KIWANJA CHA CHANG'OMBE MARKAS, SI MALI YA WAISLAMU-MASHAHIDI
Na Happiness Katabazi
MWENYEKITI
wa Baraza la Wadhamini la (BAKWATA),Masoud Ikome(72), jana ameithibitishia
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kiwanja kilichopo Chang’ombe
Markas ni mali halali ya kampuni ya
Agritanza Ltd na siyo mali waislamu(Bakwata).
Itakumbukwa
kuwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda Issa na
wenzake 49 , Oktoba mwaka jana walivamia eneo la Kiwanja hicho kwa madai kuwa
kiwanja hicho ni mali ya Waislamu na hivyo polisi kulazimika kuwakamata na
kuwafikisha mahakamani kwa makosa mbalimbali.
Ikome
ambaye ni shahidi wa nne katika kesi ya uchochezi na
wizi wa mali za sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda Issa na wenzake 49 ,alitoa maelezo hayo jana
wakati akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka kutoa ushahidi
wake ,kwasababu jana kesi hiyo ilikuwa imekuja kwaajili ya kuendelea
kusikilizwa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa.
Ikome
ambaye alianza kwa kuyataja majukumu ya baraza la wadhamini la Bakwata kuwa ni
kumiliki mali za waislamu wote nchini ambazo zinaamishika na zisizoamishika
kama viwanja, nyumba, magari,vifaa na kwamba baraza analoliongoza linapata
nguvu za kuongoza kutoka kwenye Baraza la Maulamaa.
Ikome
akijibu swali la wakili Kweka lilomtaka aeleze anafahamu nini kuhusu kiwanja
hicho cha Chan’gombe Markas, alidai kuwa anachokifahamu ni kwamba akiwa na
Mwenyekiti wa Baraza hilo mwaka 2010 aliitisha kikao cha wajumbe wa baraza na
wakazungumzia kuhusu hitaji la Bakwata kupata eneo kubwa la kujenga Chuo Kikuu
na kwamba wakafikia uamuzi wa kufanya mabadilishano ya kiwanja hicho kilichopo
Markas ambacho awali kilikuwa kikimilikiwa na Bakwata ambacho kina ukubwa wa
hekari nne na wakabadilishana na Kampuni ya Agritanza Ltd ambapo kampuni hiyo iliipatia Bakwata hekari 40 zilizopo Kisarawe na hatimaye
Bakwata lile eneo la Markas wakaipatia kihalali kampuni hiyo.
“Na
kabla kikao cha baraza langu hakijafikia uamuzi huo, tayari baraza la Maulamaa
lilishaketi na kufikia uamuzi huo wa kubadilisha kiwanja hicho na kampuni hiyo
kwa hiyo kikao cha baraza langu nacho kiribariki azimio hilo na mkataba
ukaandaliwa na hatimaye makabidhiano ya kubadilishana ardhi hiyo yakafanyika
….kwa hiyo leo hii anapoibuka mtu anasema kiwanja cha Chang’ombe Markas ni mali
ya Waislamu anakosea sana kisheria kwani ile si mali tena ya waislamu “alidai
Ikome.
Akijibu
maswali ya mawakili wa utetezi yaliyokuwa yakiulizwa na Nassor Mansoor na
wenzake kuwa nyaraka za kuonyesha vikao vya mabaraza hayo ya maulamaa na baraza
la wadhamini vilikaa zikowapi na ataje
kama kiwanja cha Kisarawe kilifanyiwa tathimini, kinathamani gani na
kwamba ni kwanini kila jambo analoulizwa anadai hakumbuki.
“Sikiliza
wewe wakili, misiwezi kukumbuka kila kitu nimeishakwambia kuwa makubaliano ya
kubadilishana kiwanja hicho yalifanyika katika vikao halali na nyaraka hizo
zipo ofisini na kuhusu eneo la Kisarawe kama lilifanyiwa tathimini ,linathamani
gani,waulize wataalamu watakujibu misiwezi kukujibu ….na ninafahamu kuwa
unataka neno sijui,sijui litoke mdomoni mwangu…namimi nakwambia hivi hutalipata
neno sijui kutoka mdomoni mwangu minakujibu sifahamu kwani hata wewe huwezi
kukumbuka kila kitu ila kuhusu maswali ni rahisi sana kama wewe
unavyoniuliza”alidai Ikome na kusababisha watu kuangua vicheko.
