Header Ads

CCM HAITAAHIDI UONGO-DK.BILAL

Na Happiness Katabazi, Mtwara

MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Gharib Bilal, amesema chama chake hakipo tayari kutoa ahadi za uongo kwa wananchi katika kampeni zake zinazoendelea hivi sasa ili kipate kura.


Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Umoja mjini Mtwara ambapo alisema chama chake kitatoa ahadi na kutekeleza yale yaliyo ndani ya uwezo wake na si vinginevyo.

Akihutubia mkutano huo , alisema wapinzani wamekuwa wakijinasibu kwamba wakiingia Ikulu wataleta maendeleo zaidi ya CCM , huku wakibeza maendeleo kiliyoyafanya chama hicho.

“Hivi wana Mtwara, Mtwara ya mwaka 1960 ndiyo Mtwara ya sasa? CCM haiwezi kuahidi jambo isilo na uwezo nalo,” alisema Dk. Bilal.

Mgombea mwenza huyo aliwataka wananchi wa Mtwara wawasikilize viongozi wa CCM kwa umakini mkubwa huku akiwasisitiza kuwa wawasikilize wapinzani kwa nusu sikio na ikiwezekana wasiwasikilize kabisa.

Aliwataka wafuasi wa chama hicho kufanya kampeni za kistaarabu na kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kampeni kwani taifa lisipokuwa makini katika Uchaguzi Mkuu nchi inaweza kuingia kwenye machafuko yasiyo ya lazima.

Alibainisha kuwa mifano hai ya madhara ya vurugu za uchaguzi imeonekana kutoka nchi jirani, hivyo ni vema wananchi wakachukua tahadhari mapema.

“Nawaombeni mkimaliza kupiga kura rudini majumbani msubiri matokeo yatangazwe, ni lazima CCM itashinda, nchi yetu inasifika kwa amani na utulivu, tusikubali uchaguzi uwe mwanzo wa mfarakano.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 29 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.