Header Ads

NAMLILIA WAKILI STANSLAUS BONIFACE 'JEMBE'

Na Happiness Katabazi ILIKUWA ni siku ya Jumapili saa 1:57,asubuhi ya Mei 27 mwaka huu, nikiwa kitandani nilipigiwa simu na aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa la TBC1, Jerry Murro, nilishtuka kwasababu sina mazoe ya mara kwa mara ya kuwasiliana naye. Murro alianza kwa kunisalimu na kuniuliza moja kwa moja kuwa anajambo anataka kulithibitisha kutoka kwangu kwasababu anaamini mimi nitakuwa na majibu ya hilo analotaka kuniliuza nikamruhusu aniulize. Murro akaanza kwa kusema amepata taarifa mbaya licha hana uhakika nazo kuwa Wakili wa Serikali aliyekuwa akiendesha kesi iliyokuwa ikimkabili ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo ilimalizika mwaka jana ambapo Hakimu Mkazi Frank Moshi alimuona Murro hana hatia, Stanslaus Boniface amefariki dunia. Taarifa hizo zilinishtua na kunifanya nikurupuke kitandani na kukimbilia nje ya nyumba yetu huku nikiwa na simu yangu ya kiganjani , ili kuthibitisha taarifa hizo mtu wa kwanza kumpigia alikuwa ni rafiki yangu ambaye ni Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi katika simu zake ambazo hata hivyo hazikuwa zikipatikana. Nikapata akili nyingine nikaamua kumpigia Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Mganga na kumuuliza,huyo ndiye aliyenithibitishia taarifa hizo na nikajikuta naanza kulia kwa sauti, nilipotulia nikamtumia ujumbe mfupi Murro wa kumjulisha kuwa ni kweli Stanslaus Boniface Makulilo (44) amefariki ghafla dunia usiku wa kuamkia siku ya Jumapili katika Hospitali ya Regency. Ilipofika saa tatu asubuhi nilianza kupokea na kusambaza ujumbe mfupi kwa baadhi ya mawakili wa serikali ,wakujitegemea na waandishi wa habari wenzangu kuhusu kifo hicho. Nikiwa kama Mwandishi wa Habari za Mahakamani kwa takribani miaka 13 sasa hapa nchini, nilianza kumfahamu kikazi na rasmi Boniface,Novemba 4 mwaka 2008. Nilimfahamia pale katika Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.Na tarehe hiyo itabaki kuwa ni tarehe ya historia hapa nchini hususani serikali ya awamu ya nne chini ya Utawala wa Rais Jakaya Kikwete kwasababu Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Dk.Feleshi ndiyo alifungua kesi nne kwa mpigo zinazohusu wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na hivyo kufanya washtakiwa wengi akiwemo Kada wa CCM, Rajabu Maranda, mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Patel ‘Jeetu Patel” kupanda kizimbani na kwenda gerezani kwa siku kadhaa baada ya kukosa dhamana. Tangu hapa hadi Ijumaa ya wiki iliyopita nimekuwa karibu na Boniface katika masuala ya kikazi nikisema mahusiano ya kikazi namaanisha yeye na baadhi ya mawakili wa serikali, kujitegemea tumekuwa tukishirikiana kitaaluma, kwani wao wanaendesha kesi na kufungua kesi hivyo wanatutegemea sisi waandishi wa habari za mahakamani turipoti kesi hizo na sisi waandishi tumekuwa tukipata msaada wa jinsi ya kuripoti kesi hizo ilitusizipotoshe. Hakuna ubishi kwamba Boniface alikuwa ni miongoni mwa mawakili wachache wa serikali wazalendo kwa taifa lao, wachapakazi na mahiri katika uendeshaji wa kesi hasa kesi za jinai. Mawakili wengi wa kujitegemea ambao wamekuwa wakiwatetea wateja wao pindi walipokuwa wakisikia Boniface amepangwa kuuwakilisha upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, walikuwa wakitikisika na kujipanga sawa sawa. Kwa sisi ambao kila kukicha tunaoshinda mahakamani kuudhulia kesi mbalimbali mara kadhaa tumekuwa tukiwasikia mawakili wa kujitegemea pindi Boniface akipita mbele yao kwenda kuudhulia kesi nyingine , wamekuwa