Header Ads

MDOGO WA ROSTAM AZIZ AACHIRIWA HURU

Na Happiness Katabazi HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Tanga imemwachiria huru mdogo wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga(CCM), Rostam Aziz,Assad Aziz Abdulrasul aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kula njama na kuingiza dawa za kulevya zenye uzito wa Kg. 92. 2 ambazo zina thamani ya Sh 2,397,274,000 baada ya kumuona hana kesi ya kujibu. Washtakiwa katika kesi hiyo Na.19B ya mwaka 2011 inayomkabili Abdulrasul ambaye ni yeye peke yake alikuwa akikabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kusafirisha kiasi hicho cha dawa za kulevya aina ya Heroine na alikua akitetewa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza , washtakiwa wengine ni Kileo Bakari Kileo, Yahaya Zumo Makame, Mohammadal Gholamghader Pourdad,Said Ibrahim Hamis,Bakari kileo na upande wa Jamhuri unawakiliwa na Wakili wa Mwandamizi wa Serikali,Biswalo Mganga. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Kipenka Mussa ambaye alisema kesi hiyo ilikuja kwaajili ya yeye kutolea uamuzi wa ama washtakiwa wana kesi ya kujibu ambapo alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na vielelezo ushahidi ulitolewa na mashahidi 200 na vielelezo 25 vya upande wa Jamhuri, mahakama hiyo imeona ushahidi na vielelezo hivyo havithibitishi mshtakiwa wa saba(Abdulrasul) alitenda makosa hayo mawili aliyoshitakiwa nayo. Uamuzi huo ambao gazeti hili inayo nakala yake, Jaji Kipenka alisema ushahidi na vielelezo vyote vimeshindwa kuthibitsiha kesi dhidi ya mshtakiwa huyo wa saba kuwa alitenda makosa hayo ila ushahidi huo umeweza kuishawishi Mahakama iwaone washtakiwa waliosalia kuwa wana kesi ya kujibu. ‘Kwa sababu hiyo mahakama hii inamuachilia huru mshtakiwa wa saba(Abdulrasul) kwasababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yake na kwa maana hiyo mahakama hii inamuachiria huru ila kwa washtakiwa wengine waliobakia mahakama hii imewaona wana kesi ya kujibu hivyo watatakiwa wapande kizimbani wajitetee katika tarehe itakayopangwa na mahakama hii”alisema Jaji Kipenka. Mapema 2011 ilidaiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mganga mahakamani hapo kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kula njama kusafirisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 pamoja na kifungu cha 22(a) and 25 cha Sheria ya Dawa za Kulevya. Kuwa washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Aprili Mosi mwaka na Machi 8 mwaka 2009 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, Tanga na Jamhuri ya Iran ,washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kusafirisha dawa hizo kinyume na kosa la pili ni ni la kukutwa na dawa hizo Machi 8 mwaka 2010 huko kijiji cha Kabuku Wilayani handeni mkoani Tanga,kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 16(1)(b)(1) cha Sheria ya Dawa za Kulevya. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Mei 7 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.