Header Ads

SERIKALI YAKWAMISHA KESI YA KIBANDA

Na Happiness Katabazi KWA mara nyingine tena upande wa Jamhuri katika kesi ya kuruhusu na kuchapisha makala inayodaiwa ni ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake, jana ulishindwa kuwasomea maelezo ya washtakiwa hao kwa madai kuwa hawakuwa tayari. Mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema , wakili wa serikali Lasdirous Komanya aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuja kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa lakini hawataweza kufanya hivyo kwasababu Mei 4 mwaka huu, walipokea barua toka kwa mshitakiwa wa pili(Kibanda) kuwa kati yta Mei 9-18 anasafiri kwenda nje ya nchi kuudhulia mafunzo na akaomba mahakama impatie hati yake ya kusafiria ili aweze kusafiri na akapewa hati hiyo na kwamba kwa sababu hiyo upande wa jamhuri ukatumaini kuwa jana mshitakiwa huyo asingekuwepo mahakamani. Wakili Komanya alidai sababu ya pili ya kushindwa kuwasomea maelezo hayo ni kwamba Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda anayesikiliza kesi hiyo yupo nje ya Dar es Salaam, kwa shughuli nyingine za kikazi , hivyo akaiomba mahakama iairishe kesi hiyo. Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa wa tatu ,Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga aliiomba mahakama hiyo impatie ruhusa mteja wake ya kwenda Afrika Kusini kati ya Mei 11-28 mwaka huu,kwaajili ya kuudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa dola wastaafu za SADC kama mwandishi wa habari mwandamizi. Hata hivyo ombi hilo lilipingwa vikali na wakili wa Serikali Komanya kwa madai kuwa ombi hilo lilipaswa lilipaswa liwasilishwa na ushahidi wa barua ya mwaliko lakini wakili Mnyere amewasilisha ombi hilo bila nyaraka hizo na kuongeza kuwa anapinga ombi hilo kwa nguvu zote hadi pale wakili huyo wa utetezi atakapoleta mahakamani uthibitisho wa nyaraka zinazoonyesha mshtakiwa huo amealikwa kuudhulia mkutano huo. Kwa upande wa hakimu Lema alilikataa ombi la Wakili Mnyere kwa madai kuwa alipaswa aliwasilishe mahakamani hapo kwa kuambatanisha na uthibitisho wa barua ya mwaliko hata kama imegushiwa na kwamba muda wowote kuanzia leo endapo ataleta uthibitisho huo mahakama hiyo itampatia ruhusa na kwamba anaiarisha kesi hiyo Juni 26 mwaka huu, itakapokuja kwaajili kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa. Mbali na Kibanda washtakiwa wengine ni mwandishi wa makala hiyo Samson Mwigamba na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando, Juvenalis Ngowi, Isaya Matamba, John Mhozya na Frank Mwilongo. Machi 7 mwaka huu, Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda. Shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake ni la kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti Na.229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwamba Novemba 30 mwaka 2011, Makunga akiwa na wadhifa huo alichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011, iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Magereza na Polisi wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 16 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.