Header Ads

MEMBE AMDUWAZA DK.BILAL

Na Happiness Katabazi, Lindi

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, juzi alimduwaza mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mohammed Gharib Bilal, baada ya kukamata kipaza sauti jukwaani na kuanza kuimba na kucheza wimbo wa kabila lake la Wamwela.


Tukio hilo la aina yake, ambalo lilivutia umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kumlaki Dk. Bilal kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mtama, Wilaya ya Lindi Vijijini, ambako mgombea mwenza huyo alitumia fursa ya kumnadi Membe, anayewania ubunge wa Mtama.

Kabla ya Dk. Bilal kupanda jukwaani kumnadi, Membe alitangulia na kushika kipaza sauti na kusema kuwa, yeye atamkaribisha jukwaani mgombea mwenza kwa kumuimbia wimbo wa kabila lao la Wamwela, uliokuwa na maneno yasemayo: “Pano Pano Palipanda, Pano Pano Palipanda,”. Membe alisema, wimbo huo una maana kwamba, hapo hapo ndipo alipotoka yeye.

Wakati Membe akiimba wimbo huo, huku akionekana kupandisha mzuka, vikundi vya ngoma vilikuwa vikimchagiza kwa midundo sambamba na alivyokuwa akiimba jukwaani kwa zaidi ya dakika tano, huku umati wa wananchi akiwamo Dk. Bilal na mkewe Asha Bilal wakiangua vicheko meza kuu, wasiamini alichokuwa akikifanya Membe.

Baada ya Membe kumaliza kuuimba wimbo huo huku akitokwa jasho, alisema ulikuwa una maana ya kumweleza Dk. Bilal kwamba, yeye ametokea Mtama si Dar es Salaam.

Kwa upande wake Dk. Bilal alivyopanda jukwaani, alianza kwa kubainisha kwamba inamuwia vigumu kuamini Membe yule anayemuona Dar es Salaam, ndiye aliyemuona Mtama akiwa jukwaani akiimba wimbo wa kwao bila kujivunga na kumpongeza kwa kumwimbia wimbo huo, kwani alipata burudani.

Aidha, Dk. Bilal akimnadi mgombea huyo ambaye amepita bila kupingwa jimboni humo, aliwaomba wananchi wa Mtama wampatie kura nyingi mbunge huyo, kwani katika uongozi wake ameweza kusimamia ujenzi wa zahanati kadhaa, ambazo hivi sasa zimeletewa magari ya kubebea wagonjwa, shule, maji safi na salama yanapatikana kwa uhakika jimboni humo.

Mkutano huo wa kampeni kufanyika jimboni hapo, ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa Dk. Bilal mkoani Lindi, leo ameanza kampeni mkoani Mtwara.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 29 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.