Header Ads

WAKILI KESI YA ZOMBE AFARIKI DUNIA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Jasson Kaishozi katika kesi ya mauji ya wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelele Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP),Abdallah Zombe na wenzake nane amefariki dunia jana.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Elizer Feleshi alisema ofisi yake ilipata taarifa za kifo hicho jana mchana kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kwamba alikwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kumuona daktari, alipomaliza aliishiwa nguvu na kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

“Nikiwa kama DPP wa Tanzania na timu yangu wa waendesha mashtaka nchini, tumepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Kaishozi kwani alikuwa ni miongoni mwa mawakili mahiri wa serikali hasa kwa upande wa uendeshaji wa mashauri ya jinai,” alisema Feleshi kwa masikitiko.

Alisema taratibu za mazishi zinafanywa na mwili wa marehemu utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwao Bukoba Vijijini kwa mazishi. Hadi kifo chake Kaishozi alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Kanda ya Mbeya.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi
Agosti 17 mwaka jana, Jaji wa Salum Massati aliwaachilia huru washtakiwa wote kwa maelezo kuwa upande wa Jamhuri ambao ulikuwa ukiwakilishwa na marehemu Kaishozi, Mwipopo, Mgaya Mtaki, Mzikila umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo ambayo ilikuwa ikivuta hisia za watu wengi hapa nchini.

Kaishozi ambaye katika kesi ya Zombe alikuwa akisaidiana na mawakili wenzake wa serikali, Angaza Mwipopo, Mgaya Mtaki na Alexanda Mzikila ni wakili wa pili kufariki dunia katika kesi hiyo wa kwanza alikuwa wakili aliyekuwa akimtetea Zombe, Moses Maira.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.