Header Ads

HAKIMU KESI YA LIYUMBA MGONJWA

Na Happiness Katabazi MASHAHIDI wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba jana walishindwa kuendelea kutoa ushahidi wao kwasababu Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Stewart Sanga anayesikiliza kesi huyo anaumwa. Wakili Mwandamizi wa Serikali Elezabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka aliikimbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya shahidi wa nne wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake na kwamba wao walikuwa tayari kwaajili ya kuendelea. Lakini Hakimu Kisoka alisema mashahidi hao hawataweza kutoa ushahidi wao kwasababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo Sanga anaumwa hivyo akaiarisha kesi hiyo hadi Juni Mosi itakapokuja kwaajili ya kutajwa na Julai 2 itakuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa. Liyumba anayetetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu na wakili Kaganda walikubaliana na amri hiyo ya mahakama. Septemba mwaka jana ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Julai 27, 2011, Liyumba alikuwa ni mfungwa mwenye namba 303/2010 katika gereza la Ukonga baada ya mahakama hiyo mwaka 2010 kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma. Wakili huyo wa serikali aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo akiwa gerezani humo alikutwa na simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 yenye rangi nyeusi ambayo ilikuwa na line yenye namba 0653 0004662 na IMEI namba 356273/04/276170/3.Hata hivyo alikana shtaka na hivi sasa yupo nje kwa dhamana. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 11 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.