Header Ads

KESI YA MRAMBA YASHIKA KASI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), Christine Shekidele(54), katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, ameimbia mahakama kuwa Kampuni ya Alex Stewart Bussiness Corporation ilikuwa haifuati sheria za kodi.

Mbali na Mramba, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Shekidele ambaye ni shahidi wa 13 wa upande wa jamhuri katika kesi , alitoa madai hayo mbele ya Jaji John Utamwa aliyekuwa akisaidiwa na Mahakimu Wakazi Sam Rumanyika na Saul Kinemela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Kiongozi wa Serikali Fredrick Manyanda.

Shekidele aliambia mahakama kuwa mwaka 2007 wakati akiwa na wadhifa huo pia alikuwa ni Kaimu Kamishna wa Kodi za ndani, na majukumu yake yalikuwa ni kuangalia utendaji wa makusanyo ya kodi za ndani na kujijbu mawasiliano na barua zitokazo nje ya Idara yake na kwamba kampuni hiyo ilikuwa haileti ripoti za mahesabu yake.

Hata hivyo Shekidele alianza kubabaika baada ya kubanwa maswali na wakili wa Mramba, Hurbert Nyange kwamba ana ushahidi gani kama zile ripoti za mahesabu za mwaka za kampuni hiyo ambazo zilitolewa na TAKUKURU kwa TRA kama kweli ni za kampuni hiyo.

“Mh! sikuziona hizo ripoti ya mahesabu ya kampuni hiyo.....aah waheshimiwa mahakimu naomba nibadili jibu langu la awali, nimekumbuka niliziona hizo ripoti ila sijui ni nani alizisaini...na sifahamu kama wakati TRA inaandaa ripoti hizo za mahesabu za kampuni hiyo sifahamu kama kampuni hiyo ilituma mwakilishi wake kushiriki kushirikiana na TRA kuandaa mahesabu hayo”alidai Shekidele.Kesi hiyo inaendelea kusikiklizwa tena leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 24 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.