wakionyeshana vidole kuwa ‘Boniface ni jembe ambalo linategemewa sana na ofisi ya DPP katika kesi za’, bila yeye kufahamu na sifa hizo nilikuwa nikimpelekea. Na baadhi ya washitakiwa walikuwa wakitueleza kuwa wakili Boniface ni mwiba mkali kwao kwani hata kuongeka haongeki. Namlilia Boniface kwasababu sitamuona tena mahakamani akiendesha kesi mahakamani.Namlilia Boniface kwani nitazikosa mbwembwe zake wakati akiendesha kesi. Namlilia Boniface kwasababu sisi waandishi wa habari za mahakamani ambao tunavutiwa sana na uendeshaji kesi wake mahakamani pindi azungumzapo kutetea upande wa jamhuri kabla ya kuanza kuwasilisha hoja zake amekuwa akipenda sana kutumia neno hili “Ikupendeze ndugu Mweshimiwa’, alikuwa akimaanisha Jaji au Hakimu husika ikiwa ni ishara yake ya kuanza kujitambulisha mbele ya majaji au mahakimu wanaosikiliza kesi anayoiendesha. Neno ambalo sisi waandishi wa habari za mahakamani ilifika mahakama tukaacha kuwa tunamuita jina lake la Boniface, tukawa tukimuona tunamuita ‘Ikupendeze ndugu mweshimiwa’ na alikuwa akicheka sana. Namlilia Boniface kwasababu tutazikosa mbwembwe zake wakati akiendesha kesi ambazo mapema alikuwa akitudokeza kuwa katika kesi fulani upande wa Jamhuri una ushahidi wa kutosha ambao unaweza kuwatia hatiani washitakiwa basi katika kesi za iana hiyo Boniface alikuwa akionyesha manjonjo wakati akiwauliza maswali ya kuwabana washtakiwa kwa mara kwa mara ‘alikuwa akiweka koti la suti yake, tai vizuri’.Hizo ni mbwembwe ambazo ufanywa na mawakili wengi mahakamani pindi waaminipo upepo mzuri utavuma katika upande wao wanaouwakilisha katika kesi yake. Na wakati akifanya manjonjo hayo sisi waandishi wa habari za mahakamani ambao uwa tunaketi nyuma ya kiti cha mawakili uwa tunafinyana na tunacheka kimya kimya na kuandikiana vikaratasi kuvutiwa na aina ya uendeshaji wake wa kesi wa ‘ikupendeze mweshimiwa’. Boniface alikuwa ni miongoni mwa waendesha mashitaka wachache mno ambao walikuwa wakiwauliza maswali washitakiwa bila kuyaandaa maswali kwenye karatasi au kusoma kwanza maswali kwenye karatasi kisha ndiyo aliulize maswali. Ndiyo maana Boniface tulimpatia jina la Jembe kutokana na umahiri wake wa kikazi kwani halikuwa akiuliza maswali washitakiwa bila kusoma mahala popote, alikuwa akiwasilisha baadhj ya maombi kwaniaba ya upande wa Jamhuri kwa mahakama bila kusoma vifungu vya sheria mara kwa mara.Na hata baadhi ya mahakimu na majaji ambao nimekuwa na mahusiano nao wamekuwa wakiniuma sikio kuwa wanajisikia rah asana wanaposikiliza kesi ambayo Boniface amepangwa kuuwakilisha upande wa Jamhuri kwasababu Boniface ni wakili mzuri na anayefahamu kazi yake vyema bila kubahatisha. Umaarufu wa jina la Boniface ulianza kukua taratibu wakati akiendesha kesi za uchunaji ngozi mkoani Mbeya miaka ya 2000, kesi za EPA, kesi ya matumuzi mabaya na kuisababishia serikali hasara na mauji. Miongoni mwa kesi kubwa ambazo binafsi nilimshuhudi Boniface akiziendesha katika mahakamani mbalimbali kwa miaka mitano sasa ni kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika EPA , iliyokuwa ikimkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 23 mwaka jana, iliwahukumu kwenda jela miaka mitano. Kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC, Jerry Murro na wenzake ambapo Murro alishinda kesi hiyo mwaka jana, kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabishara Jayankumar Patel “Jeetu Patel’ na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP na Reginal Mengi iliyokuwa akitaka afutiwe kesi zake nne za EPA zilizopo katika mahakama ya Kisutu