MCHUNGAJI, MLINZI KANISA LA KKKT MBAGALA WASIMULIA VURUGU ZA KUCHOMA KANISA HILO
Na Happiness Katabazi
MCHUNGAJI Kanisa la Kilutheri la
Kiinjili (KKKT), Usharika wa Mbagala jijini Dar es Salaam, Frank John
(32) jana ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyoruka ukuta
wa Kanisa na kujificha katika Benki ya CRDB tawi la Mbagala
ili kunusuru maisha yake kwa kukwekwa kundi la watu wasiyofahamika kuvamia eneo
la kanisa hilo na kufanya uharibifu.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hii ni
Hamid Senkondo, Shego Shego, Mashaka Iman, Hamza Mohamed, Juma Mbegu, Issa
Abdallah, Hamis Kimwaga, Ramadhan Mburu na Mohamed Yusuph, wanakabiliwa na
makosa ya kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha,wizi wa vifaa mbalimbali mnamo
Oktoba 10, 2012, ndani ya kanisa hilo.
John alitoa maelezo hayo jana mbele ya
Hakimu Mkazi Waliarwande Lema,wakati
alipokuwa akiongozwa na wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka kutoa
ushahidi wake katika kesi ya kula njama ,
kuvunja jengo hilo kwa nia ya kutenda kosa, kuharibu mali kwa makusudi, unyang’anyi
wa kutumia silaha na kuchoma mali za kanisa hilo kwa makusudi
inayowakabili washtakiwa kumi mahakamani hapo.
Mchungaji John alidai kuwa Oktoba 12, mwaka jana
akiwa ndani ya ofisi za kanisa hilo kwa ajili ya kazi zake za
kawaida alipigiwa simu na
kujulishwa kuwa kuna vurugu na kwamba wawe makini.
“Baada ya kupata taarifa hiyo nilifikia
uamuzi wa kufunga ofisi na kumfuata
mlinzi awe tayari na nipange ulinzi ,lakini ghafla nilishtukiwa tumeishavamiwa na kundi kubwa la watu waliokuwa
wakirusha mawe na matofali. Kutokana na uvamizi huo na taarifa
nilizozipata moja kwa moja nilijua nipo hatarini.”alidai Mchungaji John.
Alieleza kuwa kutokana na uvamizi
askari aliyekuwa akilinda lindo la
kanisa hilo siku hiyo , Michael Samuel (30) alipiga risasi moja hewani, na
kundi hilo la watu lilitawanyika ,na
mlinzi yule alipiga risasi ya pili lakini haikusaidia kwasababu ganda la risasi ya kwanza lilikwama ndani ya bunduki.
“Wakati mlinzi yule akiangaika
kuirekebisha bunduki yake iliyokuwa imekorofisha , kundi lile la watu ambao hawakuweza kuwatambua
lilirudi tena na kuanza kurusha vipande vya matofali na mawe ,
Hivyo ‘nikazunguka nyuma ya kanisa, nikaruka ukuta ili kuokoa maisha
yangu na kukimbilia katika benki ya CRDB tawi la Mbagala
kujificha.” Alidai shahidi huyo.
Mchungaji huyo alidai kuwa yote hayo
yalifanyika majira ya mchana lakini hakumbuki ilikuwa ni saa ngapi na kwamba
baada ya tukio hilo alimpigia simu Mwinjilisti wa kanisa hilo ili kuweza
kujua kama hali imetulia na baada ya Mwinjilisti kumjulisha kuwa
hali imetulia alikwenda kanisani hapo ambapo aliwakuta askari wa jeshi la
polisi ambao nao walimuweka chini ya ulinzi hadi alipowaonyesha
kitambulisho chake kuwa yeye ni Mchungaji.
“Nilipoonyesha kitambulisho niliachiwa
nikaona milango, uzio wa Kanisa, ofisi ya mchungaji, zimeharibiwa na thamani
mbalimbali zimeibiwa huku Membari ikiwa imechomwa moto na maboksi sita ya kuwekewa sadaka na mengine niliyaona
katika ofisi ya mchungaji yakionekana kuwa yalitumika kukokewa moto
kwenye ofisi ya mchungaji.” Alieleza.
Kwa upande wake shahidi wa kwanza , Michael Samuel
ambaye ni mlinzi wa kanisa hilo alieleza mahakama hiyo jana kuwa Oktoba
11, mwaka jana aliingia kazini na ilipofika saa 12 jioni hali
ilikuwa shwari na ilipofika
Oktoba 12, mwaka jana,saa 5 asubuhi watu waliokuwa na vipande vya
matofari na mawe walipowavamia na kuyarusha kuelekea ndani ya kanisa hilo na
baada ya hali hiyo ya hatari kutokea aliamua kupiga risasi moja kuelekea juu,
kundi hilo la watu lilitawanyika na kukawa na amani.
Samwel alidai baada ya kundi lile la watu kutawanyika, yeye
alianza kufungua bunduki na kuona ganda la risasi likiwe limeganda hivyo
kufanya risasi ya pili kushindwa kutoka na kwamba baada ya saa moja kupita kundi
lile la watu lilirudi tena kwa mara ya pili na kuanza kufanya
mashambulizi makalikwa mashambulizi makali.
“Baada ya kuona hivyo na bunduki
imekorofisha nikaamua kujificha kwenye
upenyo na hatimaye nikaruka ukuta na kukimbia ili kuokoa maisha yangu. Hivyo
mengine yaliyokuwa yakitokea sikuyajua wala idadi ya watu hao sikuweza
kuifahamu kwa sababu ilikuwa kama vita, mimi nilichoangalia ni
kusalimisha roho yangu.” Alidai.
Alidai kuwa alipofanikiwa kukimbia
kutoka katika eneo hilo, hakurejea tena katika eneo hilo nyakati za jioni
alipokwenda kufuata nguo zake ambazo nazo hakuziona na kuona
mazingira na vitu mbalimbali mali ya kanisa vikiwa vimeharibiwa
ikiwemo uzio wa kanisa ulikuwa umebomolewa, membari imeunguzwa moto, mageti ya
milangoni na madirishani yamebomolewa, feni zimevunjwa na ofisi ya
mchungaji imechomwa moto. Hakimu Lema aliiahirisha kesi hiyo hadi
Februari 4, mwaka huu itakapoendelea kwa ushahidi.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 22 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment