Header Ads

KESI YA KUPINGA WABUNGE WA EAC KUANZA KUSIKILIZWA LEO


Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Afrika Mashariki inayoketi mkoani Arusha, leo inatarajia kuanza kusikiliza usikilizwaji wa awali wa kesi ya kupinga mchakato uliofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwapata wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki kwasababu ulikiuka Ibara ya 50 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kesi hiyo Na.7/2012 ilifunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa mgombea Ubunge wa bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Antony Komu ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kesi hiyo ambayo itasikilizwa na jopo la majaji wa tano wa mahakama hiyo litaongozwa na jaji Johnston Busingye, Merry Tella, Arack Amoco, John Mkwawa,Isaac Leneoli.
Akizungumza na gazeti hili kutokea mkoani Arusha wakili wa Komu, Mbogoro alisema tayari ameishafika Arusha kwaajili ya leo kuudhulia kesi hiyo ya kihistoria  na kwamba madai ya msingi ya mteja wake ni kwamba anapinga mchakato mzima ulioendeshwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuwapata wabunge  wa Bunge la Afrika Mashariki  kwasababu mchakato wote ulikiuka matakwa ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Uanzishwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Komu ambaye naye alikuwa ni mgombewa nafasi ya bunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya Chadema, hakuweza kushinda nafasi hiyo na hivyo kufanya chama cha Chadema kukosa mbunge wa bunge la Afrika Mashariki, na Komu hakulidhishwa na mchakato huo muda mfupi baadaye aliamua kufungua kesi hii katika Mahakama hiyo ya Afrika Mashariki.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 30 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.