HEKO MAHALU,HEKO KORTI KUU
Happiness Katabazi
JUMATATU ya wiki hii, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, iliandika historia mpya katika tasnia ya sheria nchini, baada ya kutoa hukumu iliyotamka bayana kuwa kifungu cha 36(4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002, ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sambamba na hiyo, mahakama hiyo ilitoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku hiyo awe amefanyia marekebisho kifungu hicho ama sivyo mahakama hiyo itakitamka kifungu hicho ni batili.
Kifungu hicho kilikuwa kinatamka kila mwenye kushitakiwa au kutuhumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi ili apate dhamana ni lazima adhaminiwe kwa nusu ya kiwango anachotuhumiwa nacho.
Mfano, mtu mwenye kutuhumiwa kuiingiza hasara serikali ya sh bilioni 12 atatakiwa apatiwe au atoe dhamana ya sh bilioni sita, kinyume na hapo ataendelea kusota rumande.
Hukumu hiyo ya kesi ya kikatiba ya mwaka 2008, iliyofunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilitolewa Oktoba 5, mwaka huu, saa nane mchana na jopo la majaji watatu.
Jopo hilo lilikuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Agustine Mwarija na Projest Rugazia, ambaye hakuwepo mahakamani hapo wakati hukumu hiyo ikisomwa.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Jundu alisema kimsingi Mahakama Kuu inakubaliana na hoja za mawakili wa mlalamikaji (Mahalu), aliyekuwa akitetewa na mawakili mahiri wa kujitegemea, Alex Mgongolwa na Cuthbert Tenga kwamba kifungu hicho cha 36 (4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kinakwenda kinyume na Katiba ya nchi na kinaleta ubaguzi.
Alisema wanakubaliana na hoja za mawakili wa Mahalu, kwamba uwepo wa kifungu hicho unafanya mshitakiwa mwenye fedha ndiye apate dhamana na mshitakiwa ambaye hana fedha kutoweza kutimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo kuishia kusota gerezani.
Hata hivyo, Jaji Jundu alisema kwa mujibu wa Ibara ya 30 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama Kuu inapoona kifungu chochote cha sheria kinakiuka ibara za Katiba, ina mamlaka ya kutoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu kukifanyia marekebisho.
Hii ni kesi ya pili ya kikatiba kufunguliwa na wananchi katika mahakama hiyo hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwisho wa siku, wanashinda tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani.
Kesi ya kikatiba ilifunguliwa na kituo cha Haki za Binadamu, ambapo pia kituo hicho kilikuwa kikitetewa na wakili Alex Mgongolwa waliomba mahakama hiyo itamke takrima katika uchaguzi ni rushwa.
Mwaka 2006 Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za wakili Mgongolwa ambapo ilitamka Takrima ni rushwa na ikamwagiza Mwanasheria Mkuu akafanyie marekebisho katika kifungu hicho kinachoruhusu takrima katika Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985.
Mahalu, alilazimika kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, ikiwa ni muda mfupi baada ya mwaka 2006, kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya sh bilioni tatu, ambapo hata hivyo kesi hiyo usikilizwaji wake unashindwa kuendelea katika mahakama hiyo kwa sababu jalada la msingi la kesi hiyo lipo katika Mahakama ya Rufani nchini.
Mahalu aliwasilisha ombi la kuiomba mahakama hiyo ya juu nchini ifanye mapitio ya uamuzi uliotolewa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu (mstaafu), Juxon Mlai, ambaye alitupilia mbali ombi la Mahalu lililokuwa likiomba mahakama hiyo imuache huru kwasababu utaratibu wa kisheria haukufuatwa kabla ya yeye kufunguliwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa maelezo hayo hapo juu, napenda kutoa pongezi zangu za dhati Profesa Mahalu kwa moyo wake wa ujasiri wa kufungua kesi hiyo tena kwa kutumia gharama zake kwa kuwaweka mawakili mahiri.
Nawapongeza mawakili hao kwa kazi nzuri ambayo iliweza kuwashawishi Jaji Kiongozi Fakhi Jundu na wenzake kukubaliana na hoja zao na mwisho wa siku wakatoa hukumu ambayo nalazimika kusema itawasaidia wananchi wengi ambao watapatwa na mabalaa ya kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi .
Kwa wale wananchi ambao si waumini wa tasnia ya sheria au hawajawahi kufika mahakamani na kuona baadhi ya watu wanaokabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na mahakama inapowatamkia washtakiwa wa kesi za aina hiyo kwamba ili wapate dhamana ni lazima watoe nusu ya kiasi cha fedha wanachotuhumiwa kuiba au kusababisha hasara, naamini itawawia vigumu kuona uzito, maana na faida ya hukumu hii.
Vyombo vingi vya habari havijaipa uzito wa kipekee hukumu hii, kama vyombo hivyo vilivyokuwa vizipata uzito wa kipekee hukumu ya rufaa ya mgombea binafsi au kesi ya mauaji ya watu wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi, Abdallah Zombe na wenzake na kesi za wizi wa akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu (EPA). Na si vyombo vya habari peke yake pia jamii kwa ujumla na hizo taasisi zinazojinasibu kila kukicha kwamba ni taasisi za kiharakati za kutetea wanyonge na maskini.
