Header Ads

WEREMA APIGANIA UBUNGE WA AESHI



Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)nchini,Jaji Fredrick Werema  amewasilisha sababu 10 katika Mahakama ya Rufani nchini akiomba mahakama hiyo itengue hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga ambayo Aprili mwaka jana ilimvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini(CCM), Aeshi Hillary kwasababu hukumu ile ilikuwa na dosari za kisheria.
Sambamba na hilo pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), ameomba mahakama hiyo ya juu kabisa nchini itoe amri ya kusitisha utekelezwa wa hukumu.
Rufaa hiyo iliwasilishwa chini ya hati ya dharula ambayo bado haijapangiwa jopo la majaji wa kuanza kuisikiliza, mrufani(mwanasheria Mkuu), anaiomba Mahakama ya Rufani  itangaze kwamba uchaguzi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini uliofanyika Oktoba 31, 2010, ulikuwa ni wa huru na wa haki hivyo matokeo ya yalimtangaza Hillary kuwa mshindi, yalikuwa ni halali na yalikidhi matakwa ya Sheria ya Uchaguzi na Kanuni zake.

Mbali na AG, warufani wengine ni  Justus Kasirama (msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Katandala) na Vistus Kapufi (msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Matanga), walikata rufaa hiyo Januari 10, mwaka huu, dhidi ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo hilo kupitia CHADEMA Nobert Yamsebo na Aeshi.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya rufaa, warufani hao wanadai waneleza kuwa wamefikia uamuzi wa kukata rufaa hiyo chini ya hati ya dharula kwasababu   Jimbo la Sumbawanga Mjini halina mwakilishi tangu matokeo ya uchaguzi yalipofutwa  Aprili 30, 2012 na hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga iliyotolewa na Jaji Bethuel Mmila na kwamba ikiwa rufaa hiyo haitaamriwa wakazi wa Jimbo hilo wataendelea kubaki kuwa hawana mwakilishi bungeni.
“Tunaiomba  Mahakama itoe amri ya kuifuta hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ambayo ilimvua ubunge Hillary  na pia itoe amri ya kuiweka kando amri ya utekelezwa wa hukumu ile….na pia “tunaiomba mahakama ya rufani itangaze kwamba uchaguzi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini uliofanyika Oktoba 31, 2010, ulikuwa ni wa huru na wa haki hivyo matokeo ya uchaguzi yalikidhi matwaka ya Sheri ya Sheria,” ilieleza hati hiyo ya rufaa.

Miongoni mwa sababu zilizoainishwa na wakata rufani ni kwamba Mahakama Kuu ya Sumbawanga, ilijielekeza vibaya kisheria kupanga tarehe ya kusikiliza na hatimaye kutoa uamuzi katika kesi ya uchaguzi kabla ya mdaiwa wa kwanza (Yamsebo) kuweka dhamana ya gharama(security of Cost).
Aidha waomba rufaa hao wanadai Jaji Milla alikosea kisheria kuamuru kwamba kutofautiana  kwa ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mlalamikaji, hakukuwa na uzito ambao ungesababisha kuvuruga msingi wa haki.
Aidha, wanadai  Jaji alikosea kisheria kwa kusema kwamba  kulikuwepo na vurugu katika mikutano ya kampeni ya Yamsebo katika vijiji vya Kisumba na Namtimbwa Septemba 5 na Oktoba 22, mwaka 2010.
Warufani hao  wanadai kutokana na kupingana kwa ushahidi wa mashahidi wanne, Jaji huyo alikosea kusema  kwamba usumbufu uliotokea katika vijiji hivyo uliathiri mikutano ya kampeni zile za ubunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini.
 
 Pia, wanadai Jaji alijielekeza vibaya kwa kushindwa kuchambua ushahidi uliotolewa kwa kiwango kinachotakiwa cha kuthibitisha pasipokuacha mashaka  yoyote na matokeo yake alifikia uamuzi ule wa kumvua ubunge Aeshi ,uamuzi ambao wanadai siyo sahihi kisheria.
Mbali na hayo, wanadai kuwa Jaji alikosea kisheria kwa kuhamisha jukumu la kuthibitisha kesi kutoka kwa mlalamikaji wa kwanza (Yamsebo) kwenda kwa (Aeshi), kwa madai kuwepo kwa rushwa ambayo inadaiwa kutolewa  Oktoba 29, mwaka 2010, katika Shule ya Msingi Kantalamba na  kuamua madai hayo yalithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Pia Warufani hao wanadai pia Jaji alikosea kuamua kwamba mashahidi wawili wa utetezi walikuwa mawakala wa mlalamikiwa wa pili (Aeshi) na ndio waliotoa hiyo rushwa inayodaiwa huku akijua na kwa idhini yake.
Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 17 mwaka 2013

No comments:

Powered by Blogger.