kwasababu Mengi alimuhukumu kabla ya hajahukumiwa na mahakama kwa sababu alimuita ni Fisadi Papa, ambapo Boniface alimwakilisha AG na DPP na aliibuka mshindi katika kesi hiyo. Kesi nyingine kubwa ambayo marehemu alikuwa akiziendesha ambazo bado hadi umauti unamkuta hazijatolewa hukumu ni ile ya mauji ya Ubungo Mataa ambayo inaendelewa kusikilizwa na Jaji Projestus Rugazia, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomwona mfanyabiashara Naeem Gile ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Laurence Kaduri ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LCC, kuwa hana kesi ya kujibu, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Kisutu iliyomuona Jerry Murro hana hatia na kesi ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili waliokuwa mawaziri wa Fedha na Nishati, Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja na kesi nyingine zaidi. Ukiachilia mbali hilo, Namlilia Boniface kwasababu mimi binafsi amekuwa msaada mkubwa kwangu katika shule yangu ya sheria ninayosoma kwa kunifundisha baadhi ya masomo ya sheria na pia alikuwa akinipatia msaada wa sheria na kesi mbalimbali ili ziweze kunisaidia katika shule yangu. Boniface mara kwa mara alikuwa akiniimiza nikazane na masomo kwani anaamini mwandishi wa habari za mahakamani akisoma na sheria,basi mwandishi huyo atakuja kuwa mwandishi mzuri zaidi baadaye kwani ataweza kuwa anaripoti bila kupotosha mwenendo wa kesi mbalimbali na jamii itanukafaika na mchango wa mwandishi huyo kwani hadi sasa hakuna mwandishi wa habari za mahakama aliyesoma sheria akaendelea kuripoti habari za mahakama.Wana habari waliosoma sheria pindi wamalizapo kusoma sheria wanakimbia fani ya uhandishi wa habari. Na mimi nilizingatia ushauri wake huo na kila nilipokuwa nikimaliza mitihani na kupata matokeo nilikuwa nikimuonyesha matokeo yangu.Namlilia Boniface kwani hatutamuona tena katika mahakama zetu hapa nchini hususani pale Mahakama ya Kisutu, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na mahakama nyingine. Natamani Boniface ufumbue macho uone mawakili wenzako wa serikali Dk.Feleshi, Winfrida Koroso, Fredrick Manyanda, Timon Vitalis, Araf Msafiri, Ben Lincoln, Prosper Mwangamila,Ephery Sedekia, Biswalo Mganga,Malangwe Mchungahela,Shadrack Kimaro,Ponsian Lukosi, Justus Mulokozi na wengine wengi. Waandishi wa habari za mahakamani, Happiness Katabazi, Regina Kumba(Habari Leo),Magai James na Tausi Ally(Mwananchi), Hellen Mwango(Nipashe) Rose Japhet(TBC1), Kulwa Mzee(Mtanzania) na wengine tunakulilia Boniface. Jamii ya wasomi wa sheria nchini na wananchi wa kada mbalimbali wanavyokulilia,lakini ndiyo haiwezekani. Namlilia Boniface ambaye hayupo tena nasi duniani, ila mazuri aliyotuachia tutayafuata na kuyatekeleza kwa vitendo.Hata hivyo Boniface kama walivyo binadamu wengine alikuwa na upungufu na udhaifu na mabaya yake, hatutayafuata. Boniface pia alikuwa ni mcheshi na mtu mwenye kupenda utani pia, kwani Mei 9 mwaka huu, akiwa mkoani Arusha alinipigia simu akiniuliza ni ushahidi wa aina gani ulitolewa Mei 8 mwaka huu, na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwenye kesi ya wizi wa zaidi ya Euro milioni moja ambayo inamkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin, nilimthibitishia kuwa ni kweli Mkapa alifika mahakamani na kutoa ushahidi wake. Boniface hatua hiyo ya Mkapa imeandika historia mpya katika tasnia ya sheria nchini na nikamuuliza ingetokea yeye ndiyo mwendesha mashitaka katika kesi hiyo angekuwa na maswali yapi ya kumhoji Mkapa. Nakumbuka Boniface alicheka sana na akasema yeye