LULU AREJEA URAIANI,ADAI MUNGU NDIYE ALIYEMPA DHAMANA
Na Happiness
Katabazi
HATIMAYE
msanii wa filamu nchini, Elizabeth
Michael ‘Lulu’ amepata dhamana baaada ya kutimiza masharti matano aliyopewa na
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, juzi wakati mahakama hiyo ilipokuja
kusikiliza ombi lake la kuomba apatiwe dhamana katika kesi inayomkabili ya kuua
bila kukusudia aliyekuwa msainii mwenzie Steven Kanumba.
Lulu
alitimiza masharti hayo jana saa tisa Alasili kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu
Francis Kabwe na baada ya kutimiza
masharti hayo ya dhamana aliwaeleza waandishi wa habari huku akitoka machozi
kuwa anamshukuru mungu kwani yeye ndiye alifanya akapata dhamana hiyo na hivyo
kumfanya atoke gerezani na kurejea kuishi uraiani.
Lulu ambaye
alikuwa ameongozana na wakili wake Peter Kibatara alisema anawashukuru wale wote waliyokuwa nae bega kwa bega,tangu kesi
yake ilipoanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Ninachoweza
kusema ni kuwashukuru wale wote walioniangaikia na kuniombe kwa mungu hadi leo
nimepata dhamana narudi kuungana na familia yangu …lakini naomba watu hao
waendelee kuniombea kwani leo nimepata dhamana tu na ile kesi yangu ya msingi
ya kuua bila kukusudia bado haijaanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi hivyo
naombeni sana waendelee kuniombea na wasinitupe”alisema Lulu.
Msanii huyo
amedhaminiwa na Flolian Matungwa,ambaye anatoka Wizara ya Ardhi na Verus
Mboneko,ambaye anatoka Wizara ya Afya.
Lulu
alifikishwa eneo la Mahakama Kuu saa 7:58 mchana na gari ya Jeshi la Magereza
lenye namba za usajili STK 2823.Baada ya kupatiwa dhamana aliondoka na gari aina ya Land Cruser VX
V8,lenye namba za usajili T480 CFX.
Hata hivyo
wakili Kibatara, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kwaniaba ya mteja wake
anakanusha uvumi uliokuwa umeenea kuwa
Lulu akiachiwa kwa dhamana jana angeenda moja kwa moja kwenye kaburi alilozikwa
Kanumba lilopo eneo la Kinondoni na kuongeza kwa kumshukuru Msajili Kabwe kwa
kumpatia dhamana mteja wake kwani muda wa kazi ulikuwa umepita.
Juzi Jaji Zainabu Mruke muda mfupi baada
ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe
kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye amesota rumande
katika gereza la Segerea tangu Aprili mwaka jana ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1) ,(2) Cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .
Jaji Mruke
alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe kwa Msajili wa mahakama hiyo hati ya
kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam
bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa
msajili kila mwezi ,kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali ambao watasaini bondi ya Sh.milioni 20 kila
mmoja.
Baada ya
jaji huyo kutangaza masharti hayo Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi
uliokuwa ukiendeshwa kwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza
masharti hayo lakini kwa bahati mbaya Msajili hakuwepo ofisini na hivyo kufanya
Lulu kurudishwa rumande na akarejeshwa jana mchana mahakamani hapo kwaajili ya
kuja kutimiza masharti ya dhamana mbele ya msajili huyo Kabwe ambapo
aliyatimiza jana na kupatiwa dhamana.
Kufuatia
mahakama hiyo juzi kumpatia masharti ya
dhamana Lulu kutoka na ombi lake Na.125/2012 la kuomba mahakama hiyo impatie
dhamana, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili Lulu ambayo ni ya kuua bila
kukusudia bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Wasanii
waliyokuwepo kumuunga mkono Lulu mbali na mama yake mzazi mahakamani hapo
alikuwepo Mahsein Awadh maarufu Dk.Cheni, Muna na msanii mwingine mmoja.
Desemba 21 mwaka jana ,
Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi
ya kuua bila kukusudia Lulu na kuiamishia rasmi kesi hiyo katika Mahakama Kuu,
na uamuzi huo wa mahakama ulitokana na upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya
kesi yake kwa kina mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta
jumla ya mashahidi tisa.
Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Jumatano, Januari 30 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment