatua?
Jibu: Ni kweli zipo changamoto nyingi, mimi kama rais na wenzangu, tunao utayari wa kuzitatua tukianza na katiba inayokidhi mahitaji ya riadha ya sasa, jambo ambalo ndani ya miezi mitatu panapo majaliwa tunaamini tutakuwa tumelikamilisha.
Swali: Unauzungumziaje uchaguzi mkuu wa RT uliofanyika Mei 20 mwaka huu? Je, ulikuwa wa uhuru na haki?
Jibu: Uchaguzi ulikuwa wa uhuru na haki, kila mgombea alikubaliana na matokeo na kila mmoja aliridhika na mwenendo wa zoezi zima la uchaguzi, kwa maana ulitawaliwa na uwazi, usio na mizengwe wala harufu ya rushwa.
Mpaka sasa, wagombea walioshinda na kushindwa tumebaki marafiki na nina imani watakuwa msaada kwangu mwenyewe na safu yetu ya uongozi, itakapobidi tutawashirikisha kupata ushauri na uzoefu wao, kamwe hatutasita kufanya hivyo.
Swali: Hivi karibuni uliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, je utawezaje kutenda kazi za ukuu wa wilaya na zile za riadha?
Jibu: Ni kweli nimeteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero. Jambo ambalo namshakuru sana Rais kwa kuniamini na kuniteua, nami namhakikishia sitamuangusha, kama ambavyo nawahakikishia wananchi wa Mvomero kwamba sitawaangusha katika utekelezaji wa majukumu yangu. Ukuu wa wilaya ni kazi ya kila siku.
Nafasi ya urais katika riadha ni kazi ya vikao, si utendaji wa kila siku, mimi kama rais nabaki kuwa mwendesha vikao, mtoa dira na pia haya yote nayafanya nikisaidiana na wenzangu, makamu wangu wawili wa rais, William Kallage anayeshughulikia mambo ya utawala na Dk. Hamad Ndee, anayeshughulikia ufundi.
Katibu Mkuu, Suleiman Nyambui, Katibu Msaidizi, Ombeni Zavalla, Mhazini, Is-Haq Suleiman huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mwinga Mwanjala, Meta Petro, Peter Mwita, Rehema Killo, Lwiza John, Zakaria Barrie, Zakaria Gwanda, Robert Kalyahe, Christian Matembo na Tullo Chambo.
Katika utaratibu huu ni dhahiri majukumu yangu ya ukuu wa wilaya hayataathirika na kazi za Chama cha Riadha, sambamba na hilo, natoa rai kwa Watanzania kuchagua watu wenye anuani, ama za ajira au vipato vinavyoeleweka, hasa kwenye hizi taasisi za michezo ili kuepuka waganga njaa, ambao siku zote wanageuza vyama vya michezo kuwa mahala pa kujipatia vipato vyao na kujikuta michezo inakufa kwa migogoro isiyokwisha kila siku.
Mimi ni Mkuu wa Wilaya, Makamu wangu Kallaghe yuko benki ya NBC na Dk. Ndee ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hata kamati yetu utendaji kwa sehemu kubwa inaundwa na watumishi wa umma, sekta binafsi na wadau wa riadha wenye majukumu yao ya kuwaingizia kipato, jambo linalotupa moyo wa kuona ufanisi katika mipango yetu.
Swali: Umeandika historia mpya ya kuwa rais kijana wa chama cha riadha, je umejipanga vipi kuuthibitishia umma kuwa vijana wakipewa nafasi za uongozi wanaweza?
Jibu: Ni kweli nimeandika historia, si tu Tanzania bali katika riadha ya dunia, mimi ndiye Rais mdogo zaidi nikiwa na miaka 30, ninayeongoza chama cha riadha katika nchi.
Napenda kuwahakishia Watanzania kwamba, sitawaangusha vijana wenzangu katika uaminifu na uwajibikaji, ni suala la muda lakini naamini chini ya uongozi wangu, riadha itahuishwa upya na matunda yataonekana, kikubwa wadau watuunge mkono, tunahitaji kuona eneo hili linazalisha ajira na kipato kwa vijana wa Kitanzania kama ambavyo soka, muziki, uigizaji na michezo mingine ilivyowakwamua kutoka katika umaskini wa kipato.
Swali: Wananchi wa Mvomero watarajie nini kutoka kwako?
Jibu: Kama mkuu wao wa wilaya, wategemee utumishi wangu wa dhati kwao, changamoto kubwa ni kuhimiza na kusimamia shughuli za maendeleo, nawaomba waniunge mkono, kuhakikisha vipaumbele vya elimu, afya, kilimo, migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, kwa pamoja vinapata suluhisho lenye afya kwa wanajamii wa Mvomero.
Lakini pia, kama rais wa riadha, wana Mvomero watarajie hamasa kubwa katika michezo, hasa ikizingatiwa Mbunge wa Mvomero, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, ni mwanamichezo mahiri, kwa pamoja wana Mvomero watarajie mafanikio katika shughuli za maendeleo na michezo.
