Header Ads

JK,BILAL WAENDELEA KUTOA AHADI

Na Happiness Katabazi

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete na mgombea mwenza wake, Dk. Mohamed Gharib, wameendelea kutoa ahadi mbalimbali katika mikutano yao ya kampeni.

Akimalizia ziara yake katika Mkoa wa Kagera, Kikwete amewaahidi umeme wa uhakika wakazi wa Ngara na maeneo jirani, kupitia mradi mkubwa unaoshirikisha nchi tatu utakaozalisha megawati 63 kutoka kwenye maporomoko ya Mto Rusumo yaliyopo wilayani humo.

Akizungumza na wakazi wa Ngara mjini, mgombea huyo alisema mradi huo unatarajia kuanza mapema mwakani baada ya taratibu za mwisho za kumpata mkandarasi kukamilika.

Alisema, kupitia mradi huo, tatizo la umeme litamalizika na kuzitaja nchi zitakazonufaika kupitia mradi huo kuwa ni Burundi, Rwanda na Tanzania ambapo kila moja itapata megawati 21 huku akifafanua kwamba umeme huo utaingizwa kwenye gridi ya taifa.

“Huu ni mradi mkubwa ambapo megawati 63 zitakazozalishwa hapo tutagawana… sisi tutapata megawati 21 na wenzetu kila mmoja atapata kama hizo. Napenda kuwa hakikishia ndugu zangu tatizo la umeme litakuwa limemalizika kabisa. Tuchagueni tuendelee kuwaletea maendele.

“Penye umeme maendeleo yapo. Nawaomba msiniangushe, juhudi zetu mmeziona,” alisema Kikwete aliyekuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa Ngara kwenye uwanja wa posta mjini hapa ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya mikutano ya kampeni zake mkoani Kagera.

Akizungumzia changamoto za maendeleo zinazoikabili serikali yake kwa upande wa elimu, mgombea huyo alisema mikakati ya kuhakikisha kuwepo kwa walimu wa kutosha inafanyika, ikiwa ni pamoja na kuwapatia ajira wahitimu wote wa fani ya ualimu ngazi ya shahada, wanaomaliza kwenye vyuo binafsi.

Rais Kikwete leo ataanza mikutano ya aina hiyo kwa siku mbili kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kigoma kabla ya kwenda Rukwa.

Kwa upande wake, mgombea mwenza, Dk.Mohamed Gharibu Bilal akiwahutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Ruangwa na Liwale, aliwataka wasomi kote nchini kuanzisha utamaduni wa kujenga makazi yaliyo bora ili taifa liweze kupiga hatua katika sekta ya makazi.

“Tunao mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata makazi bora. Mpango huu upo katika ilani ya ccm na ni imani yangu kuwa wananchi wakimchagua Rais Kikwete katika uchaguzi ujao, basi itakuwa kazi rahisi kwetu kufanikisha azima hii muhimu katika maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.

Katika kampeni hizo, Dk. Bilal pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kutambua kuwa serikali ya CCM imejipanga vema na kwamba ina kila sababu za kutaka kuwapa maendeleo zaidi ya hapo walipo. Mgombea mwenza huyo bado anaendelea na kampeni katika Mkoa wa Lindi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 27 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.