WAKILI STANSLAUS BONIFACE KUZIKWA LEO DAR
Na Happiness Katabazi
MWILI wa aiyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface Makulilo (44),leo unatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kinondini jijini Dar es Salaam.
Mdogo wa marehemu ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Alexander Makulilo aliwaeleza waandishi wa habari jana jioni nyumbani kwake eno la Chuo KIkuu ambapo msiba ndipo unapofanyika kuwa bado wanasubiri ripoti ya madaktari ili waweze kufahamu chanzo cha kifo cha marehemu na kuongeza mwili wa marehemu ambao umeifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ,utazikwa katika makaburi hayo.
“Sisi kama familia tumeupokea msiba wa ndugu yetu kwa mshituko mkubwa ila kazi ya mungu haina makosa ,tunachoomba mungu atupe subira na uvumilivu katika kipindi cha msiba huu na kwamba tayari wazazi wa marehemu wameishawasili Dar es salaam,wakitokea mkoani Kigoma kwaajili ya kuja kuudhulia mazishi ya mtoto wao”alisema Dk.Makulilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Sheria kwa vitendo(Law School), Dk.Geradi Ndika ambaye naye alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwepo kwenye msiba huo alisema yeye alisoma na marehemu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwamba marehemu alikuwa ni mhadilifu,mchapakazi na aliyetanguliza haki,usawa na masilahi ya taifa mbele na kwamba kifo hicho ni pigo si kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka bali taifa kwa ujumla.
Boniface alifariki dunia alfajiri ya kuamkia siku ya jumapili katika Hospitali ya Regence muda mfupi baada ya kufikishwa hapo usiku huo. Juzi Mkurugenzi wa Mashitaka Dk.Elizer Feleshi aliliambia gazeti hili kuwa marehemu aliingia Dar es Salaa,jumamosi mchana akitokea mjini Moshi kwaajili ya kutoa mafunzo ya uendeshaji wa mashitaka kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji akiwa mzima wa afya lakini ghafla usiku wa manane alianza kujisikia vibaya na kukimbikizwa katika Hospitali ya Regency anbapo alifariki dunia.
Miongoni mwa kesi kubwa ambazo mwandishi wa habari hizi amekuwa akimshuhudia akiziendesha kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama mbalimbali hapa nchini sasa ni kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika EPA, iliyokuwa ikimkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 23 mwaka jana, iliwahukumu kwenda jela miaka mitano, kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC, Jerry Murro na wenzake ambapo Murro alishinda kesi hiyo mwaka jana, kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabishara Jayankumar Patel “Jeetu Patel’ na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP na Reginal Mengi iliyokuwa akitaka afutiwe kesi zake nne za EPA zilizopo katika mahakama ya Kisutu kwasababu Mengi alimuhukumu kabla ya hajahukumiwa na mahakama kwa sababu alimuita ni Fisadi Papa, ambapo Boniface alimwakilisha AG na DPP na aliibuka mshindi katika kesi hiyo.
Kesi nyingine kubwa ambayo marehemu alikuwa akiziendesha ambazo bado hadi umauti unamkuta hazijatolewa hukumu ni ile ya mauji ya Ubungo Mataa ambayo inaendelewa kusikilizwa na Jaji Projestus Rugazia, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomwona mfanyabiashara Naeem Gile ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Laurence Kaduri ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LCC, kuwa hana kesi ya kujibu, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Kisutu iliyomuona Jerry Murro hana hatia na kesi ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili waliokuwa mawaziri wa Fedha na Nishati, Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja.
Boniface alizaliwa Februali 21 mwaka 1968 ameacha mke na watoto watatu, aliitimu shahaha ya kwanza ya Sheria mwaka 1995 na shahada ya pili ya sheria alimaliza mwaka 2008 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Julai Mosi mwaka 1995 aliajiriwa rasmi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kama Wakili wa Serikali, ilipofika Oktoba Mosi mwaka 2006 alipandishwa cheo na kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi.Oktoba Mosi mwaka 2007 alipandishwa cheo tena na kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali.
Nyadhifa ambazo Boniface aliwahi kuzishika enzi za uhai wake ni kati ya mwaka 2003-2007 alikuwa ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mbeya.Kati ya Mei 2007 na Oktoba 2010 alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Mwanza.Novemba 2009 hadi Novemba 2010 alikuwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali mkoani Dar es Salaam. Kutokana na utendaji kazi wake mzuri ilipofika Desemba 2010 hadi mauti yanamkuta aliteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia awaka Msimamizi wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake liimidiwe.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 29 mwaka 2012
No comments:
Post a Comment