Swali: Ni mikakati gani mipya ambayo unayo na unaamini watangulizi wako katika chama cha riadha hawakuwa nayo, ili hatimaye mchezo wa riadha uweze kutambulika na kuheshimika ndani na nje ya nchi?
Jibu: Kikubwa uongozi uliopita ulifanya mengi mazuri, chini ya uongozi wangu na wenzangu, katika yote tutajitahidi walau turudishe mashindano ya riadha ya taifa na tutajitahidi uwenyeji wa mashindano haya uzunguke kwa kila mkoa kwa zamu, ili kuhuisha mchezo huu kote nchini, lakini pia kuwashirikisha wadau wa ndani na nje katika kuwanoa walimu wa riadha nchini, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya mchezo wa riadha vya kisasa, walau kujenga Athletic Academy Center, ambayo itatumiwa na timu ya taifa kujiandaa katika mashindano mbalimbali na kwa baadaye kuangalia nafasi ya chama cha riadha kuwa na kitega uchumi chake, ili mbeleni isimame kwa miguu yake.
Swali: Hivi unajisikiaje wewe ukiwa kijana hivyo, halafu katika kipindi kisichozidi wiki mbili umeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya na kisha ukachaguliwa kuwa Rais wa Chama Riadha?
Jibu: Kama mwanadamu mwingine yeyote mwenye akili timamu, namshukuru sana Mungu wangu, hakika amenitendea makuu katika siku za ujana wangu, namuomba Mungu anisimamie, daima aniongoze katika dhamana hizi nilizonazo, maana katika yeye yote yanawezekana.
Swali: Kitu gani kilikusukuma hadi ukaamua kugombea nafasi hiyo ya urais wa RT?
Jibu: Siku zote nimekuwa nikikwazwa na matokeo mabovu ya riadha nchini, sikupenda kuwa sehemu ya kulaumu, nikaamua mimi mwenyewe kwa hiyari yangu kujitosa ili kuona namna ya kuuokoa mchezo huu; mimi naamini vijana wa Kitanzania bado tunao uwezo wa kurudisha hadhi ya michezo katika nchi yetu, kikubwa tujiondoe katika makundi ya kulalamika na sasa tuwe na uthubutu wa kuomba ridhaa ya kutumikia na tukiaminiwa, basi kweli watu wayaone matunda na si ubabaishaji.
Swali: Matarajia yako ya siku za usoni ni yapi?
Jibu: Matarajio yangu ya siku za usoni ni kuiona Tanzania siku moja inairudia historia iliyowahi kuandikwa na wanariadha mashuhuri kina Meja mstaafu, Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Kanali mstaafu Juma Ikangaa, Nzael Kyomo, Mwinga Mwanjala, Simon Mrashani wa Jeshi la Polisi na wengineo wengi.
Pia Watanzania wakirejea kutoka kwenye mashindano ya Olimpiki na mengineyo mbalimbali wawe na medali za dhahabu na fedha, ndoto hii yaweza chelewa, lakini kama Mungu atanipa uhai mimi na wenzangu katika uongozi huu, chini ya uenyekiti wa Dioniz Malinzi kama Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), mwenye maono ya mafanikio, hakika Watanzania miaka ijayo watarajie medali, mwanzo ni mgumu, lakini naamini tutaweza.
Swali: Unawaeleza nini vijana wenzako?
Jibu: Vijana tuache kulaumu na kulalamika, nchi hii inazo fursa nyingi, naomba wajitokeze kuzitumia.
Swali: Nieleze ni jambo gani ambalo hutalisahau katika maisha yako na je ni kwa nini?
Jibu: Nimepatwa na matukio mengi ya furaha yaliyonigusa katika maisha yangu, hakika sitasahau siku nilipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na siku niliposhinda kiti cha urais wa Riadha Tanzania, sikuamini kama Mtanzania wa kawaida wa aina yangu yangewezekana haya.
Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa upana wake?
Jibu: Mimi ni mtoto wa kwanza kati ya wanne wa mwalimu Meryciana Magati na Mzee John Mtaka Chiganga. Ndugu zangu wengine ni Masegenya, Msafiri na Mgengere.
Nimesoma elimu yangu ya Msingi, Suguti iliyopo Wilaya Musoma Vijijini Mkoa wa Mara, ambapo baadaye nilihitimu shahada ya kwanza ya Utawala, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2009.
Nimeshiriki michezo katika ngazi ya shule ya msingi na sekondari, nikiwa mshiriki katika riadha mbio za kupokezana vijiti ‘relay’, mbio fupi mita 100, kurusha kisahani, kurusha tufe, kulenga shabaha na kidogo nimecheza basketball nikiwa sekondari ya Mwembeni Musoma.
Kama mwanafunzi, michezo hii yote sikuicheza katika mafanikio makubwa ya kujulikana kitaifa, lakini imenijenga kuwa mwanamichezo na mpenzi wa michezo hata kunichochea kuomba ridhaa ya kuongoza chama cha riadha Tanzania, nikiamini ninao uwezo wa kuurudisha mchezo wa riadha katika ramani ya nchi yetu, kwani naamini ni mchezo wenye mashabiki kila kona au pembe ya nchi yetu ndani na nje.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu:
0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Mei 28 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment