SHEIKH PONDA ABAKI RUMANDE
*Wenzake wapata dhamana,wengine 11 washtakiwa
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana iliwapatia dhamana washitakiwa 49 wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi na wizi wa mali za sh milioni 59, huku Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa, akiendelea kusota rumande.
Hatua ya Ponda kuendelea kusota gerezani inatokana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP), Dk.Eliezer Feleshi, kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana ya mshitakiwa huyo kwa kile alichokieleza kuwa kwa ajili ya maslahi ya taifa.
Hata hivyo ,wakati watuhumiwa hao 49 wakipatiwa dhamana,watu wengine 11 waumini wa dini ya Kiislamu wamefikishwa mahakamani hapo jana, wakikabiliwa na makosa mawili ya kukaidi amri ya Jeshi la Polisi, iliyowataka wasifanye mkutano na kuvuruga amani.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Victoria Nongwa nduye alitoa dhamana kwa mshitakiwa wa 2-50 kwa kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya sh milioni 59 mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd inayomkabili Sheikh Ponda na wenzake.
Hakimu Nongwa ambaye jana washitakiwa hao walikuja mbele yake kwaajili ya kuakikisha kama wametimiza masharti ya dhamana ambayo yalitolewa na hakimu huyo Novemba Mosi mwaka huu, wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajawa ambapo alitoa masharti ya dhamana na kusema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini bondi ya milioni moja ambapo.
‘Nimelidhika washtakiwa wote mmetimiza masharti ya dhamana hivyo nawapatia dhamana hivyo mtakuwa nje kwa dhamana na kwamba dhamana hiyo haitamhusu mshitakiwa wa kwanza yaani Ponda ambaye dhamana yake imefungwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi”alisema Hakimu Nonga na kuairisha kesi hiyo hadi Novemba 15 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali.
Kupewa dhamana kwa shitakiwa hao 49, kuna mfanya Ponda peke yake aendelee kusota rumande licha makosa yanayomkabili yanadhaminika ila kwasababu DPP ,Dk.Feleshi, Oktoba 18 mwaka huu, aliwasilisha mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana ya Ponda peke ya kwaajili ya usalama na maslahi ya taifa.
Kuhusu washtakiwa wapya, wakili Mwandamizi wa serikali Shadrack Kimaro mbele ya hakimu mkazi Liad Chamshama aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Salum Shabani,Salum Mkulega,Ernest Silvester,Josephat Alocye,Edwin Sadoki,Stanley Nhonya,Athumani Sajuki,Thabit Kombo,Abdully Rashid na niga Ndiganga.
Wakili Kimaro alidai shitaka la kwanza ni la kudharau amri halali ya Jeshi la Polisi kinyume na kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kwamba Novemba 2 mwaka huu, huko Mtaa wa Tandamti katika Msikiti wa Idrisa jijini Dar es salaam, washitakiwa hao waikaidi amri hiyo waiyopewa na jeshi la polisi iliyokuwa ikiwakataza washitakiwa hao wasifanye mkusanyiko wowote.
Wakili huyo wa serikali alilitaja shitaka la pili kuwa ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifuncha cha 74 na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 vinavyosomwa pamoja na vifungu vya 43,41,45 na 46 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 .
Kuwa mnano Novemba 2 mwaka huu, eneo la mtaa wa Tandamti katika Msikiti wa Idrisa ,washitakiwa hao wakiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu walifanya mkusanyiko haramu ambao ulisababisha kuvuruga amani katika eneo hilo na upelelezi bado haujakamilika.
Hata hivyo washitakiwa hao walikanusha mashitaka hayo na Hakimu Shamshama alisema ili mshitakiwa apate dhamana nilazima awe na wadhamini wawili toka ofisi zinazotambuliwa na serikali ambapo kila mdhamini atasaini bondi ya milioni tano lakini hata hivyo washitakiwa hao walipelekwa mabusu kwasababu ya kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana hadi Novemba 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Novemba 8 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment