Header Ads

MAOFISA HALMASHAURI JIJI DAR KORTINI KWA UBADHILIFU WA FEDHA ZA UMMA


Na Happiness Katabazi
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), jana ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhasibu  Msaidizi  na Afisa Maalipo Mkuu, Elida  Mponda wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wenzake wanaokabiliwa na makosa 90 ya kula njama,wizi na kuisababishia halmashauri hiyo ya jumla ya Sh 306,258,270.
Mbali na Mponda washtakiwa wengine ni Mhasibu  na Mkusanya wa Mapato, Geofrey Kibasa na  Afisa wa Mapato, Ernest Maduhu wote wafanyakaz wa Halmashauri hiyo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU , Hellen Osujaki alidai kuwa washtakiwa hao walifanya makosa hayo kinyume na vifungu vya  306,258, 270 na 284 A (1) vyote vya sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa mrekebisho mwaka 2002.
Osujaki alidai kuwa  kati ya mwezi Januari, 2004 na Juni, 2007 mshtakiwa Mponda akiwa  ni mwajiriwa wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kama Mhasibu Msaidizi na Afisa Maalipo Mkuu kwa uzembe aliisababishia serikali  hasara ya Sh 379,868,665.04.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa kati ya  Januari 2005 na Juni 2007, Kibasa kwa wadhifa wake na akiwa mwajiriwa wa halmashauri hiyo kwa uzembe aliisababishia serikali hasara ya Sh 87,576,091.11.
Osujaki  alidai kuwa  kati ya Januari 2004 na Septemba 2005 na Novemba 2005/ Januari 2007,  Maduhu akiwa wajiriwa wa Halmashauri hiyo ya  kama Afisa wa Mapato kwa uzembe aliisababishia serikali  hasara ya Sh 187,051,169.55.
Mbali na kuwasomea mashtaka hayo,mwendesha mashtaka huyo   aliiomba mahakama itoe hati ya kumkamata Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Mahesabu wa Halmashauri hiyo Fatiel Emmanuel ili waweze kuja kumuunganisha katika kesi hiyo ambapo mtuhumiwa huyo naye ameisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh milioni 347.9.
Katika kesi hiyo, namba 13 ya mwaka 2013, hati ya mashtaka inaonyesha Elida anakabiliwa na jumla ya mashtaka 71 yakiwamo ya kula njama, wizi  na kuisababishia hasara serikali.
Katika mashtaka hayo, Elida anadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti tofati kati ya mwezi Januari, 2004 na  mwezi Juni, 2007 alikuwa akiiba fedha mbalimbali za makusanyo ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo ambazo ni mali ya mwajiri wake na kuzibadilisha  kwa kuonyesha hundi  zilizokuwa zilizolipwa na kampuni mbalimbali.
Kampuni hizo ni  kampuni ya Superdoll, benki ya NBC, kampuni ya Scania, kampuni ya Gapco, Hoteli ya Temirnal, kampuni ya Sanya, Benki ya NMB, benki ya CRDB, Msae Investment, kampuni ya Scandnavia, benki ya Azania, benki ya Baclays, benki ya Standard Chertered, benki ya Exim, Wizara ya Fedha na Tanzania Investment.
Naye Kibasa kwa mujibu wa hati ya mashtaka inaonyesha anakabiliwa na jumla ya mashtaka 16 ya wizi na kuisababishia serikali hasara, wakati mshtakiwa Maduhu akikabiliwa na shtaka la kuisabishia serikali hasara.
Hata hivyo washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa jamhuri ukadai upelelezi bado haujakamilika.Na mawakili wa washtakiwa ambao ni  Ademba Gomba, Alipo Mwamanenge na Jesro Tuliamwesiga waliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wao hao kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhamana kisheria.
Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Nongwa aliwataka washtakiwa hao kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya nusu ya mali ambayo washtakiwa wanatuhumiwa kuiba.
Pia alimtaka Elida kuwasilisha fedha taslimu Sh 190 milioni mahakamani hapo au  hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Mbali na Elida, alimtaka Geofrey kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni 44  mahakamani hapo ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha na kwa upande wa mshtakiwa, Ernest yeye alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni 94 mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika  yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Baada ya kutoa masharti hayo ya dhamana, Hakimu Nongwa aliwaambia washtakiwa hao kuwa hati zote za mali ni lazima zihakikiwe kama ni halali na kuiahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, mwaka huu na hivyo kufanya washtakiwa wote kwenda rumande.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 23 mwaka 2013

No comments:

Powered by Blogger.