Header Ads

UBAGUZI KATIKA CHAGUZI USILIVURUGE TAIFA

Na Happiness Katabazi

KWA takribani miezi miwili mwandishi wa safu hii nilishindwa kuwaletea makala kama ilivyoada kwasababu ya kuwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu, hapa nchini.


Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikizunguka nchini nzima na aliyekuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi(CCM), ambaye kwa sasa ndiye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Mohamed Ghalib Bilal ,nikiwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache tuliochaguliwa kuunda timu ‘Press Team Bilal 2010 Campaign’.

Namshukurumu mungu tumeweza kumaliza kazi hiyo salama na kurejea ofisini kwangu tayari kabisa kwaajili ya kuendelea kulitumikia taifa hili kupitia kalamu yangu.Hivyo nawaomba radhi wasomaji wangu kwa kushindwa kuwaletea makala kwa kipindi chote hicho.

Mbali na maelezo hayo leo katika safu hii, nitajadili kwakina mchakato mzima wa uchaguzi mkuu uliopita pamoja na makandokando yake.
Watanzania tumeuona uchaguzi mkuu wa 2010 ukimalizika kwa taswira ambayo ni ya mchanganyiko.Wapo waliofurahi kwa kuwa ama wameshinda ama wagombea wao wameshinda.

Lipo kundi jingine la walioshindwa ambao wao wameshindwa ama wagombea wao wameshindwa .Lakini hivyo ndivyo ilivyotazamiwa iwe katika mazingira ya kinyang’anyiro ambacho kinapelekea kupatikana kwa mshindi mmoja tu kati ya wengi.Kura moja ni ushindi na hiyo ndiyo falsafa ya ushindi .

Sasa uchaguzi mkuu ulimalizika hivi karibuni ni wa tatu kufanyika tangu vyama vingi vianzishwe hapa nchini Julai 1992.

Je, tukiondoa mazingira tuliyoyataja hapo juu, Watanzania tumejifunza nini cha kuweza kujivunia kuwa sasa tunaelekea kwenye demokrasia bora iliyokomaa?

Mosi; nililoliona ni kukosekana kwa mazingira bora ya kisheria ya uchaguzi huru na wa haki.Jambo hili ni kubwa kwasababu chanzo chake ni Katiba ya nchi ,ambacho ni kilio cha wananchi wengi tangu mwaka 1992.
Hatujapa Katiba mpya inayopiganiwa na wana mageuzi na wala hatujapata Katiba nzuri kutokana na viraka vinavyobandikwa mara kwa mara na watawala waliopo madarakani.

Hivyo hatuna Tume huru ya Uchaguzi , hatuna sheria inayoweka mazingira sawa ya ushindani wa vyama vya siasa na hatuna uwezeshwaji wa washiriki wa uchaguzi ili kuakikiasha kila raia ana faidi haki yake ya binadamu na Katiba ya kuchagua au kuchaguliwa.

Pili;uchaguzi wa mwaka 2010,umeonyesha udhaifu mkubwa wa misingi kitaifa tuliokuwa tunajivunia kuwa tunayo na tunaheshimu sana.Msingi wa kwanza ambao ufa wake umeshindikana kuzibwa katika uchaguzi huu ni udini.Ghafla baadhi ya wagombea wakuu na wafuasi wa vyama vya siasa hasa wa CCM na CHADEMA walijikuta wakirushiana makombora ya udini .Kila mmoja akimlaumu mwenzake akitumia udini kujipatia udini kujipatia ushindi.

Ni kweli kwamba katika nchi yetu wengi wetu tuna dini kwa hiyo ni vigumu kumpata mgombea asiye na dini.Lakini ni hatari dini inapotumika kama mbinu halali ya kusaka uongozi.

Hilo halina mjadala kuwa ni baya ,la kukemewa vikali na ni la aibu na lina hatarisha usala wa taifa.Ila wasiwasi wangu ni viongozi wanapaswa wawe mstari wa mbele kukemea pepo huyo wa udini ,baadhi yao walitumia mbinu hiyo ya ubaguzi wa udini katika kampeni zao na kufanikiwa kupata madaraka na kwakuwa wanasiasa hao wenye hulka za kinyang’au wamefanikiwa kisiasa kwa kutumia mbinu hiyo ambayo ina hatarisha usalama wa taifa letu.

Sasa tujiulize katika chaguzi nyingine za kiasa wanasiasa hawa wataacha kutumia mbinu hiyo hatari ya udini katika chaguzi nyingine za kisiasa ili waweze kutwaa tena madaraka ya kisiasa?

Tayari hivi sasa watu wanangojea kuona serikali itakayoundwa na Rais Jakaya Kikwete itakuwa na sura kutokana na balaa hilo la udini?.

Kila mara mteuaji atakapoweka usawa au uwiano wa kidini ,haina maana kwamba hatumii kigezo cha udini.
Tatu; ukabila,ukanda,sehemu anakotoka mgombeaji. Tanzania ni nchi mmoja na Watanzania ni taifa moja linalojitambua kuwa ni ndugu moja.

Pamezuka hatari kubwa ya watu kuulizana asili,koo,kabila zao,ukanda anakotoka au sehemu anapotokea mgombeaji.

Kwa hiyo imefika mahali sasa imekuwa nongwa mfano mgombea atokee Karagwe mkoani Kagera aje kugombea udiwani au ubunge jijini Dar es Salaam, au atoke mkoa wa Mbeya aende akagombee katika moja ya jimbo au Kata mkoani Tanga.Mgombea atakayeenda kugombea Tarime ataulizwa kabila na anatokea ukoo gani?
Kwa hiyo mgombea ubunge wa mfano jimbo la Ubungo,Kawe na majimbo mengi atapata ushindi kwasababu watu wengi wanaoishi katika majimbo wa kabila lake.

Hivi tangu lini tumeulizana makabila?Hata unapoenda kununua kiwanja ujenge nyumba ,kweli ni nani anauliza kwanza ni eneo gani watu wa kabila lake wanaishi wengi?

Huu ni puuzi na umaamuma.Na kama utamaduni wa aina hii utapewa nafasi uote mizizi ,kwa sababu tayari umeishaanza kuchipua, ni wazi hatuwezi kuamisha vijiji vyetu tulikozaliwa huko mikoani tukaviamishia Dar es Salaam.

Nne; jinsia , baada ya miaka 15 ya vyama vingi bado taifa letu halijaweza kuimarisha uwiano wa kijinsia katika siasa za nchi. Kwa hiyo wanawake hawajapewa nafasi katika fikra za kisiasa kwa wa wananchi kuwa ni watu wanaostahili kuongoza kwa hiyo tumezidi kuimarisha mfumo wa Viti Maalum badala ya kuimarisha mafunzo ya kiungozi kwa wanawake ili waweze kuwa na ushindani uliobora katika Nyanja ya siasa.

Kwa hiyo japo kuwa wanawake wenzangu wamekuwa wakidai kwamba Viti Maalum viongezwe hadi kufikia asilimia 50; uwiano huo hautuakikishii sisi wanawake uwezo endelevu wa kiungozi.

Hivyo inabidi turejee suala hili kwa kudai mafunzo ya kiuongozi kwa wanawake yatolewe katika shule za msingi , sekondari na vyuoni ili kuwaandaa wawe washindani bora katika mfumo wa sasa wa siasa za ndani na nje ya nchi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716-774494


Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumapili, Novemba 15, mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.