Header Ads

MASHAHIDI WA SERIKALI WAKWAMISHA KESI YA PONDA


Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa jamhuri  katika kesi ya uchochezi na wizi wa mali ghafi za Sh milioni 59 inayomkabili Katibu Mkuu  wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49    kwasababu mashahidi watatu wa upande wa jamhuri walikuwa wanatarajiwa kufika jana mahakamani hapo kutoa ushahidi wao hawakuweza kufika kutokana na sababu mbalimbali.
 
Mbali na hatua hiyo, Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ametoa hati ya kukamatwa kwa shahidi mmoja wa upande wa jamhuri ambaye naye alipaswa afike jana kutoa ushahidi lakini hakuweza kufika bila kutoa sababu ya kushindwa kufika hapo na wakati alishapewa nakala ya wito wa kuitwa mahakamani na akausaini lakini jana akashindwa kufika mahakamani hapo bila kutoa taarifa.
 
Hakimu Nongwa alisema anakubaliana na ombi la Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka  na Yasinta Peter ambao waliomba kesi hiyo jana isiendelee kusikilizwa badala yake iairishwe kwasababu mashahidi watatu walikuwa wamewaita leo waje  kutoa ushahidi hawakuweza kufika na hivyo anaiarisha kesi hiyo hadi Janauri 14 itakapokuja kwaajili ya kutajawa na kusema kuwa siku hiyo mshtakiwa wa kwanza Ponda na mshtakiwa wa tano Mukadam Abdal Swalehe(45) ambao wanaishi gerezani kwasababu dhamana zao bado zimefungwa na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi ndiyo wafike mahakamani ila washtakiwa wengine ambao wapo nje kwa dhamana siku hiyo wasije mahakamani na kwamba Januari 17 mwaka huu, kesi hiyo itakujwa kwaajili ya kuendelea kusikilizwa na mashahidi wafike bila kukosa.
 
Awali kabla ya Hakimu Nongwa kuarisha kesi hiyo, Wakili Kweka alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya mashahidi nne, tano na sita waanze kutoa ushahidi wao ila kwasababu ambazo zipo nje ya uwezo wake mashahidi hao ambao alikataa kuwataja majina yao  wameshindwa kufika mahakamani kwasababu shahadi mmoja ni mgonjwa, mwingine kasafiri na mwingine alisaini wito wa kuitwa mahakamani lakini hajatokea mahakamani bila ya kutoa taarifa na kwamba wanaiomba mahakama hiyo itoe hati ya kukamatwa kwa shahidi huyo ambaye ameshindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa.
 
Kwa upande wake wakili wa washtakiwa Mansoor Nassor alidai kuwa siku zote wamekuwa wakiomba wapatiwe majina ya mashahidi na upande wa jamhuri lakini jamhuri imekuwa ikakataa kuwapatia majina hayo na kwamba kupitia maelezo ya wakili Kweka leo ambayo alieleza kuwa walikusudia jana kuleta mashahidi mashahidi wa tatu ,ina maana Kweka anawafahamu kwa majina mashahidi hayo na akaimba mahakama imtake Kweka ataje majina hayo ya mashahidi lakini hata hivyo hakimu huyo akuzungumzia hoja hiyo ya wakili Mansoor na akaiarisha kesi hiyo na kutoa hati ya kukamatwa kwa shahidi wa upande wa jamhuri ambaye ameshindwa kufika mahakamani hapo bila kutoa taarifa.
 
Oktoba 18 mwaka  jana,wakili Kweka alilidai  kosa la kwanza  ni la kula njama ambalo linawakabili washitakiwa wote,kosa la pili ni kwaajili ya washitakiwa wote ambalo ni la  kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha  85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Oktoba 12 mwaka huu huko Chang’ombe Markas, wasipokuwa na sababu za msingi waliingia kwa jinai kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia ya iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi ambapo baada ya kuvamia waliiba vifaa na malighafi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza na kosa la tano ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo sasa kosa hili la uchochezi litamkabili Mukadamu na Ponda peke yao  kuwa wakiwa ni viongozi wa jumuiya hiyo , Oktoba 12 mwaka huu ,waliwashawishi wafuasi wao watende makosa hayo hata hivyo walikanusha mashtaka yote.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari Mosi mwaka 2013

No comments:

Powered by Blogger.