Header Ads

KAMISHNA TRA:MRAMBA HAKUITIA HASARA SERIKALI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), Christine Shekidele(54), katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake,amesema kampuni ya Alex Stewart Bussiness Corporation haijailetea serikali hasara.

Mbali na Mramba, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.Ambao kesi yao inasikilizwa na Jaji John Utamwa anayesahidiana na Hakimu Mkazi Sam Rumanyika na Saul Kinemela na wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbet Nyange, Elisa Msuya na Profesa Leonard Shahidi na upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili Kiongozi, Fredrick Manyanda na Ben Lincoln.

Shekidele ambaye ni shahidi 13, alitoa maelezo hayo jana wakati akijibu swali la wakili wa upande wa utetezi, Elisa Msuya alilomtaka aieleze mahakama kwamba endapo kampuni imepewa msamaha wa kutokulipa kodi na serikali kwa kufuata kanuni na sheria za nchi ,je kiasi hicho cha kodi alichosamehewa kitahesabika kuwa ni hasara kwa taifa?

“Kwa mujibu wa sheria za Kodi, pale serikali inapotoa msamaha wa kodi kwa kampuni husika , kile kiwango cha kodi kilichosamehewa katu hakiwezi kuhesabiwa kuwa kimeletea hasara kwa serikali, hivyo kampuni hiyo ya Alex Stewart ambayo Mramba aliidhinisha ipewe msamaha wa kodi na serikali yetu kwa ujumla ikakubali kutoa vibali vya kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kufuata sheria, nasisitiza serikali yetu haikupata hasara kwasababu kampuni hiyo ilisamehewa isilipe kodi.”alisema Shekidele.


Aidha Shekidele akijibu swali la Jaji Utamwa lilomtaka kuieleza mahakama mahakama kwamba juzi alieleza kuwa TRA ilikuwa haina kumbukumbu za ripoti ya fedha ya kampuni hiyo na iweje jana aimbie mahakama hiyo kuwa TRA inayo taarifa za fedha za kampuni hiyo, na ninani mwenye jukumu la kuandaa ripoti ya taarifa za fedha kodi za makampuni pale TRA?

“Mhh! Nikweli Jaji unavyosema lakini …toka mwaka 2004,TRA ilikuwa haina ripoti za fedha za kampuni hiyo lakini ilipofika mwaka 2007, TRA ndiyo ikapata ripoti za fedha za kampuni hiyo na TRA na hizo ripoti za fedha za kampuni hiyo zililetwa TRA na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk.Edward Hosea…..lakini hata hivyo mwenye jukumu la kuandaa taarifa za fedha za kodi ni mlipa kodi na msaidizi wake” alieleza Shekidele huku akionekana kubabaika babaika.

Shahidi huyo ni shahidi wa mwisho wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, ila upande wa utetezi umeiomba mahakama imuite shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ambaye alishatoa ushahidi wake ili afike tena mahakamani hapo ili upande wa utetezi uweze kumuhoji na mahakama hiyo ilikubali ombi hilo na kuairisha kesi hiyo hadi Desemba 17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na Januari 19-20 mwaka 2011 itakuja kwaajili ya kumalizia kusikiliza ushahidi wa shahidi wa kwanza.

Mbali na Mramba washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja ambao wanatetewa na mawakili wakujitegemea , Hurtbet Nyange, Elisa Msuya na Professa Leonard Shahidi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 25 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.