Header Ads

BARCLAYS YAMBURUZA KORTINI MADABIDA NA MKEWE




Na Happiness Katabazi
BENKI  ya Barclays  Tanzania Limited, kimeifungulia kesi ya madai Kiwanda cha kutengeneza Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited, kinachodaiwa kumilikiwa na  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na mkewe Zarina Madabida ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), kwa kushindwa kurejesha  mkopo uliokopa katika benki hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya madai iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 147 ya mwaka 2012, ni kiwanda hicho, na wadaiwa wengine ni Madabida na mkewe Zarina na Salum Shamte.

Hati hiyo  ya madai inadai kuwa kiwanda hicho ni mdaiwa mkuu wa mlalamikaji, (Barclays) na kwamba mdaiwa wa pili, wa tatu na wa wanawajibika kwa mdaiwa  kutokana na nafasi zao kwa mdaiwa wa kwanza, wakiwa ni wadhamini katika mkopo huo.
Hati hiyo inaanisha  kuwa mkopo huo ulitolewa kwa mdaiwa wa kwanza katika makao makuu ya ofisi zake (mdaiwa wa kwanza), jijini Dar es Salaam, na   dhamana  ya mkopo huo ilitolewa na mdaiwa wa pili, wa tatu na wa nne makao makuu ya ofisi za mdaiwa wa kwanza, jijini Dar es Salaam.

Kuwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2002 na mwaka 2008, mlalamikaji Benki ya Baclays  alitoa mkopo kwa mdaiwa katika namna tofautitofauti, yenye thamani tofautotofauti, ikiwemo mikopo ya muda mfupi, hati za dhamana, hati za ufanisi, hati za viapo na mikopo ya muda mrefu.

“Hadi   kufikia Novemba 8, 2012, mdaiwa huyo wa kwanza anadaiwa mkopo wenye thamani ya Dola za  Marekani 4,551,492.86, kama mkopo wa muda mreru na hadi kufikia muda huo mdaiwa kwanza anadaiwa Dola za Marekani, 74,294.86, Sh10,051,993, katika akaunti namba 0014002677, na kwamba riba iliyoongezeka hadi kufikia Novemba 8, 2012 ni Dola za Marekani 307,825.49, na hata  hivyo hati hiyo inadai kuwa kiasi cha salio la riba ambalo halijalipwa ni Dola za Marekani 45, 631.25’ ilisomeka hati hiyo.

Aidha  mdaiwa wa pili, wa tatu na wa nne, walidhamini urejeshwaji wa mikopo hiyo lakini hata hivyo  wadaiwa hao  wameshindwa au wamepuuza kurejesha mkopo huo licha ya kudaiwa na kukumbushwa mara kwa mara.

Hivyo mdai katika kesi hiyo anaiomba mahakama itoe hukumu na kuwaamuru wadaiwa wote kwa pamoja kulipa kiasi cha Dola 4,551,492.86 kama mkopo wa muda mrefu.

Pia anaiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa walipe mikopo mingine yenye mfumo wa hati za dhamana na hati za viapo, hati za ufanisi yenye thaman ya Dola za Marekani, 74,294.86, Sh10,501,993, katika akaunti namba 0014002677.

Mbali na mikopo hiyo, mdai pia anaiomba Mahakama iwaamuru wadai walipe riba iliyoongezeka ya Dola za Marekani 307,825.49 na salio la riba ambalo halijalipwa la Dola za Marekani 45,631.25.
Madai hyo pia anaendelea kudai kuwa Mahakama iwaamuru wadaiwa walipe riba ya asilimia 12 kiasi cha riba kilichoongezeka kilichotajwa hapo, kutoka Novemba  8,2012, hadi siku ya hukumu au tarehe ya malipo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 15 mwaka 2013

No comments:

Powered by Blogger.