Header Ads

RUFAA YA DPP V JERRY MURRO KUANZA KUSIKILIZWA LEO




Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Novemba 28 mwaka huu, inatarajia kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyotolewa Novemba 30 mwaka jana , ambayo ilimwachilia huru aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Murro na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi kula njama na kuomba rushwa ya Sh milioni 10 .

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama kuu, inaonyesha Jaji Dk.Fauz Twaib ndiye amepangwa kuisikiliza rufaa hiyo na itaanza kusikilizwa leo asubuhi. 

Awali Februali 5 mwaka 2010, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi katika ofisi ya (DPP), marehemu  Stanslaus Boniface alidai kuwa  hati ya mashitaka ilikuwa na jumla ya mashitaka matatu, ambapo shitaka la kwanza ni la kula njama kinyume cha kifungu namba 32, shitaka la pili ni kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage, kinyume cha kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambalo wanadaiwa kulitenda Januari 29, mwaka 2010.

Shitaka la tatu ambalo linamkabili mshitakiwa wa pili, Edmund Kapama ‘Dokta’ na mshitakiwa wa tatu, Deogratius Mugassa, ni kudai kuwa wao ni maofisa wa Takukuru kinyume cha kifungu cha 100 B cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambacho kinasomwa pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2002.

Dadika chache baada ya Hakimu Moshi kumaliza kutoa hukumu yake Novemba 20 mwaka huu, wakili wa serikali katika kesi hiyo ambaye alikuwa ni  Mkurugenzi Msaidizi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, marehemu Stanslaus Boniface, akizungumza na gazeti hili  na alisema  Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini inayoongozwa na Dk. Eliezer Feleshi haijaridhika kabisa na hukumu hiyo na kwamba jana siku hiyo hiyo  saa saba mchana aliwasilisha  hati ya kusudio la  kukata rufaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye alikata rufaa katika mahakama kuu kupinga hukumu hiyo kwa madai kuwa mahakama hiyo ilikosea kisheria kuwaachilia huru washtakiwa hao na kwamba upande wa jamhuri ulikuwa umeleta ushahidi ambao unatosha kuwatia hatiani washtakiwa.

Februari 5, mwaka 2010, washitakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka hayo ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa Michael Wage, mashitaka ambayo waliyakana na kwa wakati wote huo hadi jana kesi hiyo ilipotolewa hukumu washitakiwa hao walikuwa nje kwa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 28 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.