Header Ads

DK.MAHANGA ASHINDA KESI

Na Happiness Katabazi HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyakataa madai ya aliyekuwa Mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasi(Chadema), Fred Mpendazoe yaliyokuwa yanaiomba mahakama hiyo ibatilishe matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza mbunge wa jimbo hilo Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa mshindi kwasababu kanuni na taratibu za sheria ya uchaguzi zilikiukwa kwa maelezo kuwa Mpendazoe ameshindwa kuleta mahakama ushahidi mahususi wa kuthibitisha bila kuacha shaka madai yake.
Sambamba na hilo Jaji Profesa Ibrahim Juma alisema katika kesi hiyo kuna jambo zito lilijitokeza ambalo ambalo halikuwepo kwenye hatia ya madai ya Mpendazoe na jambo hilo lililetwa na Mpendazoe na wakili wake Peter Kibatara na Novemba 2 mwaka 2010, gazeti la Mwananchi lilichapisha habari hiyo kuwa Dk.Mahanga alikamatwa na polisi akiwa na masanduku ya kura na kwamba alifishikiliwa katika kituo cha polisi cha Bunguruni na wengine wakadai alishikiliwa katika kituo cha polisi Tabata Novemba Mosi mwaka huo. “Jaji Profesa Juma alisema ieleweke wazi mlalamikaji ameshinda kuthibitisha tuhuma hizi ambazo bila kumung’unya maneno mahakama hii inadiriki kusema tuhuma hizo ni nzito na zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwani kitendo cha kuenea uvuvi huo una maanisha maamisha wa Tume ya Uchaguzi hawakuwa makini na kazi yao hadi mgombea mmoja (Mahanga) akapata upenyo wa kukimbia na masanduku ya kura na cha kushangaza Mpendazoe ameshindwa kuleta mashahidi ambao ama ni wakuu wa vituo hivyo wa polisi kuja kuthibitisha kuwa ni kweli tarehe hiyo Mahanga alikamatwa na masanduku hayo…hivyo mahakama hii inaona tuhuma hiyo hazina ukweli wowote”alisema Jaji Profesa Ibrahim Juma. Profesa Juma ambaye kabla ya kuanza kusoma hukumu yake mbele ya mamia ya wananchi waliokuwa wamefurika ndani ya chumba cha mahakama na nje ya Jengo la Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ambako ndiko hukumu hiyo ilisomwa alianza kwa kutoa angalizo kuwa hukumu yake yenye kurasa 79 ameiandika kwa lugha ya Kiingereza licha ataisoma kwa lugha ya Kiswahili huku Mpendazoe na Dk.Mahanga nao walikuwemo ndani ya chumba hicho kusikiliza hukumu hiyo. Alisema kabla ya mahakama ya kutoa hukumu yake mawakili wa pande mbili yaani wakili wa mlalamikaji, Peter Kibatara na wale wa wadaiwa ambapo Wakili Mwandamizi wa Serikali David Kakwaya anayemwakilisha mdaiwa wa kwanza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mdaiwa wa pili ,Msimamizi wa Tume ya Uchaguzi na wakili Jerome Msemwa ambaye anamwakilisha mdaiwa wa pili ambaye ni Dk.Mahanga walimkabidhi hoja 11 ambazo ndiyo walimwomba jaji huyo atoe hukumu yake kulingana na hoja hizo na kwamba yeye alikubaliana na mawakili hao na kuzifanyiakazi kama ifuatavyo; Jaji huo aliitaja hoja ya kwanza kuwa ni Je utaratibu wa kuhesabu kura wa jimbo la Segerea ulikiuka sheria ya Uchaguzi kwani msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo hakufanya jitihada zozote za kutafuta ufumbuzi wa zilizokuwa zina mgogoro na kwamba ya baadhi ya vituo hayakusainiwa na msimamizi wa uchaguzi ? Akiichambua hoja hiyo Jaji Juma shahidi wa upande wa wadaiwa ambaye Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo matatu ya wilaya ya Ilala, Fuime alidai kuwa malalamiko toka kwa mgombea wa chama cha CUF na Sauti ya Umma kuwa kuna baadhi ya kula wanazilalamikia na kwamba kama kweli malalamiko hayo yangekuwepo yangepaswa kupelekwa na wasimamizi wa uchaguzi wa vituo na siyo kwakwe. “Mahakama hii imeona hoja hiyo ya mgogoro wa kula haikupaswa kupelekwa mahakamani kwani kwa mujibu wa kifungu cha 79 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka mlalamikaji apeleke malalamiko hayo kwa msimamizi wa kituo cha uchaguzi ili ayatolea uamuzi na kama akulidhika na uamuzi huo mlalamikaji atalazimika kupeleka lalamiko hilo kwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo na kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa hakuna ushahidi unaonyesha malalamiko hayo yaliwahi kufikishwa na walalamikaji kwa kufuata taratibu hizo na kwa maana hiyo mahakama hiyo inaitupilia mbali hoja hiyo”alisema Jaji Ibrahim. Alisema hoja ya pili ni kwamba Je zoezi zima uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Serikali ulifuata sheria na ulikuwa huru, uwazi na haki? Akichambua hoja hiyo ya pili Jaji huyo alisema kwa kuwa mlalamikaji ameshindwa kuleta ushahidi mahsusi ambao umeshindwa kuutikisa ushahidi wa upande wa wadaiwa, mahakama yake kwa kauli moja imetupilia mbali hoja hiyo na imeridhika kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikidhi matakwa yote ya sheria na kanuni na kwamba NEC ilikuwa sahihi kumtangaza Dk.Mahanga kuwa ndiye mshindi na alishinda kihalali na kwamba mahakama hiyo inatoa cheti kuthibitisha Mahanga ndiye mbunge halali wa jimbo la Segerea na si vinginevyo na kwamba mahakama hiyo anaamuamuru Mpendazoe awalipe wadaiwa gharama za uendeshaji kesi hiyo. Hoja ya tatu ilikuwa ni je kura za vituo 120 vya Kata Kiwalani na 129 vya Kata ya Kiwalani Mpendazoe alidai hazikujumuishwa katika matokeo ya jumla yaliyompa ushindi Mahanga na kwamba mawakala wake hawakupatiwa na NEC vifaa hivyo kusababisha mawakala wake kuja matokeo ya kura katika fomu zisizo rasmi na kuwa ili kuthibitisha hoja hiyo mlalamikaji katika hati yake ya madai aliambia mahakama kuwa angewasilisha mahakamani mkanda wa video kuthibitisha hoja hiyo. “Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili kuhusu hoja hii ya tatu ambayo mahakama imeona hoja hii ni nzito, mahakama inaitupilia mbali hoja hiyo kwasababu si Mpendazoe wala mashahidi wake waliweza kuleta ushahidi wa kuthibitisha hoja hiyo na kwamba hata wakati Mpendazoe alipotoa ushahidi wake mawakili wa utetezi walimtaka awapata huo mkanda wa video alioahidi angeuleta kama kielelezo, mlalamikaji huyo alishindwa kuuleta mkanda huo na pia hakuleta ushahidi wa kuthibitisha mapungufu hayo na kwamba mashahidi wa tatu wa upande wa wadaiwa walitoa ushahidi wakidai wao walisambaza vifaa vya zaoezi la upigaji kula kwa wakati na kwamba hakukuwepo na mapungufu yanayodaiwa na mlalamikaji; “Edwin Mwakatobe mwanachama wa Chadema