Header Ads

DK.SLAA AUKACHA USULUHISHI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kuendesha usuluhushi katika kesi ya madai ya kupora mke wa mtu inayomkabili aliyekuwa mgombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia chama (CHADEMA), Dk.Willbroad Slaa baada ya mdaiwa na wakili wake kutotokea mahakamani.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya usuluhishi lakini katika hali isiyotarajiwa mdaiwa huyo wala wakili wake Mabere Marando walishindwa kufika mahakamani hapo wala kutoa taarifa za udhuru.

Hali hiyo iliyomsababisha msuluhishi wa kesi hiyo(Jaji )Zainabu Muruke kusema kuwa kitendo hicho kimetafsiriwa na mahakama kuwa mdaiwa Dk.Slaa hayuko tayari kwaajili ya usulushi kwahiyo ataandika taarifa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage ili aweze kupanga jaji mwingine wa kuanza kuisikiliza kesi hiyo.
“Kutokana na mdaiwa (Dk.Slaa) na wakili wake Marando kutokufika leo(jana) mahakamani hapa kwaajili ya usuluhishi kama walivyokuwa wamekubali awali kushiriki katika meza ya usuluhishi tena bila hata kutoa taarifa ya udhuru , mahakama hii imetafsiri kitendo hicho kuwa mdaiwa hayupo tayari kwaajili ya usuluhishi na hivyo nitaandika taarifa kwa Jaji Mfawidhi ili aweze kupanga jaji mwingine kwaajili ya hatua zitakazofuata ili ianze kusikilizwa..”alisema Jaji Muruke.
Awali pande zote mbili katika kesi hiyo zilikubalina kushiriki katika meza usulushi na kwamba kama usuluhishi huo ukishindika , kila upande utaleta mashahidi wa nne pindi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Kisheria kesi za madai kabla haijaanza kusikilizwa kunakuwa na usuluhishi ambapo jaji ndie anakuwa msuluhishi na endapo mdaiwa akikubali madai anayolalamikiwa,kesi humalizikia hapo na endapo mdaiwa atakwepa kushiriki kwenye usuluhishi au akashiri kwenye meza ya usulushi lakini wakashindwa kufikia mwafaka kesi hiyo uendelea kusikilizwa mahakamani.

Katika kesi hiyo ya madai inayomkabili Dk.Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa (CHADEMA). Aminiel Mahimbo amemshitaki Dk. Slaa akidai kuwa amempora mke wake Josephine Mushumbusi na kuwa anamnadi katika majukwaa ya kisiasa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kuwa ni mchumba wake, hoja ambazo Dk .Slaa alizipinga katika majibu yake na kudai kuwa hakufahamu kuwa mwanamke huyo ni mke wa mtu.

Mahimbo anaomba mahakama imwamuru Dk.Slaa amlipe Sh.bilioni moja ikiwa ni fidia ya kudhalilishwa kiongozi huyo wa kisiasa. Mahimbo katika madai yake anadai kuwa Septemba 7, 2002 alifunga ndoa na mwanamke huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kijitonyama na wala ndoa yao haijawahi kuvunjwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Novemba 17 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.