Header Ads

UB YAPATA SERIKALI YA WANAFUNZI



Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Chuo Kikuu Kipya cha Bagamayo (UB) chenye makoa yake Makuu Mikocheni jijini Dar es Salaam, kimepata serikali mpya ya mpito ya wanafunzi.

Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa jana katika chuo hicho chenye madarasa yake eneo la Kawe Beach, Katibu wa Tume ya Katiba ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Debora Charles ambaye pia ni mwanafunzi, alisema katika nafasi ya raia wa serikali ya wanafunzi jumla ya wagombea walikuwa ni wanne na jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa ni 149.

Debora alisema mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa fani ya Information Communication Technology(ICT),Vicent Jonas  aliibuka mshindi baada kupata kura 65 kati ya 149 zilizopigwa na hivyo kufanya Katibu huyo kumtangaza kuwa Jonas ndiye rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho kipya cha Bagamayo(UB) ambacho kilianza rasmi mwaka wa masomo, Novemba 2011. 

Aidha Debora alisema  nafasi ya Makamu wa Rais imechukuliwa na Mubaraka Salum ambaye alishinda kwa kura 42 kati ya kura 122 zilizopigwa na Katibu Mkuu anakuwa Alex Mhando  na Waziri Mkuu wa serikali hiyo wa wanafunzi  anakuwa Dickson Msaki na kuongeza kuwa serikali hiyo ni ya mpito ambayo itakaa madarakani hadi pale Tume ya Katiba ya Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho itakapomaliza kutunga Katiba ya wanafunzi ambapo kwasasa Tume hiyo ipo katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wanafunzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kutangazwa kuwa rais wa serikali ya wanafunzi wa UB, Jonas alisema kwanza anashukuru uchaguzi umeendeshwa kwa amani,utulivu na ustaarabu wa hali ya juu ukilinganisha na  chaguzi nyingine za serikali za vyuo vingine kwani chaguzi nyingine za serikali za vyuo vingine zimekuwa zikigubikwa na vurugu.

“Kwanza naomba ieleweke wazi kuwa mimi na nyie wote wote mliopiga kura ni wanafunzi na kilichotuleta hapa UB ni kusoma ,hivyo katika uongozi wangu huu wa mpito natambua changamoto zipo ila nitaakikisha wanafunzi wote tunaendeleza mshikamano, amani na kuzingatia kile kilichotuleta hapa chuoni na kuakikisha nafikisha yale yote mnayoyataka yafanyike katika uongozi wa chuo’alisema Rais Jonas.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 17 mwaka 2013.


No comments:

Powered by Blogger.