ambaye ndiye aliyekuwa wakala wa Mpendazoe ngazi ya Jimbo ambaye ni shahidi wa 13 ndiye alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kuthibitisha madai kuwakulikuwa na mapungufu katika vituo hivyo lakini katika ushahidi wake aliutoa mahakamani Mwakatobe alieleza kuwa yeye hakuwahi kupokea malalamiko hayo toka kwa mawala wa chadema ngazi ya vituo kuwa kulikuwa na matatizo katika fomu namba 21B ya matokeo ya uchaguzi na kwamba NEC haikuwapatia vifaa na matokeo yake wakaamua kuja matokeo ya Mpendazoe katika fomu zisizo rasmi”alisema Jaji huyo. Jaji huyo alisema Kanuni ya 60 ya Sheria ya Uchaguzi msimamizi wa uchaguzi baada ya kuhesabu kula za mgombea urais na ubunge ataandika kumbukumbu yaa taarifa za matokeo hayo katika fomu rasmi Na. 21A kwaajili ya kura za urais na Na.21B kwa mgombea ubunge na kuwa sheria za nchi zinautaratibu wake wa kuandika matokeo katika fomu maalum na msimamizi wa uchaguzi wa kituo na siyo wakala kuamua kujaza matokeo yake katika fomu isiyorasmi kama ilivyofanywa na baadhi ya mawakala wa Chadema kwa kisingizio kuwa NEC haikuwapatia fomu hizo ndiyo maana wakaamua kujaza baadhi ya matokeo ya vituo katika fomu zisizo rasmi ambazo hhazitambuliki na kanuni hiyo ya 60 ya Sheria ya Sheria ya Uchaguzi na kwasababu hiyo hoja hiyo ya tatu pia Mpendazoe ameshindwa kuithibitisha na hivyo anaitupilia mbali. Akiizungumzia hoja ya nne ambayo msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Segerea alimtangaza kwa lazima Mahanga kuwa mshindi Novemba 3 mwaka 2010 bila kujumlisha kura za vituo 120 ya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ya Kata Vingunguti licha aliombwa afanye hivyo na Mpendazoe . Alisema katika ushahidi wake Mpendazoe kuhusu hoja hiyo alidai kuwa matokeo ya Kata hizo mengine hayakuhesabiwa na mengine hayakujazwa katika fomu rasmi na mawakala wake.Alisema kuhusu madai ya fomu za kujaza matokeo hazikuwafikia mawakala wake, mashahidi wa Mpendazoe katika maelezo yao walitofautiana wakati wakitoa ushahidi wao. “Kutokana ushahidi wa mashahidi wa Mpendazoe kuhusu hoja hiyo mahakama hiyo imeona kuna matokeo ya ngazi ya Kata ya Kiwalani na Vingunguti fomu zilipotea.Pia inaonekana matokeo hayo hayakutangazwa kwa ngazi ya Jimbo la Segerea.Aina pili mahakama imeona majumuisho ya kura ngazi ya Kata ni kwaajili ya kukusanywa tu na ngazi ya jimbo ni kwaajili ya kujumuishwa na kisha kutangazwa. “Kisheria mahakama hii imejiuliza ni wakati gani majumuisho ya kula ufanyika katika ngazi gani na wakati gani?Kifungu cha 81 cha Sheria ya Uchaguzi ndiyo kinampa mamlaka msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mshindi.Na kifungu cha 79(a), 80 na 81 vya sheria hiyo vinatamka bayana kuwa matokeo ya uchaguzi yatajazwa katika fomu Na.21 B na kwamba matokeo hayo yatapia hatua nne; “Mosi, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika kupokea matokeo toka katika vituo atavihakiki na msimamizi wa uchaguzi ndiye atakayehakiki matokeo na aidha yeye mwenyewe au msaidizi.Pili, ni pale msimamizi wa uchaguzi anatoa uhalali kama kuna mogogoro ya kura halali.Tatu, msimamizi atakapotangaza matokeo