Kwa
upande wake shahidi wa tano ambaye ni miongoni mwa Wakurugenzi wa Kampuni ya
Agritanza Ltd, Afidhi Seif Othman
(42), aliambia mahakama kampuni yake ya
Agritanza Ltd ilibadilisha eneo la Chang’ombe na Bakwata na kwamba yeye ndiye
alikuwa mmiliki wa eneo la Kisarawe na ndiye aliyeipatia Bakwata eneo hilo na
Bakwata ikawapatia eneo la Chang’ombe na kwamba mabadilishano hayo yalifanyika
Oktoba 10 mwaka 2010.
Othman alidai kuwa baada ya kubadilishana
Oktoba mwaka jana kampuni yake ilinunua vifaa mbalimbali kwaajili ya kuanza
kujenga ukuta wa kutenganisha kiwanja cha Agritanza Ltd na Chang’ombe Markas
ambacho ndicho kampuni yake imepewa na Bakwata na kwamba wakati wakianza kuanza
ujenzi huo.
Kwamba
mlinzi na mjenzi waliokuwa wakijenga hapo Markas walinipigia simu asubuhi wakaniambi mshtakiwa
wa kwanza(Ponda), yupo katika kiwanja hicho ameambatana na mpigapicha
wanakipiga picha kiwanja hicho na kwamba yeye akamwambia mlinzi huyo ampatie
simu azungumze na Ponda ambapo alimuuliza Ponda kwanini amefika eneo hilo
, Ponda alimtaka yeye ampigie simu saa
mbili usiku wa siku hiyo.
Akadai
ilivyofika saa mbili usiku akampigia Ponda, na Ponda akamtaka akutane nae siku
ya tatu yake na siku ya tatu yake shahidi huyo alienda kukutana na Ponda katika
Msikiti wa Mtambani na ilikuwa ni siku ya Jumanne wakaanza mazungumzo yao
ambapo Ponda alimweleza Bakwata wamekosea kubadilisha kiwanja hicho bila ya
kuishirikisha taasisi yake na kwamba shahidi huyo akamwambia kama Bakwata
wamekosea basi kampuni yake ipo tayari kuipatia taasisi ya Ponda nayo eneo
jingine.
Baada
ya kumaliza majadiliano hayo alidai kuwa alhamisi yake alipata taarifa za siri
kuwa Ponda na wafuasi wake walikuwa wamepanga kesho yake(ijumaa),kuja kuvamia
katika eneo la kiwanja hicho cha Chang’ombe Markas na kwamba yeye alichokifanya
alienda Kituo Kikuu cha Polisi Kati kutoa taarifa ambapo mapolisi walimtaka
aende kituo cha Chang’ombe akatoe taarifa hizo na akaenda Chang’ombe siku hiyo
ya Alhamisi ambapo mapolisi wa Chang’ombe walimweleza kuwa asuburi hadi tukio
hilo la uvamizi litendeke.
“Kweli
ilipofika Ijumaa, Ponda na kundi la
wafuasi wake walivamia katika kiwanja hicho wakiwa na mbao,nondo na wakaanza
ujenzi na wakati wanavamia eneo hilo na sisi tulikuwa tumeweka vifaa vyetu vya
ujenzi wa ukuta vyenye thamani ya Sh.milioni 59
ambapo nao walianza kujenga na
upande mmoja wa ukuta waliandika neno linalosomeka Masdji Hassan Bin Amir na walikaa katika eneo hilo kwa zaidi ya siku
mbili hadi Oktoba 12 mwaka jana walivyoondoka na wengine kukamatwa na jeshi la
Polisi “alidai Othaman.
Kesi
hiyo ambayo ilimalizika jana saa tisa Alasiri iliarishwa hadi Januari 31 mwaka
huu,na akaamuru Ponda na Mshtakiwa wa tano warudishwe gerezani kwasababu bado
Mkurugenzi wa Mashtaka(DDP),Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana, na
kwamba siku hiyo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya shahidi wa sita wa upande wa
jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake.Hata hivyo kadri siku zinavyozidi kwenda
idadi ya wafuasi wa Ponda kuja mahakamani kusikiliza kesi hiyo inazidi kupungua
kwa kasi ukilinganisha na awali.
Chanzo:Gazeti
la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 18 mwaka 2013
No comments:
Post a Comment