Header Ads

WAKILI MAARUFU AFARIKI DUNIA

Na Happiness Katabazi
MKURUGENZI Msaidizi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface Makulilo (44) ‘Jembe’ amefariki ghafla usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashitaka nchini(DPP), Dk.Eliezer Feleshi alilithibishia Tanzania Daima jana asubuhi kutokea kwa kifo hicho ambapo alisema bado ofisi yake na taifa limepata pigo kubwa lakuondokewa na gwiji hilo la uendeshaji wa mashitaka hususani ya jinai hapa nchini na kwamba mchango wake mzuri katika uendeshaji wa kesi hususani za jinai hautasaulika na utaenziwa. Dk.Feleshi alikuwa akizungumza na gazeti hili kwa uzuni alisema Jumamosi jioni Boniface ambaye pia alikuwa Msimamizi wa Uendeshaji wa Kesi zenye maslahi kwa umma, aliingia Dar es Salaam, akitokea Moshi kwaajili ya kutoa mafunzo ya jinsi ya uendeshaji wa mashitaka kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji akiwa mwenye afya njema na alirejea nyumbani kwake Kinondoni lakini ilipofika usiku wa siku hiyo hali yake ilibadilika ghafla na kukimbizwa katika Hospitali ya Regency kwaajili ya matibabu. “Baada ya kufikishwa hospitalini hapo alifariki dunia ila mimi kama kiongozi wake wa kazi kwa sasa siwezi kusema chanzo cha kifo hicho hadi pale tutakapopata taarifa rasmi za madaktari na msiba upo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mtaa wa Sinza Load Kitalu Na.4 na hadi kufikia leo utaratibu shughuli za msiba zitakuwa zimefahamika na tutawajulisha”alisema Dk.Feleshi. Dk.Feleshi alimuelezea Boniface kuwa ni miongoni mwa mawakili wa serikali waliokuwa wakijitoa kwa moyo wao wote katika kuitumikia serikali yao katika uendeshaji wa kesi bila woga na katika kuthibitisha hilo ni katika kesi za mauji yaliyoibuika miaka ya nyumba mkoani Mbeya ambapo watu walikuwa wakiwachunya binadamu wenzao ngozi, kesi za wizi wa fedha za EPA, matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuongeza kuwa marehemu alikuwa akitumia taaluma yake kwa kuwapatia watu wengine waliokuwa wakiitaji. Miongoni mwa kesi kubwa ambazo mwandishi wa habari hizi amekuwa akimshuhudia akiziendesha kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama mbalimbali hapa nchini sasa ni kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika EPA, iliyokuwa ikimkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 23 mwaka jana, iliwahukumu kwenda jela miaka mitano, kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC, Jerry Murro na wenzake ambapo Murro alishinda kesi hiyo mwaka jana, kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabishara Jayankumar Patel “Jeetu Patel’ na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP na Reginal Mengi iliyokuwa akitaka afutiwe kesi zake nne za EPA zilizopo katika mahakama ya Kisutu kwasababu Mengi alimuhukumu kabla ya hajahukumiwa na mahakama kwa sababu alimuita ni Fisadi Papa, ambapo Boniface alimwakilisha AG na DPP na aliibuka mshindi katika kesi hiyo. Kesi nyingine kubwa ambayo marehemu alikuwa akiziendesha ambazo bado hadi umauti unamkuta hazijatolewa hukumu ni ile ya mauji ya Ubungo Mataa ambayo inaendelewa kusikilizwa na Jaji Projestus Rugazia, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomwona mfanyabiashara Naeem Gile ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Laurence Kaduri ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LCC, kuwa hana kesi ya kujibu, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Kisutu iliyomuona Jerry Murro hana hatia na kesi ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili waliokuwa mawaziri wa Fedha na Nishati, Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja. Boniface alizaliwa Februali 21 mwaka 1968 ameacha mke na watoto watatu, aliitimu shahaha ya kwanza ya Sheria mwaka 1995 na shahada ya pili ya sheria alimaliza mwaka 2008 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Julai Mosi mwaka 1995 aliajiriwa rasmi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kama Wakili wa Serikali, ilipofika Oktoba Mosi mwaka 2006 alipandishwa cheo na kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi.Oktoba Mosi mwaka 2007 alipandishwa cheo tena na kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali. Nyadhifa ambazo Boniface aliwahi kuzishika enzi za uhai wake ni kati ya mwaka 2003-2007 alikuwa ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mbeya.Kati ya Mei 2007 na Oktoba 2010 alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Mwanza.Novemba 2009 hadi Novemba 2010 alikuwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali mkoani Dar es Salaam. Kutokana na utendaji kazi wake mzuri ilipofika Desemba 2010 hadi mauti yanamkuta aliteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia awaka Msimamizi wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake liimidiwe. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Mei 28 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.