angemuuliza rais huyo mstaafu maswali yafuatayo. “Ndugu shahidi yaani(Mkapa) ni kwanini una upara na ni kwanini umenenepa sana”. Nilicheka sana na yeye Boniface alicheka sana kwenye hiyo simu na ninakumbuka siku hiyo alikuwa akitumia simu ya wakili wa serikali Malwangwe Mchungahela kuwasiliana na mimi.Tulicheka sana kupitia simu kama dakika mbili nzima na nikamuuliza Boniface aoni swali hilo haliusiani na kesi akanijibu hivi ‘Rais wa nchi siyo mtu wa mchezo’, na akamalizia kwa kusema yeye alikuwa ananiambia kwa utani na kuhusu ushahidi wa Mkapa tuiachie mahakama.Hadi sasa naandika makala hii licha nina majonzi lakini nikikumbuka maneno hayo ya Boniface nacheka peke yangu. Wakili wa siku nyingi wa serikali Boniface amefikwa na mauti. Alifikwa na mauti katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, muda mfupi baada ya kufikishwa hapo akitokea nyumbani kwake Kinondoni ambapo alizidiwa ghafla lakini kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Elizer Feleshi alisema Boniface wiki iliyopita alikuwa mjini Moshi akitoa mafunzo ya uendeshaji wa mashitaka kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji na aliletea jijiji Dar es salaam, Jumamosi jioni akiwa mzima wa afya lakini usiku wa Jumamosi ghafla hali ya afya yake ilibadilika na kukimbizwa hospitali kwaajilii ya matibabu lakini alifariki dunia. Ama kwa hakika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayoongozwa na Jaji Fredrick Werema na ile Kurugenzi ya Mashitaka,imepoteza mtu muhimu katika shughuli za ofisi hizo za kila siku.Lakini kwakuwa Boniface hakuwa mchoyo wa taaluma yake aligawa taaluma yake kwa waliochini yake na aliowazidi naamini wale walio bahatika kupata msaada wa kikazi kutoka kwa marehemu huyo watauendeleza kwaajili ya kuleta tija katika taifa letu. Historia ya maisha yake: marehemu ambaye ni Mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma alizaliwa Februali 21 mwaka 1968 ameacha mke na watoto watatu, aliitimu shahaha ya kwanza ya Sheria mwaka 1995 na shahada ya pili ya sheria alimaliza mwaka 2008 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Julai Mosi mwaka 1995 aliajiriwa rasmi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kama Wakili wa Serikali, ilipofika Oktoba Mosi mwaka 2006 alipandishwa cheo na kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi. Oktoba Mosi mwaka 2007 alipandishwa cheo tena na kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali. Nyadhifa ambazo Boniface aliwahi kuzishika enzi za uhai wake ni kati ya mwaka 2003-2007 alikuwa ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mbeya.Kati ya Mei 2007 na Oktoba 2010 alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Mwanza. Novemba 2009 hadi Novemba 2010 alikuwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali mkoani Dar es Salaam. Kutokana na utendaji kazi wake mzuri ilipofika Desemba 2010 hadi mauti yanamkuta aliteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia awaka Msimamizi wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma. Namlilia Boniface kwani tutamkosa kwenye vijiwe vyetu tulivyokuwa tukikutano baada ya muda wa kazi kuisha na kupata moja baridi,moja moto na nyama choma. Pia utakumbukwa na washirika katika yale mambo yenu yale ya kuvuta sigara. Pia utakumbukwa na mkeo na watoto Boniface sisi tulikupenda, lakini Bwana amekupenda zaidi. Mungu ailaze roho yako mahala pema peponi. Amina. Namlilia Stanslaus Boniface ‘Jembe’. 0716 774494 Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 29 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.