Header Ads

MSAJILI WA MAHAKAMA KUU AMKWAMISHA LULU
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimpatia masharti matano ya kupata dhamana kwa msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael ‘Lulu’,  anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba.

Masharti hayo yaliyolewa jana na Jaji Zainabu Mruke muda mfupi baada ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye anasota rumande tangu April mwaka jana ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1) ,(2) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .

Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe  kwa Msajili wa mahakama hiyo hati ya kusafiria,  kutotoka nje ya Dar es Salaam  bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi ,kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali  ambao watasaini bondi ya Sh.milioni 20 kila mmoja.

Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa kwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo lakini kwa bahati mbaya Msajili hakuwepo ofisini na hivyo kufanya Lulu kurudishwa rumande hadi leo atakapoletwa kwaajili ya kujatimiza masharti hayo mbele ya Msajili wa mahakama hiyo.

Kufuatia mahakama hiyo jana kumpatia masharti ya dhamana Lulu kutoka na ombi lake Na.125/2012 la kuomba mahakama hiyo impatie dhamana, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili Lulu ambayo ni ya kuua bila kukusudia bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Desemba 21 mwaka jana , Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia Lulu na kuiamishia rasmi kesi hiyo katika Mahakama Kuu, na uamuzi huo wa mahakama ulitokana na upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 29 mwaka 2013  

No comments:

Powered by Blogger.