ya uchaguzi kwa sauti.Nne, Msimamizi huyo atajaza atajaza fomu hiyo ili aweze kumtangaza mshindi kwa sauti. Na utaratibu huu unatumika kwa ngazi ya Jimbo. Jaji Ibrahim alisema mahakama ilijiuliza mambo hayo manne kabla ya kutolea uamuzi hoja hiyo ya nne kuwa je hatua hizo nne zilifanyika ngazi ya jimbo ikiwa mlalamikaji anaomba ubunge wa Mahanga utengeliwe? Je huyo Mwakatobe wakala mlalamikaji alikuwepo wakati hatua hizo nne zinafikiwa? Ni kwanini mlalamikaji hakuleta ushahidi unaonyesha hatua hizo hafikufuatwa na msimamizi wa uchaguzi?Je ni kweli msimamizi wa uchaguzi hakutangaza kwa sauti matokeo ya kura na mshindi? Aidha jaji huyo ambaye alitumia muda kuichambua hoja hiyo akidai ni hoja nzito, alisema Msimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Segerea,Ilala na Ukonga, Fuime katika ushahidi wake aliweza kuleta ushahidi wa kuthibitisha hatua hizo zilifuatwa na kwamba majumuisho ya kura yalifanyika kwa ngazi ya Jimbo na kutangazwa katika Ukumbi wa Arnautoglu na kwamba kabla ya kutangaza matokeo hayo aliwaalika wagombea na wafuasi wa vyama vyote lakini ikiwamo CCM,CUF na Chadema lakini Chadema walikataa kuudhuria na Mpendazoe akiwa na wafuasi wake sita walimkataza Fuime asimamishe utangazaji wa matokeo hayo ya ubunge lakini kanuni za sheria ya uchaguzi inamruhusu msimamizi kuendelea kujumlisha kura na kutangaza matokeo. Alisema kwasababu mawakala na mgombea wa Chadema waligoma kuuingia kwenye chumba cha kuhesabia kura ni wazi kabisa si Mpendazoe wala huyo wakala wake Mwakatobe wanaweza kuleta ushahidi ambao ungethibitisha kura za vituo vyote hazikujumuishwa kwasababu walikiri hapa mahakamani kuwa hawakuwepo kwenye chumba cha kujumulishia kura za ubunge. Kuhusu hoja ya tano ambayo Mpendazoe alidai kuwa Imelda Kafanabo ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Kata ya Tabata kuwa alikamatwa na polisi pale Arnaotoglu akiwa matokeo yaliyogushiwa, jaji huyo alisema Mpendazoe ameshindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha Kafanabo alikamatwa na matokeo na maamuzi mbalimbali ya mahakama ya rufaa yameeleza kuwa jukumu la kuthibitisha madai ni la mlalamikaji na katika dai hili mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha kuwa ni kweli Kafanabo alikamatwa na matokeo ya kura feki. Kuhusu hoja ya sita ambayo mlalamikaji alidai kuna kijana mmoja alikamatwa Arnaotoglu akiwa na mhuri wa NEC,jaji huyo alisema hoja hiyo ni dhahifu pia kwasababu mlalamikaji ameshindwa kuleta ushahidi kama kweli mshtakiwa huyo alikamatwa na jeshi la polisi akiwa na mhuri huo na pia ameshindwa kuthibitisha hata kama kweli kijana huyo alikamatawa na mhuri huo uliathiri vipi matokeo ya jimbo la segerea na kwamba pale Arnaoutoglu ndiyo kilikuwa Kituo Kikuu cha kuhesabia na kutangaza matokeo ya majimbo matatu ya Ilala,Ukonga na Segerea yaliyopo ndani ya Wilaya ya Ilala, na kuongeza kuwa huyo kijana aliyekamatwa na mhuri huyo alikuwa akienda kuutumia kufanya hujuma katika matokeo ya jimbo la segerea. Akiipangua hoja ya saba ambayo mlalamikaji alidai masanduku yaliyokuwa yamebeba kura hayakuwa Rakimu yaani yalikuwa hayajafunikwa, Jaji huyo alisema kulingana na ushahidi uliotolewa amelidhika na upande wa wadaiwa kuwa kuwa hata kama masanduku hayo kweli yangekuwa wazi yasingeweza kuathiri kura zilizokuwa ndani ya masanduku hayo na kuongeza kuwa pia mlalamikaji ameshindwa kuleta ushahidi unaonyesha hayo masanduku yaliyokuwa wazi yalikuwa yakitokea Kata zipi na namba za masanduku hayo. Kuhusu hoja ya nane,ambayo mlalamikaji alidai mawakala wake, mawakala wa CUF na SAU waligoma kusaini fomu za uchaguzi kwasababu matokeo ya kura za Kata za Vingunguti, Buguruni na Kiwalani hayakujumuishwa .Jaji alisema mlalamikaji alishindwa kuwaleta wagombea ubunge wa CUF na SAU mahakamani kuja kuthibitisha dai hilo na kuongeza katika ushahidi wa Mwakatobe na Mpendazoe walioutoa mahakamani walikiri kuwa hawakuwepo kwenye chumba cha kuhesabia kura na kwamba walikataa kusaini mwaliko wa Msimamizi wa uchaguzi wa kushuhudia akitangaza matokeo hayo. Aidha akiichambua hoja ya 10 na 11 ambayo mlalamikaji yeye ndiye aliyeshinda kutokana na matokeo aliyopewa na mawakala wake wa Chadema kuwa alipata kura 56,962 na kufuatiwa na Dk.Mahanga aliyepata kura 44,904 na kwamba Mpendazoe alipohojiwa na mawakili wa utetezi alidai kuwa alipata idadi hiyo ya kura za ushindi kwa makadirio na kwamba matokeo hayo alipewa na mawakala wake ambao mawakala wake waliandika idadi hizo za kura katika kipande cha karatasi ambacho amekisahau kwenye gari lake. “Kanuni ya 13(1) inayoongoza kesi za uchaguzi zinamtaka mgombea anataka kuwasilisha dai la aina hiyo dhidi ya mgombea mwenzake alishinda uchaguzi wa jimbo,mlalamikaji huyo atapaswa kwa muda usiozidi siku sita kabla ya kupangwa kwa tarehe ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa atapaswa apeleke orodha ya matokeo hayo anayodai kushinda kwa Msajili wa Mahakama ambayo anukusudia kuyatumia katika kesi yake: Na kwamba Mpendazoe hilo hakulifanya. “Kwa sababu zote za kisheria nilizozitaja hapo juu mahakama hii inatupilia mbali madai 11 ya Mpendazoe yaliyotaka nibatilishe ubunge wa Mahanga kwasababu ameshindwa kuleta ushahidi ambao ungeutisha ushahidi wa upande wa wadaiwa na kwa mahakana hiyo mahakama hii inasema Dk.Mahanga ndiye mbunge wa Jimbo la Segerea kwasababu hakuna sheria yoyote iliyokiukwa wakati wa zoezi la uchaguzi wa jimbo hilo”alisema Jaji Ibrahim. Baada ya kumaliza kusoma hukumu hiyo saa 6:53 mchana, wafuasi wa Chadema na CCM walitoka nje ya jengo la mahakama Kuu kitengo cha biashara na kufanikiwa kuifunga kwa muda barabara hiyo hukuwa wakiwa wameshika bendera za vyama vyao na wafuasi wa CCM walionekana na kusikika wakiimba CCM, CCM na wale wafuasi wa Chadema wakiimba CCM Mafisadi,CCM wezi kwa dakika tisa huku wakinyeshewa na mvua na kusababisha magari kushindwa kupita hali iliyosababisha askari kanzu na wale waliovalia kiraia ambao walikuwa wametanda kwa wingi ndani na nje ya jengo la Mahakama ya Biashara kutumia mbinu za hali ya hali ya juu kuwaondoa wafuasi hao barabani bila kusababisha uvunjifu wowote wa amani. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 3 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.