Header Ads

GIRE AIKANA RICHMOND KORTINI

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA, Naeem Adam Gire, anayekabiliwa na mashitaka ya kughushi hati ya nguvu ya kisheria na kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali kuhusu Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond LLC ya Texas, Marekani amekana kuwa miongoni mwa wakurugenzi wa kampuni hiyo na kwamba wala hakutoa taarifa za uongo.


Gire alikanusha tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake na upande wa Jamhuri katika kesi hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Walirwande Lema, muda mfupi baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Fredrick Manyanda, kumaliza kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza.

“Nakanusha mbele ya mahakama hii kuwa mimi si mkurugenzi wa kampuni hiyo ila nakubali kwamba mfanyabiashara anayeishi Marekani, Mohamed Gire, ambaye ni Mwenyekiti wa Richmond Development Company Limited, Liabilities Company (LLC), ni kaka yangu na mimi pia ni mfanyabishara ninayemiliki Richmond Internet Café iliyopo Mtaa wa Kipata nyumba Na.66 Dar es Salaam,” alidai Naeem Gire.

Manyanda aliendelea kueleza kuwa Machi 13, 2006, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Mohamed Gire, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Manyanda aliendelea kuieleza mahakama kuwa Juni 2006 hapa jijini, mshitakiwa huyo pia alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Mkuu huyo wa serikali Manyanda, aliendelea kuieleza mahakama kuwa Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Mohamed Gire, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Aidha, wakili Manyanda alisema baada ya mshitakiwa huyo kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola Oktoba 13 mwaka 2008, alikiri kutenda makosa hayo aliyoshitakiwa nayo mahakamani.
Hakimu Lema baada ya kusikiliza maelezo hayo ya awali aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 8 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani Januari 13 mwaka jana na Gire amefikishwa mahakamani ikiwa ni mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.