Header Ads

MAHAKAMA KISUTU KUPOKEA VIELELEZO KESI YA MURRO

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjini Dar es Salaam, imesema leo itatoa uamuzi wa kupokea au kutopokea kielelezo cha pili kilichotolewa na upande wa Jamhuri jana katika kesi ya kuomba rushwa ya sh mil. 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Jerry Murro na wafanyabiashara wawili.


Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe, alifikia uamuzi huo baada ya kuibuka malumbano makali ya kisheria baina ya pande hizo katika kesi hiyo. Upande wa utetezi unaowakilishwa na wakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala na kuiomba mahakama isipokee picha za CCTV zilizotolewa mahakamani hapo, kama kielelezo na shahidi wa pili wa Jamhuri ambaye ni Meneja Teknolojia ya Mawasiliano wa Hoteli ya Sea Cliff, Apaumr, kwa madai picha hizo ni kivuli na si halisi .

Kwa upande wake Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, aliomba mahakama ipuuze pingamizi hilo la utetezi, kwa madai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 40A cha Sheria ya ushahidi ya mwaka 2002, kinairuhusu mahakama kupokea ushahidi wa kielektroniki, video, redio unaomhusu mshitakiwa na wala kifungu hicho hakiizuii mahakama kupokea ushahidi wa aina hiyo ambao ni kivuli au halisi.

Awali shahidi huyo wa pili kabla ya kutoa kielelezo hicho cha picha ya CCTV ambazo zinawaonyesha washitakiwa hao wakiwa kwenye Hoteli ya Sea Cliff, Januari 29, mwaka huu, kipokewe mahakamani kama kielelezo.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Kiongozi wa Serikali, Boniface, shahidi huyo alieleza kuwa Februali 2, mwaka huu, meneja mkuu ambaye ni bosi wake alimuita ofisini kwake akimtaka aongozane na maofisa watatu wa polisi waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZDCO), Charles Mkumbo, awapeleke kwenye chumba maalumu cha kurekodi (CCTV) ili waweze kuangalia wageni waliofika kwenye hoteli hiyo siku ya Januari 28-31 mwaka huu.

Mbali na Murro, washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa, ambao Februari 15 mwaka huu, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama za kutaka kupokea rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashitaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashitaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 12 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.