Header Ads

MAHAKAMA YAMBWAGA HAMAD RASHID


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali ombi lilotaka mahakama hiyo itoe amri ya kuliita Baraza la Wadhamini wa Chama cha Wananchi(CUF) na wenzake waje wajieleze ni kwanini walikaidi amri ya mahakama na ni kwanini wasitiwe hatiani kwa kosa la kudharau amari ya mahakama ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na Mbunge wa Wawi(CUF), Hamad Rashid na wenzake 10.


Rashid na wenzake waliwasilisha maombi mahakamani hapo  Januari 10, 2012,na walikuwa wakiiomba mahakama  iwaite Wadhamini wa Cuf wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri ya mahakama hiyo kutokana na uamuzi wa Baraza la Taifa la Uongozi la Cuf kumfukuza uanachama Hamad na wenzake.

Katika ombi hilo walalamikaji hao walidai kuwa licha ya Baraza hilo kupata taarifa za kuwepo kwa amri hiyo ya mahakama ilitolewa saa tatu ya Januari 4 mwaka huu, kabla ya kikao cha cha Baraza la CUF kuanza, baraza hilo liliendelea na kikao chake na kufikia maamuzi ya kuwavua uanachama walalamikaji hao.

Mbali na wadhamini wa CUF, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni wajumbe wa Baraza Taifa la Uongozi la CUF.

Kwa hiyo walalamikaji waliomba  mahakama iwatie hatiani na kuwafunga jela wadhamini hao wa pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Uongozi la chama hicho akiwemo Makamu wa kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika maombi hayo, Rashid na wenzake walikuwa wakidai kuwa Baraza la Taifa la Uongozi la Cuf lilipuuza amri ya mahakama hiyo iliyolizuia kuwajadili wala kuwachukulia hatua zozote wakati wa mkutano wake wa Januari 4, 2012, mjini Zanzibar.

Hata hivyo Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Agustine Shangwa,alisema kuwa hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa baraza wadaiwa walipata amri hiyo.

Jaji Shangwa alisema kwamba ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa wadaiwa walipewa amri hiyo, lakini alisema kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa wadaiwa waliipata amri hiyo wakati likiendelea na mkutano wake kabla ya kutoa uamuzi wa kuwavua uanachama walalamikaji.

“Kwa sababu hiyo mahakama hii imeshindwa kuwaita wadaiwa hapa mahakamani waje wajieleze ni kwanini walikaidi amri ile ya mahakamana…hivyo basi natupilia mbali ombi la walalamijaji”alisema Jaji Shangwa.

Amri hiyo ya Mahakama kulizuia baraza hilo kuwachukuliwa hatua yoyote Rashid na wenzake ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa Januari, 2012 kufuatia maombi waliyoyawasilisha mahakamani hapo na kina Rashid, Januari 3, 2012, chini ya hati ya dharura.


Hata hivyo kwa mujibu wa mawakili hao, hata kama amri hiyo ingekuwa ni halali na hata kama ingekuwa na ushahidi kuwa iliwafikia wadaiwa kabla ya kutoa uamuzi wa kuwavua uanachama walalamikaji bado Mahakama Kuu haiwezi kuwachukuliwa hatua.

Mbali na Hamad Rashid wengine waliofukuzwa uanachama CUF ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma na Juma Saanane, wote wakiwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 29 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.