Header Ads

MAHAKAMA YA KISUTU YALITUPA PINGAMIZI MURRO

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ilitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh mil. 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC1), Jerry Murro na wafanyabiashara wawili.


Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe, ambapo alisema baada ya kusikiliza malumbano ya kisheria yaliyoibuliwa na pande zote mbili juzi, amefikia uamuzi wa kutupilia mbali pingamizi za mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala, waliotaka mahakama hiyo ikatae kupokea kielelezo cha pili cha upande wa Jamhuri, kwa sabababu pingamizi hilo halina hoja za msingi.

Juzi Wakili wa Rweyongeza aliwasilisha pingamizi la kutaka kielelezo hicho ambacho ni picha za CCTV zinazomuonyesha mshitakiwa wa kwanza, Murro, Deogratius Mugassa na aliyekuwa Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage, wakiwa wanaingia na kutoka ndani ya Hoteli ya Sea Cliff, siku ya Januari 31 mwaka huu, saa 7:31 wakiingia katika hoteli hiyo na picha nyingine inaonyesha walitoka hotelini hapo saa 8:27 ya siku hiyo, kilichotolewa na shahidi wa pili wa upande wa mashitaka ambaye ni Meneja wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Hoteli ya Sea Cliff, Pounama Kumar, kwa madai kwamba picha hizo ni kivuli na si halisi.

Hakimu Mirumbe, alisema amefikia uamuzi wa kukubalina na hoja za Wakili Kiongozi wa Serikali, Boniface aliyeiomba mahakama hiyo ipuuze pingamizi la utetezi, kwa madai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 40A cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002, kinairuhusu mahakama kupokea ushahidi wa kielektroniki, video na redio unaomhusu mshitakiwa na wala kifungu hicho hakiizuii mahakama kupokea ushahidi wa aina hiyo ambao ni kivuli au halisi.

“Mahakama hii inatupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na linakubaliana na hoja za upande wa jamhuri, kwa sababu ni za msingi na ni za kisheria, hivyo mahakama hii inapokea picha hizo za CCTV kama kielelezo cha pili kilichotolewa na upande wa Jamhuri na inaahirisha usikilizaji wa kesi hii hadi Januari 17,18 na 19 mwaka kesho,” alisema Hakimu Mkazi Mirumbe.

Katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao wanadaiwa kula njama kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 13 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.