Header Ads

SHAHIDI AKWAMISHA KESI YA MATTAKA

Na Happiness Katabazi MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa upande wa jamhuri kwa sababu shahidi mmoja wa upande kudai kuwa jana hakuwa tayari kutoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara Kampuni ya Air Tanzania Limited ya Dola za Kimarekani 143,442.75 inayomkabili Mkurugenzi Mstaafu wa kampuni hiyo David Mattaka na wenzake. Wakili Mwandamizi wa serikali Oswald Tibabyekomya mbele ya Hakimu Mkazi Ritta Tarimo alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake lakini shahidi waliyokuja nae jana ambaye jina hakumtaja amewaeleza kuwa hayupo tayari kutoa ushahidi kwa siku ya jana hivyo akaiomba kesi hiyo iarishwe. Ombi hilo lilikubaliwa na mawakili wa utetezi Alex Mgongolwa na Peter Swai ambao walisema hawana pingamizi nalo. Kwa upande wake Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo ambapo aliailisha kesi hiyo hadi Juni 11 itakapokuja kwaajili ya kutajwa na Juni , 14,15 na 16 kesi hiyo itakuja kwaajili ya kauanza kusikilizwa mfululizo. Mbali na Mattaka,washitakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji anayetetewa na wakili Alex Mgongolwa. Novemba 22 mwaka 2011,washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa sita ,ambayo ni kula njama kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka na walitenda kosa hilo kati ya Machi na Julai 2007 kisha waliagiza magari hayo ya mitumba bila kutangaza tenda ya ushindani,bila kusainiwa mkataba wa manunuzi na Mwanasheria mkuu wa Serikali na bila serikali kuwepo kwa bajeti ya serikali. Magari hayo 26 waliyanunua kwa thamani ya dola za kimarekani 809,000 kutoka kampuni ya 3 IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai katika Jamhuri ya Emireti,na bila ya kuwepo ya kumbukumbu ya manunuzi hayo kinyume na kifungu cha 59 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake. Itakumbukwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania Desemba 21 mwaka 2005 muda mchache baadaye alimteua Mattaka kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la ATCL na kisha baadaye kumteua Mattaka kuwa Mjumbe wa Tume ya Rais ya Kikosi Kazi cha Kurekebisha Shirika la Bima la Taifa. Wakati Rais Kikwete akimteua Mattaka kushika nyadhifa hizo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, wananchi mbalimbali walilaani uteuzi huo bila mafanikio. Na kabla ya Rais Kikwete kumteua Mattaka kushika nyadhifa hizo,Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikuwa amemstaafisha Mattaka kwa manufaa ya umma.Na wakati Mkapa anamstaafisha mshtakiwa huyo kwa manufa ya umma alikuwa akishikilia cheo cha Ukurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pesheni wa Mashirika ya Umma(PPF). chanzo:Gazeti la Tanzana Daima la Jumamosi, Mei 12 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.