Hili ni jambo la kusikitisha kama si la kushangaza kwani ndani ya jamii yetu hasa kwa sisi tunaotokea kwenye familia za kimaskini, kama si leo, basi kesho, mimi, wewe au mwingine tunaweza kujikuta mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi.
Tunaweza kuangukia katika mikono hiyo na baadaye kufikishwa mahakamani kwa kesi za uhujumu uchumi iwe tumetenda kweli kosa hilo au tumebambikiziwa kesi na mahakama italazimika kutumia kifungu hicho cha sheria ya uhujumu uchumi kwa ajili ya sisi maskini ndiyo tupate dhamana.
Nayaandika haya kwa hisia kali kwani kwa takriban miaka 11 sasa nimekuwa mwandishi wa habari za mahakamani hapa nchini, nimekuwa nikishuhudia wananchi wenzetu wakishindwa kumudu na kutimiza masharti ya dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Watu hawa wamejikuta wanaozea magerezani miaka nenda miaka rudi wakati kesi zikiendelea kuunguruma, tena kwa kasi ya mwendo wa kinyonga kiasi kwamba zinachukua mpaka miaka minne hadi kutolewa uamuzi.
Msingi mmoja wapo wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, unapiga marufuku mtu yeyote kuchukuliwa kuwa na hatia mpaka pale mahakama itakapothibitisha kuwa mtu huyo ana hatia. Sasa kwa msingi huo wa Katiba ni dhahiri kifungu hicho cha 36(4) cha Sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002, kinapingana na msingi huo wa Katiba ambayo ndiyo sheria mama.
Wakati mwingine hukumu za washitakiwa hao zinapotoka mahakama inawaachilia huru washitakiwa hao kwasababu mahakama hiyo haijaletewa ushahidi unaojitosheleza.
Lakini vyovyote iwavyo, nadiriki kusema kuwa uwepo wa rushwa unatokana na mfumo wetu dhahifu katika masuala ya utoaji haki.Tuna matatizo makubwa kwa wale tuliowakabidhi majukumu ya kupambana na rushwa kwani baadhi yao watendaji wake wanakubali kutumiwa vibaya na wanasiasa wenye hulka za kinyang’au, kula rushwa na kisha kubambikia kesi watu wasio na hatia.
Watu hao wasio na hatia wakishaburuzwa mahakamani hujikuta wanabanwa na masharti ya kifungu hicho kilichotamkwa na Jaji Jundu na wenzake kuwa kinakwenda kinyume na Katiba ya nchini.
Ni hatari kwa sheria kumkabidhi binadamu yeyote mamlaka makubwa kiasi hicho. Leo na kesho itakapotokea kwamba mtu alifikishwa kortini na kuswekwa gerezani kwa kunyimwa dhamana kwasababu ya masharti ya kifungu hicho cha sheria ya uhujumu uchumi, na baadaye kubainika hana hatia, ana kuwa amedhalilishwa na kutopetezwa muda wake mwingi.
Kwa bahati mbaya, wengi wetu bado hatujajifunza thamani ya uhuru wa binadamu wenzetu.
Ni vyema sheria zetu zibadilishwe ili wale wanaoonekana mapema upande wa Jamhuri hauna sababu ya kuwafungulia mashtaka walipwe fidia kwa sababu thamani ya uhuru na heshima ya binadamu ni kubwa kuliko kiasi cha fedha chochote kinachohusika kwenye hizo kesi za uhujumu uchumi.
Kwenye tasnia ya sheria tunasema hivi ‘ni afadhali wahalifu tisa waachiliwe huru kuliko mtu mmoja asiye na hatia kuwekwa hatiani’.
Aidha, nimalizie kwa kumpongeza Profesa Costa Mahalu kwa uzalendo wake wa kufungua kesi hiyo na kisha kushinda, matunda ya hukumu hiyo si yake pekee, ni ya Watanzania wote watakaopatwa na matatizo ya kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.
Nina matumaini kuwa hukumu hii itawasaidia wanafunzi wa fani ya sheria vyuoni kwani watatumia hukumu hiyo kujibu maswali kweye mitihani, pia ni faida pia kwa majaji, mahakimu na mawakili ambao sasa watalazimika kutumia hukumu kama kielelezo cha kuunga mkono hoja zao za kisheria na kuitumia kutolea maamuzi katika kesi mbalimbali.
Hukumu hii iwe ni changamoto kwetu sisi waandishi wa habari hapa nchini kwani tumekuwa na kasumba ya kuinung’unikia sheria ya magazeti kuwa ni moja ya sheria mbaya lakini tunashindwa kupiga hatua moja mbele ya kutafuta mawakili watusaidie kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Oktoba 10 mwaka 2010

No comments:
Post a Comment