WANA MTWARA NI KWELI BOMBA LA GESI KUJA DAR?
Na Happiness
Katabazi
MWISHONI mwaka jana baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara walifanya maandamano ya amani
wakishinikiza kuwa gesi iliyogundulika
Mtwara iwanufaishe watu wa mkoa huo.
Wananchi hao
miongoni mwao walibeba mabango mbali
kwa lengo la kufikisha ujumbe wao
huo ambapo pamoja na madai mengine wanataka bomba la gesi lisijengwe kutoka Mtwara
kuja Dar es Salaam.
Kimsingi
wananchi wale ambo wengine walikuwa wamebeba bendera za vyama vya siasa walikuwa wakiitumia haki yao ya Kikatiba iliyoainishwa
wazi kwenye Ibara ya 18(a) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 , inayosomeka hivi ; ‘kila mtu
anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake’.
Lakini
wakati wakazi wa Mtwara mkiifurahia haki hiyo ya Kikatiba nataka mtambue kuwa Rais wa
nchi ndiyo msimamizi wa ardhi yote hapa nchini kwa niaba ya
wananchi wote.Natunapozungumzia ardhi maana yake ni kila kitu kilichopo juu na
ndani ya ardhi.Na kifungu cha 45 cha Sheria ya Ardhi ,kinampa mamlaka rais
kubadili matumizi ya ardhi fulani kwaajili ya maslahi ya umma.
Nasema kama
kweli wananchi wale waliandamana kwa madai hayo,kwa maoni yangu nasema siungi
mkono dai lao hilo linalotaka bomba la gesi lisiunganishwe kuja Dar es Salaam kwani ni wazi kabisa madai hayo yameanza
kujenga ubinafsi na ubaguzi baina ya wananchi wa mikoa na mikoa.
Hivi kweli
kama leo hii hao baadhi ya wananchi wa Mtwara wanaodai Gesi isije Dar es
Salaam,si kesho wakazi wa Ruvu Mkoa wa Pwani nao wataibuka na kuandaa
maandamano ya kutaka yale maji ya kunywa tunayokunywa wa kazi wa Dar es Salaam
yasiruhusiwe tena kupelekwa Dar es Salaam, kwani maji hayo ni mali ya wakazi
mkoa wa Pwani?
Kama ajenda
hiyo ya kina ‘Chinga’ itakubaliwa si kesho hapa nao watu wakabira la Wakwere
wataibuka na kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete ni rais wao na si rais wa makabila
mengine yaliyomo ndani ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania?
Kama ajenda
hiyo ya kina ‘Chinga’ ikikubalika basi na sisi Wayambo, wahaya na Wachaga nao waanzishe
maandamano ya kutaka ndizi tunazolima katika mikoa yetu ya Kagera na Kilimanjaro
zisije kuuzwa Dar es Salaam?
Na kama
ajenda ya kina Chinga’ itakubaliwa basi
na sisi wakazi wa Dar es Salaam, tuandae maandamano ya kutaka
‘Chinga’wasiruhusiwe kuja Dar es Salaam, kufanyabiashara ndogondogo?
Nyie wa kina
chinga mbona mwaka 2000-2010 mtoto wenu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alivyokuwa
rais wa Jamhuri, mbona hamkujitokeza hadharani kusema huyo ni rais wa kina
Chinga kwasababu ni mzaliwa wa Mtwara?
Kwanza
tuwaulize hao waandamanaji kama wanaushahidi wowote unaonyesha kuwa serikali ilishawahi kutoa azimio ya kuwakataza wawekezaji
wasijekuwekeza huko Mtwara? Na je hiyo gesi ikifungwa bomba ikapelekwa Dar es
Salaam, ndiyo wakazi wa Mtwara mtakuwa hampati nishati hiyo?
Au wakazi
hao wanaweza kutoa ushahidi wowote unaonyesha endapo bomba hilo la gesi
likifungwa kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, basi mkoa huo wa Mtwara utarudi
nyuma kimaendeleo na gesi wanayoitumia hivi sasa wakazi wa Mtwara itapungua kwa
kiasi kikubwa?
Leo baadhi
ya wakazi wa Mtwara mmeandamana kutaka gesi isipelekwe Dar es Salaam, kesho
basi nao wakazi wa mkoa wa Lindi nao waandamane wakatae gesi iliyopo Kisiwa cha
Songongoso wilaya ya Kilwa isiendelee
kuletwa Dar es Salaam?Huu ni ubinafsi na ni tishio la usalama kwa taifa hili
siku za usoni.
Kwani huwezi
kuwa na wananchi ambao wanatumia gesi hiyo iliyopo kwenye ardhi wanayoishi
lakini hawataki gesi hiyo itumiwe na wananchi wenzao wanaishi katika mikoa
mingine katika nchi moja.Tusikubali.
Mbona nyie
baadhi ya wakazi wa Mtwara hamna shukurani? Hivi Mtwara ya leo ni sawa na
Mtwara ya miaka 30 iliyopita?
Nimezunguka
Mtwara katika wilaya zake zote kwa zaidi ya mara nne.Mara ya kwanza ilikuwa
mwaka 2004, 2005 mbapo nilizunguka mara mbili na aliyekuwa mgombea urais wa
Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk.Sengondo Mvungi na aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha
Tanzania Labour (TLP), Agustine Mrema na mwaka 2010 nilizunguka tena nchi nzima
yaani Tanzania Bara na Zanzibar na aliyekuwa mgomea mwenza wa CCM, Dk.Mohamed
Gharib Bilal, hakuna ubishi kuna mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo
ukilinganisha na Mtwara ile niliyokuwa nikisiikia na kuona mwaka 2004 yamefikiwa
licha bado jitihada zaidi zinatakiwa ziongezwe.
Barabara
zinapitika licha nyingine hazijawekwa lami,nyumba za kulala wageni pale Mtwara
mjini zimeongezeka, maofisi ya sekta
binfasi na serikali yameongezeka ukilinganisha na zamani na ndiyo maana leo hii
ndugu zetu waliohamishiwa Mtwara kikazi wamekuwa wakitutambia kuwa barabara ya
kutoka Dar es Salaam, kwenda Mtwara inawapa jeuri kwani imesaidia sana uhakika
wa usafiri kwani hivi sasa unatoka Dar es Salaam asubuhi Mtwara unafika saa
tisa alasairi.Mbona hatua hii ya maendeleo iliyopigwa hamuisemi?
Tayari kuna
habari ambazo zijazithibitisha kuwa maandamano yale yana nguvu nyuma ya
wanasiasa uchwara na wenye hulka za
kinyanga’u ambao ndiyo hasa wanawachochea
baadhi ya wananchi ambao hata ukiwauliza wanafahamu hata majina ya
wataalamu waliyogundua gesi hiyo ardhini ni nani hawamjui, waandamane.
Watu wa nchi
hii siku zote hawanaga siri ,ipo siku itakuja kubainika hadharani kuwa ni
manyang’au gani ya kisiasa yanaamasisha chuki hiyo na kuchochoea maandamano hayo na ubinfasi huo wa kusema
bomba la gesi lisiunganishwe kutika Mtwara kuja Dar es Salaam.
Nihitimishe
kwa kutofautiana na wale baadhi ya wakazi wa Mtwara wanaokataa bomba la gesi
lisijengwe kuja Dar kwani ni ubinafsi wa hali ya juu na ubaguzi na pia naiomba
serikali nayo iweke wazi kwa wananchi wa Mtwara faida kama za afya, elimu,
mazingira na kiuchumi baada ya bomba hilo kuunganishwa kuja Dar es Salaam.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika
0716 774494
Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
, Januari 3 mwaka 2013
Facebook; happy katabazi
No comments:
Post a Comment